BAADA ya Serikali kubuni na kufanikiwa
kuanzisha na kuendesha usafiri wa treni jijini Dar es Salaam, sasa
inajipanga kubinafsisha usafiri huo unaosaidia kupunguza msongamano.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, alisema hayo bungeni jana,
wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa
fedha 2013/2014.
Alisema Serikali inakamilisha mchakato wa kumpata mwekezaji na mwendeshaji wa huduma hiyo jijini humo.
Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, Kampuni
Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), ndiyo itakayokamilisha
mchakato wa kumpata mwekezaji na mwendeshaji wa huduma hiyo,
atakayetumia miundombinu ya reli iliyopo na vichwa vya treni na mabehewa
maalumu ya usafiri katika miji.
Dk Mwakyembe alisema mwitikio wa
wananchi kutumia huduma ya treni ya abiria, umekuwa mkubwa
ikilinganishwa na uwezo wa kutoa huduma yenyewe, hususan nyakati za
mahitaji makubwa ya usafiri.
Wingi wa abiria Kwa sasa kwa mujibu wa
Dk Mwakyembe, treni hiyo ya jijini Dar es Salaam, inabeba watu 14,000
kwa kila siku, sawa na zaidi ya daladala 467 zenye uwezo wa kubeba
abiria 30 kila siku.
“Kwa upande wa Tazara, wastani wa idadi
ya abiria wanaosafiri kwa treni kwa siku, umefikia 9,000 baada ya
kukamilika kwa ukarabati wa mabehewa mengine saba na kichwa kimoja cha
treni na kuanza kutumika rasmi Mei 9, 2013.
“Aidha, kwa upande wa TRL, wastani wa
abiria wanaosafiri kwa siku ni 5,000,” aliongeza Dk Mwakyembe
akizungumzia usafiri huo ulioanza Oktoba mwaka jana, kati ya Stesheni na
Ubungo Maziwa na kati ya Tazara na Mwakanga.
Faida, changamoto Alisema kuanzishwa kwa
usafiri huo wa treni jijini Dar es Salaam, kumesaidia kumepunguza idadi
ya magari barabarani.
“Kuanza kwa usafiri huu, kumeshawishi
baadhi ya wananchi waliokuwa wanatumia magari binafsi kuja katikati ya
Jiji la Dar es Salaam, kuanza kutumia usafiri wa treni,” alisema Dk
Mwakyembe.
Alizitaja baadhi ya faida zingine
zinazotokana na usafiri huo, kuwa ni kupungua kwa matumizi ya mafuta,
muda unaotumika barabarani na hivyo kusaidia wananchi kufika kwa wakati
katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
Alisema Wizara inaendelea kuzifanyia
kazi changamoto mbalimbali zilizojitokeza, zikiwamo za kutokuwa na mfumo
thabiti wa kukusanya mapato, uchakavu wa miundombinu na uhaba wa injini
na mabehewa.
Kuhusu kuongeza huduma za usafiri huo,
alisema Wizara imeunda Kamati Maalumu chini ya uenyekiti wa Naibu Waziri
wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba, ili kuchambua, kuainisha na kushauri
mipango na mikakati ya kuboresha na kupanua usafiri huo.
Ruti mpya “Pia Wizara inaangalia
uwezekano wa kuanzisha huduma maalumu ya treni kati ya Stesheni ya Dar
es Salaam na Gongo la Mboto kwa ajili ya kuhudumia abiria wanaopita
kwenda Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere,” alisema Dk
Mwakyembe.
Kwa upande wake, Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Miundombinu ilishauri kuwa ili mradi huo ufanye kazi kwa
ufanisi na kuondokana na hasara, Serikali iharakishe kununua angalau
treni mbili za kisasa na maalumu kwa safari fupi, ambazo gharama yake ni
Sh bilioni 8 kila moja
Post a Comment