Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif
Sharif Hamad akizungumza na balozi wa Canada nchini Tanzania Alexandre Leveque,
ofisini kwake Migombani.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif
Hamad akiongozana na balozi wa Canada nchini Tanzania Alexandre Leveque, baada
ya mazungumzo yao yaliyofanyika ofisini kwake Migombani.Picha na Salmin
Said-Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais-
--
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif
Hamad ameihakikishia Canada kuwa Zanzibar ina maeneo mazuri ya kuwekeza na
kuwaomba wawekezaji wa nchi hiyo kuja kuwekeza katika Nyanja tofauti zikiwemo
ujenzi wa hoteli kubwa za kitalii, kumbi za mikutano na uvuvi wa bahari
kuu.
Amesema Zanzibar ina mahitaji makubwa ya uwekezaji
katika maeneo hayo, na kwamba hatua hiyo itasaidia kukuza uchumi wa taifa na
kunyanyua kipato cha wananchi.
Akizungumza na balozi wa Canada nchini Tanzania balozi
Alexandre Leveque ofisini kwake Migombani, Maalim Seif amesema serikali imelenga
kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuwawezesha wawekezaji wa ndani na nje
kuja kuwekeza miradi mbali mbali ya kiuchumi.
Aidha Maalim Seif ameiomba nchi hiyo kuangalia
uwezekano wa kuleta wataalamu wa Afya na walimu wa sayansi, ili kupunguza tatizo
la wataalamu hao nchini.
Amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta
hizo, lakini bado zina upungufu wa wataalamu wakiwemo madaktari wenye sifa,
pamoja walimu wa masomo ya sayansi.
Amesifu mchango wa nchi hiyo hasa katika sekta za afya
na elimu na kutaka isichoke kutoa misaada yake katika kusaidia kunyanyua uchumi
wa Zanzibar.
Kwa upande wake balozi Alexandre amesema Canada imekuwa
ikihamasisha wawekezaji binafsi, na kuahidi kuwahamisha kuja kuwekeza
Zanzibar.
Kuhusu upatikanaji wa wataalamu wa Afya na walimu wa
Sayansi, balozi huyo amesema atawasiliana na mamlaka zinazohusika, ili kupata
wataalamu wakiwemo wa kujitolea, watakaoweza kuja kufanya kazi katika maeneo
hayo.
Amesema Canada inajivunia uhusiano wa muda mrefu uliopo
kati yake ya Zanzibar, na kwamba uhusiano huo utaendelezwa kwa maslahi ya pande
hizo mbili.
Na
Hassan Hamad
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais
Zanzibar
Post a Comment