Markus Mpangala |
Ziara ya Barrack Hussein Obama inaelekea kuwagusa wengi mno.
Baadhi yetu tunaguswa na idadi ya watu watakaokuwepo kwenye ziara hiyo, ambao ni
700. Wengi wanajaribu kujiuliza ni kwanini Obama akae siku 4 nchini Tanzania.
Lakini kwangu mimi muhimu sio siku zake atakazokuwepo hapa wala idadi ya watu
atakaoambatana nao. Jambo muhimu kwangu ni Tanzania.
Naam, rais mstaafu George
Bush alikaa hapa siku kama hizo hizo. Lakini wengi walidhani matokeo ya ziara
yake ni siku chache ama zaidi. Sasa Obama anakuja, haendi Kenya, bali anakuja
Tanzania. Hata hivyo tuendelee kufikiri zaidi kibiashara,uchumi na ushindani wa
siasa za kimataifa baada ya ujio wa Xi Jinping.
Jambo muhimu kwetu ni kuangalia namna gani tutaweza
kuzungumza na Obama katika masuala ya kibiashara na ushindani wa kimataifa
kuhusu siasa na uwekezaji. Hatuwezi kuketi chini na kulalamika kuwa Obama
anakuja na wageni wengi ambao hawana msaada kwetu. Lazima tutambue kuwa ujio huu
unaitambulisha kwa namna nyingine nchi yetu ya Tanzania katika ulimwengu.
Wengi watakuwa
wakijiulzia kwanini Rais huyo amekuja Tanzania na sio sehemu nyingine. Ni kweli
kwamba Obama atakuwa na ziara katika maeneo mengine ambako anatarajiwa
kuzungumza na viongozi mbalimbali. Katika mfumo wa siasa za kimataifa, ujio wa
Barrack Obama ni mbinu ya kujaribu kufukuzana na China ambayo ilishamleta Rais
wake Xi Jinping.
Rais huyo wa China
aliihutubia dunia akiwa nchini Tanzania na alitumia lugha yao ya kichina. Sio
hilo tu bali pia Rais huyo aliingia mkataba na nchi yetu ambayo mojawapo ni
ujenzi wa bandari ya Bagamoyo ambapo China itakuwa msimamizi kwa kipindi cha
miaka 50.
Kwa namna nyingine
mkataba huu unaleta kizazi zaidi ya kioma kilichopo hapa nchini. Kwamba kizazi
kijacho kitaachiwa urithi unaoonekana hivyo kuona manufaa ya uhusiano wa China
na Tanzania. Kwa upande wa Obama, ziara yake lazima itakuwa na masuala ya sera
za uchumi na kutengeneza njia ya maslahi yake kama ambavyo George Bush alifanya.
Kwahiyo ili kufanikisha yote haya lazima tukubaliane
tunahitaji kushirikiana na wengi kote duniani hata kama washirika wetu wana
desturi ya kuwa walaghai au kuwa na ksumba za kuwa nduli kama Idd Amin. Ili
tuweze kuitangaza zaidi nchi yetu tunahitaji fursa kama hizi kujitokeza. Lazima
tukubali tutaingaza nchi yetu mwaka huu kwa namna mbili kuu ambazo ni ujio wa Xi
Jinping na Barrack Obama.
Lakini ujio huu sio kitu
ambacho mwananchi anaweza kudhani sadaka bali anachojua ni wazi kuna maslahi
yanafukuziwa hapa ambapo watanzania wana mali nyingi katika ardhi na mengineyo.
Wananchi wanataka kujua ni ajenda gani ambazo tutaweza kuzungumza na Obama, au
mwingine yeyote atakayekuja.
Tunafahamu ushindani
uliopo kwa upande wa Mashariki ya Kati ambako mataifa haya ya China na Marekani
yanajaribu kujenga misingi yao na kulinda maslahi yao. Sisi tunaonekana kuwa
washirika wazuri wa mataifa haya. Lakini ingefaa zaidi nitoa angalizo kuwa
katika ushirika huu lazima tukubaliane kuchukua hatua stahiki ili kuleta manufaa
kwa wananchi wetu.
