Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mhe. Seif Shariff Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Waziri;
Balozi Ombeni Sefue, Katibu Mkuu Kiongozi;
Makatibu Wakuu;
Dkt. Philip Mpango, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango;
Washirika na Wadau wa Maendeleo;
Viongozi wa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma;
Viongozi wa Kidini na Sekta Binafsi;
Wataalamu Elekezi kutoka PEMANDU na Mckinsey;
Washiriki wa Maabara;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana:
Napenda
kuchukua fursa hii kuwakaribisha wote katika Warsha ya Wazi kuhusu
mfumo mpya unaoanzishwa na Serikali wa ufuatiliaji na tathmini ya
utekelezaji wa miradi ya kitaifa ya kipaumbele. Warsha hii inatoa
nafasi ya pekee kwa wananchi kushiriki na kutoa mawazo yao jinsi ya
kuboresha mfumo huo unaopendekezwa. Ni Warsha ya kuelimishana,
kubadilishana mawazo na kufahamishana mipango na mambo ambayo Serikali
inatarajia kuyafanya katika siku za karibuni.
Namshukuru
Balozi Ombeni Sefue, Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Philip Mpango, Katibu
Mtendaji wa Tume ya Mipango, viongozi na watumishi wote wa Tume ya
Mipango kwa kuandaa Warsha hii mahsusi. Kwa namna ya pekee nawashukuru
pia wataalamu wa PEMANDU na McKinsey kwa kushirikiana vizuri na wataalam
wetu katika kila hatua ya safari hii ambayo Serikali yetu imeianza.
Ndugu Wananchi;
Kupanga
na kutekeleza mipango ya maendeleo sio jambo geni hapa nchini. Ni
jambo ambalo tumelifanya tangu tupate Uhuru na tunaendelea nalo.
Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius
Nyerere, ilianza na Mpango wa Kwanza wa Maendeleo mwaka 1961 – 1964.
Mpango huo uliainisha maadui watatu wa maendeleo ambao ni umaskini,
ujinga na maradhi. Mikakati mbalimbali na mipango madhubuti ya
maendeleo ilibuniwa ili kupambana na maadui hao. Baada ya hapo ukaja
Mpango wa Maendeleo wa Miaka 15 wa mwaka 1964 – 1980, uliokuwa
umegawanywa katika vipindi vitatu vya utekelezaji vya miaka mitano
mitano.
Baadhi yenu mtakumbuka kuwa utekelezaji wa vipindi viwili vya mwanzo ulikuwa wa kuridhisha.
Hata hivyo, utekelezaji wa kipindi cha mwisho cha Mpango ule, yaani
kati ya mwaka 1975 – 1980, ulikuwa duni mno. Utekelezaji wake
ulivurugwa sana na changamoto za wakati ule kama vile kupanda sana bei
ya mafuta, kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (1977) na Vita ya
Kagera. Mambo haya yalisababisha fedha zetu nyingi kutumika kuagiza
mafuta, kujenga taasisi zetu wenyewe na kutetea mipaka ya nchi yetu.
Rasilimali kidogo tuliyonayo ikaenda huko badala ya kugharamia miradi ya
maendeleo.
Ndugu Wananchi;
Pamoja
na changamoto zilizojitokeza, Serikali iliamua kuanzisha mpango
mwingine wa maendeleo wa muda mrefu wa mwaka 1981 – 2000. Kwa bahati
mbaya mpango huo nao haukutekelezwa kufuatia kuendelea kudorora kwa
uchumi. Kati ya mwaka 1981 na miaka ya 90 mwanzoni, Serikali ilianza
kufanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi. Tukawa na National Economic
Survival Programme (NESP) mwaka 1981 – 82 na Structural Adjustment
Programme (SAP) mwaka 1982 – 1985. Mipango hiyo haikutekelezwa vizuri
kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa rasilimali za
kutosha. Kati ya mwaka 1986 – 89, Serikali kwa kushirikiana na Mfuko wa
Fedha wa Kimataifa (IMF) ikaanza kutekeleza programu ya kwanza ya
kufufua uchumi (ERP – I). Ya pili ikafuatia kati ya mwaka 1989 – 1992.
