Na Hassan Hamad,
OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim
Seif Sharif Hamad, amesema dhamira ya msingi ya ukombozi wa Zanzibar kupitia
Mapinduzi ya Januari 12, 1964, ni Zanzibar kuweza kujitawala yenyewe na kuwa na
mamlaka kamili.
Maalim Seif ameeleza hayo katika ukumbi wa
salama hoteli ya Bwawani, wakati akifungua kongamano la pili la kitaifa
linalohusu Maridhiano ya Wazanzibari.
Amesema dhamira hiyo ya Mapinduzi ilianza
kukiukwa baada ya kutiwa saini kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao
uliipunguzia Zanzibar mamlaka yake.
Amesema wakati Wazanzibari wanapodai kuwa na
mamlaka kamili wanatetea haki na maslahi ya nchi yao, na kwamba hakuna sababu ya
kubezwa wala kupuuzwa.
Amefahamisha kuwa akiwa ni kiongozi wa
Zanzibar, atasimamia na kutetea mawazo ya wazanzibari waliowengi katika kupata
haki zao za msingi ndani na nje ya Zanzibar.
Akifafanua zaidi kuhusu msimamo wake amesema
hiyo haina maana kuwa Wazanzibari hawataki Muungano, bali wanataka kuwepo kwa
Tanzanyika na Zanzibar zenye mamlaka kamili, halafu kuwepo na muungano wa
mkataba, ili kila nchi iweze kuendesha mambo yake kwa uhuru.
“Kuwa na mamlaka kamili sio kwa maslahi ya watu
wachache bali kwa watu wote, ni kama mvua, yaani inaponyesha mimea yote
inanawirika”, alifafanua Maalim Seif na kuongeza,
“Tunataka kurejesha heshima ya nchi yetu, tuwe
na sera na Wizara yetu ya mambo ya nje, bendera yetu ipepee nchi za kigeni,
Umoja wa Mataifa na Jumuiya nyengine za Kimataifa zikiwemo Jumuiya ya Madola,
Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki”.
Amewataka wanakongamano hao kuwaongoza wajumbe
wa mabaraza ya katiba katika kutetea maoni na maslahi ya Zanzibar.
Akizungumzia kuhusu mafanikio ya maridhiano
amesema yamerejesha umoja wa wazanzibari na kuondosha uhasama na chuki miongoni
kwa wananchi.
Ameipongeza kamati ya maridhiano chini ya
Mwenyekiti wake Mzee Hassan Nassor Moyo kwa kazi kubwa wanayoifanya katika
kuyaendeleza maridhiano hayo na umoja wa wazanzibari.
Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ambaye
ni mwanasiasa mkongwe wa Zanzibar Mzee Hassan Nassor Moyo amesema maridhiano
hayo yaliyoasisiwa na Rais Mstaafu wa Zanzibar dkt. Amani Abeid Karume na Katibu
Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, yameondoa fitna na chuki zilizodumu kwa
muda mrefu miongoni mwa wananchi.
Amesema kamati yake inaisubiri kwa hamu kubwa
rasimu ya Katiba mpya itakayotolewa, ili waweze kuichambua kuona kama
imezingatia maoni ya wananchi na maslahi ya Zanzibar.
Akiwasilisha mapendekezo ya kamati hiyo Mzee
Moyo amesema kila nchi katika Muungano inapaswa kuwa na uraia wake, sera yake ya
mambo ya nje na Muungano uwe na JINA la “Muungano wa Jamhuri za Tanzania” au
“United Republics of Tanzania”.
Chanzo: zanzinews.com
Chanzo: zanzinews.com
Post a Comment