Na Lydia Churi, MAELEZO-DODOMA
Serikali
itaendelea na mpango wake wa kusafirisha gesi asilia kutoka mkoani
Mtwara, Lindi hadi Dar es Salaam. Waziri wa Nishati na Madini Prof.
Sospeter Muhongo (pichani) ameliambia bunge leo mjini Dodoma alipokuwa
akiwasilisha bajeti ya wizara yake ya mwaka wa fedha 2013/2014.
Alisema
mradi wa kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es salaam
utahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilometa 532 ambapo bomba
hilo litakuwa na uwezo wa kusafirirsha futi za ujazo za gesi asilia
milioni 784 kwa siku.
Alisema
mradi huo utaigharimu Serikali shilingi bilioni 1,960 ambapo kazi za
usanifu wa mradi na ulipaji wa fidia kwa wananchi wapatao 3,092
waliopisha maeneo ya mradi zimekamilika. Hatua za awali za ujenzi wa
mitambo ya kusafisha gesi asilia zimeanza.
Waziri
Muhongo alisema kutokana na mradi wa gesi asilia wananchi wa mikoa ya
Lindi na Mtwara watapata manufaa mbalimbali yatokanayo na mradi huo
ikiwa ni pamoja na tozo ya asilimia 0.3 ya mauzo ya gesi asilia, huduma
za jamii kama vile zahanati, shule, umeme, maji na mafunzo katika vyuo
vya ufundi (VETA) na sekondari.
Wakati huo huo,
Serikali imefanikiwa kukamata madini yenye thamani ya shilingi bilioni
13.12 kati ya mwezi Oktoba 2012 na April 2013 yaliyokuwa yakisafirishwa
nje ya nchi kinyume na sheria.
Waziri
wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo ameliambia bunge leo mjini
Dodoma kuwa wahusika wameshachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa
sheria ya Madini ya mwaka 2010.
Alisema
katika kuimarisha usimamizi wa biashara ya madini nchini, Serikali
kupitia wakala wa madini (TMAA) imeanzisha madawati maalum ya kukagua
madini yanayosafirishwa nje ya nchi kupitia viwanja vya ndege vya
kimataifa vya Dar es salaam, Kilimanjaro na Mwanza.
Wizara
ya Nishati na Madini imeomba kuidhinishiwa na Bunge zaidi ya shilingi
trilioni moja ambapo asilimia 90 ya fedha hizo ni kwa ajili ya maendeleo
na asilimia 10 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Aidha Fedha za
ndani ni asilimia 56.27 na za nje ni asilimia 43.73.
Post a Comment