Mwaka
1994 Serikali ikaanza kuandaa mpango wa maendeleo wa muda mrefu
utaowezesha kuzikabili changamoto mpya kufuatia mageuzi ya kiuchumi na
kijamii yaliyokuwa yanaendelea nchini na duniani kwa ujumla. Kazi hiyo
ilikamilika mwaka 1999 na kuzinduliwa kwa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya
2025. Malengo ya Dira hiyo ni kuleta maendeleo ya haraka nchini na
kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Maana
yake ni kwamba wananchi wawe na chakula cha kutosha, huduma ya elimu na
afya iliyo bora iwafikie watu wengi zaidi, vifo vya watoto na akina
mama vipungue, wastani wa kuishi uongezeke, maji safi na salama
yapatikane kwa wote, uhalifu upungue na umaskini uliokithiri usiwepo
kabisa na pato la wastani la Watanzania liwe zaidi ya dola za Kimarekani 3,000. Vile vile pawe na maendeleo ya viwanda, matumizi ya teknolojia na sayansi yaongezeke, miundombinu ipanuke na uchumi ukue kwa asilimia 8 au zaidi.
Ndugu Wananchi;
Juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali za awamu zote ikiwemo na hii ninayoiongoza mimi zimeleta mafanikio ya kutia moyo. Kwa mfano, uchumi wa nchi umekua kwa wastani wa asilimia 7 kwa miaka kumi iliyopita, mfumuko wa bei upo chini ya asilimia 10,
mapato ya ndani yameongezeka, mauzo ya nje yameongezeka na hifadhi ya
fedha za kigeni imeongezeka pia. Hata hivyo, idadi ya Watanzania walio
maskini bado ni kubwa hususan umaskini wa kipato. Vile vile bado
hatujafanikiwa kufikia malengo katika maeneo mengi tuliyojiwekea. Hata
tathmini ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2025 tuliyofanya mwaka 2000
imethibitisha hivyo. Hatuendi kwa kasi inayotakiwa na utekelezaji wake
siyo wa kuridhisha. Matokeo yake tupo nyuma ya hatua tuliyotakiwa
kuwa. Kwa mfano, kwa upande wa safari ya kuelekea pato la wastani la
watu kuwa dola 3,000 mwaka 2025, tulitakuwa tuwe tumefikia dola 995 mwaka 2010. Lakini ilikuwa tumefikia dola 545 tu. Kwa ukuaji wa uchumi, tulitakiwa tuwe asilimia 8, lakini tulikuwaasilimia 7.
Zipo
changamoto nyingi za ndani na nje, zilizofanya tusifikie malengo hayo:
Kubwa ni misukosuko ya uchumi wa dunia, uhaba wa rasilimali fedha na
ufuatiliaji mdogo katika utekelezaji wa miradi iliyoainishwa kuleta
maendeleo. Aidha, mipango na mikakati ya maendeleo ilikuwa na vipaumbele
vingi kwa wakati mmoja wakati rasilimali za utekelezaji wake ni
kidogo. Hali hii haikutuwezesha kujielekeza ipasavyo kwenye maeneo
yenye kuleta matokeo makubwa na kwa haraka.
Ndugu Wananchi;
Baada ya kutafakari yote haya, tukafikiria namna ya kuweza kufikia malengo yetu ya Dira ndani ya muda uliobakia.
Hivyo, tukaamua kuja na Mpango ya Maendeleo wa Muda Mrefu wa Miaka 15
ambao utatekelezwa katika awamu tatu za miaka mitano mitano. Katika
Mpango wa Kwanza Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12-2015/16), maeneo
yaliyopewa kipaumbele ni Miundombinu, Kilimo, Viwanda, Huduma za jamii
na Uendelezaji Rasilimali Watu na Utalii, Biashara na Huduma za Fedha.
Changamoto kubwa ikabaki kuimarisha mfumo wetu wa kusimamia utekelezaji
wa mipango ya maendeleo ili kuleta matokeo ya haraka. Kuendelea kufanya
vilevile tulivyokuwa tukifanya kusingeweza kuleta mabadiliko tuliyokuwa
tunayataka katika utekelezaji wa mipango yetu. Ilibidi tubadilike,
ikiwezekana tukimbie pale ambapo wengine wanatembea.
Ndugu Wananchi;
Tukiwa
katika hali hiyo ya kutafakari cha kufanya, mwezi Mei, 2011 ikawa
bahati mimi kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa “Langkawi International
Dialogue” uliofanyika mjini Kuala Lumpur, Malaysia. Katika mkutano huo,
Serikali ya Malaysia iliwasilisha mada jinsi inavyoendesha na kusimamia
utendaji wake ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo na huduma kwa
jamii. Mimi na viongozi wenzangu tuliohudhuria mkutano huo tulivutiwa
sana na mfumo wa utendaji wa Malaysia na tukadhamiria kujifunza zaidi
kutoka kwao. Tukaomba watusaidie. Bahati nzuri Serikali ya Malaysia
ikakubali ombi letu na kuandaa warsha maalum mwezi Novemba, 2011.