Sidhani kama tunahitaji
kuelezwa mengi katika misingi yoyote iwe kijeshi, kiuchumi, kisiasa na
kadhalika, yatupasa kuona kile ambacho tunatakiwa kukiona. Obama anakuja kulinda
maslahi na kuendeleza misingi iliyoasisiwa na Bush. Obama anakuja kuwakilisha
nchi yake, asilani tukaeti chini na kudhani tabasamu lake litakuwa la huruma
kwetu.
Tunafahamu kuwa Marekani
imejeruhiwa sana kiuchumi na inahitaji kujipanga na kuendeleza utawala wake
kiuchumi. Kuna hali ya wazi kabisa afrika kuwa kitovu cha sera za nchi za
mataifa mbalimbali kwahiyo hakuna njia ya mkato ambayo inatutweza kupata manufaa
kama hii ya kuzungumza nao tukiwa na ajenda zenye maana mezani.
Lazima tujitarishe na kuamini kuwa ulinzi wa maslahi yetu
ni jambo lenye maana sana hivyo hakuna sababu ya kuogopa kuweka sera zetu wazi
mbele ya Obama na timu yake ya watu 700. Hakuna sababu yoyote ya kuhofia ujio
huu kwanini kwa namna nyingine unaikumbusha dunia kuwa kuna taifa linaitwa
Tanzania.
Ziara ya wkanza ya Obama
akiwa Rais aliifanya nchini Ghana, ambako alizungumzia mengi sana. Sasa kwanino
Obama ameichagua Tanzania? Lazima tukiri kuwa Ghana ni miongoni mwa nchi zenye
ushawishi mkubwa sana kwa afrika magharibi ukiacha Nigeria hususani masuala ya
uchumi na demokrasia. Kwa upande wetu Tanzania ni nchi yenye ushawishi mkubwa
katika ukanda wa kusini mwa janwga la sahara.
Tanzania ni miongoni mwa
nchi ambazo zinasimama mstari wa mbele kulinda maslahi ikiwemo kuendeleza
misingi ya waasisi wa SADC. Tanzania ni nchi yenye ushawishi mkubwa sana katika
ukanda huu na moja ya mambo yatakayojadiliwa sina shaka kabisa kuhusua hali ya
Zimbabwe. Hali ya Zimbabwe sote tunaifahamu, na kwa eneo la kisiasa sina shaka
kabisa itakwua moja ya ajenda za Obama katika ukanda wa kusini mwa jangwa la
sahara.
Ni wazi Jacob Zuma hana
ushawishi wowote mbele ya Robert Mugabe ndiyo maana alisuswa alipotembelea
Zimbabwe. Ni Tanzania ndiyo ilifanikisha uelewano chini ya Rais Kikwete ambaye
akiwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika alifanikisha timu ya Rais Thabo Mbeki wa
Afrika kusini kumaliza mzozo wa taifa hilo. Kwa maana hiyo watanzania lazima
tukae chini na kuwahimiza watawala wetu wajipangie ajenda za msingi katika
maongezi yao na Obama.
Lazima tukubali pia Obama anakuja kulinda maslahi ya nchi
yake. Hakuna sababu zozote za kuficha hisia zetu, bali tuwahimize na kuwaambia
twahitaji kuweka sera za wazi na zenye maslahi kwa taifa letu. Nafikiri yale
yaliyoandaliwa na watawala wetu kuzungumza na Obama yanapaswa kuongezwa kwa
kiwango chochote kile, ambacho iwe zaidi ya uwekezaji. Muhimu ni kusubiri ajenda
yetu itakayowezeshwa na watawala wetu na kuinufaisha Tanzania.
CREDITS: MARKUS MPANGALA
Post a Comment