Ujumbe wa Tanzania kwenye warsha hiyo ya aina yake uliongozwa na Dkt.
Philip Mpango. Waliporudi, tukaamua kuwa na sisi tuanze kutumia
utaratibu wa Malaysia wa “Matokeo Makubwa Sasa” ama kwa Kiingereza “Big
Results Now”.
Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa mfumo wa
“Big Results Now” hapa nchini ulianza kwa kuainisha maeneo sita yenye
uwezo wa kutupatia matokeo makubwa kwa haraka. Maeneo hayo ni nishati,
elimu, maji, miundombinu, kilimo na utafutaji fedha. Kazi ya kuchagua
maeneo sita ya kwanza nayo haikuwa rahisi. Tulibishana sana katika
kuchagua vipaumbele vichache lakini vyenye kuleta matokeo makubwa.
Hatimaye tukafanikiwa. Vipaumbele hivi vinabeba msingi wa kufungulia
fursa za ukuaji uchumi wa Tanzania kwa ujumla na kuchochea ustawi wa
maisha bora kwa wananchi.
Hatua ya pili ikawa ni kufanya uchambuzi wa kina kupitia awamu ya kwanza ya maabara (lab) kama alivyoeleza Katibu Mkuu Kiongozi. Kazi hiyo ilitekelezwa kwa wiki sita mfululizo na wataalam wetu zaidi ya 300 kutoka nyanja
na sekta mbalimbali na kukamilika tarehe 05 Aprili, 2013. Nawapongeza
sana kwa kazi hiyo kubwa na moyo wao wa kujitolea. Tumeandaa ratiba ya
utekelezaji kwa kila mradi na programu ikionyesha kazi zilizopangwa
kufanywa, mtekelezaji-husika na muda na kukamilisha kazi.
Katika
mfumo huu, Mawaziri na Watendaji katika Wizara na Idara watapimwa kwa
vigezo vilivyo wazi na ninyi wananchi mtapata fursa ya kuvijua vigezo
hivi pamoja na matokeo ya upimaji. Hapatakuwa na siri. Hii itarahisisha
usimamizi wa utendaji kwa maana Waziri au Katibu Mkuu atajifunga yeye
mwenyewe kimaandishi na ataweka saini yake kwenye vigezo ambavyo
atapimwa navyo na wananchi mtashuhudia matokeo ya upimaji huo.
Ndugu Wananchi;
Ili kuweza kuratibu vyema
shughuli za ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika
mfumo huu mpya, nimeunda chombo maalum kitakachokuwa chini ya Ofisi
yangu ambacho kitajulikana kama President’s Delivery Bureau (PDB). Kazi zake za msingi zitakuwa ni pamoja na: kupanga na kuendesha shughuli za uchambuzi wa kina wa kimaabara (labs); kuandaa
mikataba ya kupima utendaji kazi wa Mawaziri kwenye miradi na programu
za maendeleo katika wizara zao; kwa kushirikiana na Tume ya Mipango
kuishauri Serikali kuhusu maeneo machache ya kipaumbele yenye kuleta
matokeo ya haraka (National Key Results Areas); kusaidia sekta binafsi
kuwekeza kwenye maeneo hayo; na kufanya tathmini huru ya utendaji kwa
viongozi wote hususan Mawaziri katika utekelezaji wa maeneo muhimu ya
kitaifa.
Ndugu Wananchi;
Tumefanya
kazi kubwa sana ya kuandaa na kuainisha maeneo ya kimkakati na
kuyaandalia programu za kina kwa ajili ya utekelezaji. Lakini tumeona ni
vyema kuwashirikisha wadau na wananchi katika jambo hili kubwa. Ndio
maana tupo hapa kuhakikisha kuwa wananchi kwa ujumla wenu mnapata fursa ya kuchangia katika miradi na programu hizo kwa maendeleo ya taifa letu na watu wake.
Ndugu Zangu;
Sitapenda kuongea sana hivyo basi nataka niwape nafasi wananchi na wadau wengine mliofika hapa kupita katika eneo la kila
maabara na kupata maelezo ya kina kutoka kwa wataalam. Muwe huru
kuuliza maswali, kujenga hoja, kutoa maoni na kukosoa na kuboresha
katika kila maabara. Baada ya kupata maoni yenu ndipo tutaboresha na
kwenda kuyafanyia kazi maoni na ushauri wenu.
Ndugu Wananchi;
Baada ya kusema hayo, napenda kutamka kuwa Warsha ya Wazi imefunguliwa rasmi. Ninawatakia majadiliano mazuri na uchangiaji mzuri.
Asanteni kwa kunisikiliza
Post a Comment