Dar es Salaam. Kuna kila dalili kwamba wabunge wa CCM wameanza kupanga majeshi kwa lengo la ‘kumalizana’ watakapokutana kwa siku mbili mfululizo na mwenyekiti wa chama hicho tawala, Rais Jakaya Kikwete.
Mkutano huo unaotajwa kuwa zao la jitihada za Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana unatarajiwa kufanyika kesho na keshokutwa mjini
Dodoma, huku kukiwapo taarifa kwamba wabunge wamegawanyika katika
makundi kwa lengo la kupenyeza, kisha kutetea hoja walizonazo dhidi ya
wenzao.
Miongoni mwa hoja zinazotajwa ni ile ya kushughulikiwa kwa wabunge ambao
wamekuwa wakitajwa kwamba ni wapinzani ndani ya CCM, wakiwamo,
Alphaxard Kangi Lugora (Mwibara), Deo Filikunjombe (Ludewa), Ally Keissy
Mohamed (Nkasi Kaskazini) na Luhaga Mpina (Kisesa).
Wabunge hao wanatuhumiwa na wenzao kwamba wanawasaidia wapinzani
kutokana na misimamo yao ya kuikosoa hadharani Serikali katika vikao na
mikutano tofauti ya Bunge.
Itakumbukwa kuwa Aprili 25 mwaka huu baada ya kukwama kwa Bajeti ya
Wizara ya Maji, wabunge wa CCM walikutana katika kikao cha dharura
kilichoongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambako Lugola na
Filikunjombe walishambuliwa kutokana na kile kilichodaiwa kwamba
wamekuwa wakiidhalilisha Serikali ya CCM bungeni.
Habari zilidai kwamba waliowashambulia wabunge hao ni wenzao, Saidi
Nkumba (Sikonge) na Livingstone Lusinde (Mtera), huku wakitetewa na
Beatrice Shellukindo (Kilindi) na Peter Serukamba (Kigoma Mjini) ambao
walikaririwa wakisema kwa nyakati tofauti kwamba hawajakosea chochote
kwani wanaeleza hali halisi ilivyo.
Baada ya mjadala huo, Pinda alikaririwa akimwelekeza Katibu wa Wabunge
wa CCM, Janister Mhagama kumwandikia barua Katibu Mkuu wa CCM, Kinana
kuhusu suala hilo ili liwe ajenda watakapokutana na Rais Kikwete.
Hata hivyo, kuna taarifa kwamba huenda hoja hiyo ikakosa nguvu kutokana
na msimamo wa sasa wa Kinana ambaye anawaona wabunge wa CCM kama ni
wapole, hali inayosababisha wale wa vyama vya upinzani hasa Chadema
kupata nguvu.
Kutokana na hali hiyo, ni dhahiri kwamba Rais Kikwete atakuwa na wakati
mgumu wa ama kukubaliana na hoja za wale wanaokosoa wenzao kwa kuikosoa
Serikali au kuegemea upande wa Kinana ambaye kimsingi anaunga mkono
ukosoaji unaofanywa na wabunge.
Harufu ya kile kinachodaiwa kuwa ni maandalizi kwa ajili ya mkutano huo
ilianza kunukia jana pale Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipomtaka Lugola
kuwasilisha ushahidi wa majina ya mawaziri aliodai kwamba wanajihusisha
na biashara ya dawa za kulevya, ili ayafikishe kwa Rais Kikwete kwa
hatua zaidi.
“Kila mtu anatakiwa aipime kauli yake kabla hajaitamka, kama Lugola ana
ushahidi aulete mbele ya Bunge na tutayapeleka kwa Rais,” alisema Pinda
wakati akijibu swali la Mbunge wa Tumbe, Rashid Ally Abdallah aliyesema
anaamini hakuna waziri anayejihusisha na biashara hiyo kwani mchakato wa
kuwapata hufanywa kwa umakini wa hali ya juu.
Abdallah alikuwa akirejea kauli iliyotolewa na Lugola mwezi uliopita
kwamba atawasilisha bungeni majina ya watendaji wa Serikali wanaopokea
rushwa ili kuficha majina ya mawaziri wanaojihusisha na dawa za kulevya
na kwamba kauli hiyo ni nzito inayolidhalilisha Bunge.
Pinda ambaye alikuwa akijibu maswali ya papo kwa papo alisema licha ya
kwamba anaheshimu kauli ya kila mbunge, Lugola anatakiwa kuleta ushahidi
kamili na majina ya mawaziri.
Kuulizwa kwa swali hilo kunatafsiriwa na wachunguzi wa mambo kwamba
inaweza kuwa moja ya maandalizi ya kwenda ‘kuwashtaki’ Lugola na wenzake
mbele ya Rais Kikwete kwamba wamekuwa wakiichafua CCM na Serikali yake.
Chimbuko la mkutano
Habari ambazo gazeti hili limezipata zinadai kuwa chimbuko la mkutano wa
Rais na wabunge wa CCM ni madai yao ya muda mrefu ambao mara kadhaa
wameeleza kutoridhishwa na mambo yanavyokwenda serikalini.
Hoja kubwa ya wabunge ni matumizi mabaya ya vikao vya wabunge wa chama
hicho (party caucus) ambavyo wanadai vimekuwa vikitumiwa na Serikali
kuwabeba kwa kuwasafisha na kuwatetea watendaji wabovu serikalini,
wakiwamo mawaziri wasiokuwa na uwezo.
“Malalamiko haya ni ya muda mrefu, wanadai (wabunge) kwamba vikao vyao
vinaitishwa tu pale kunapokuwa na mpango wa kuiokoa Serikali bungeni,
lakini hakuna vikao vingine ambako wanakaa kwa ajili ya kuishauri
Serikali yao,” kilisema chanzo chetu na kuongeza:
“Lakini pia wanalalamika kwamba hata hao watendaji wa Serikali
wanaowatetea bungeni hawako makini na wala Serikali haiwachukulii hatua
zozote wanaendelea tu kuharibu.”
Chanzo hicho kilidai kuwa wabunge wa CCM wanaona kwamba kwa kutetea uozo
ulio dhahiri mbele ya umma, wamekuwa wakiyaweka majimbo yao rehani na
kuonekana kama watu wasio na uwezo mbele ya wapiga kura wao.
Habari hizo zinasema kuwa ajenda nyingine ni kusuasua kwa miradi mingi
ya maendeleo, ajenda ambayo imejikita katika mgawanyo wa rasilimali za
nchi usiozingatia vipaumbele vya maendeleo na ufujaji wa fedha za umma.
Wabunge hao wanadaiwa kwamba wanarejea maelezo ya mawaziri katika bajeti
ambayo yanaonyesha kwamba hadi robo tatu ya Mwaka wa Fedha 2012/13,
wizara nyingi zilikuwa hazijapokea hata nusu ya fedha zilizoidhinishwa
na Bunge ilhali takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zikionyesha
kuwa kiasi kikubwa cha fedha kimekusanywa na wakati mwingine kuvuka
malengo yaliyowekwa.
“Wabunge wanahoji fedha za nchi zinakwenda wapi? Maana kama TRA
wanakusanya fedha kwa asilimia 108 halafu fedha hazifiki kunakohusika
maana yake kuna tatizo kubwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali (Hazina),”
kilisema chanzo kingine kutoka ndani ya CCM.
Juzi, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema kikao
hicho kitatoa nafasi zaidi kwa wabunge kueleza masuala yanayohusu
utekelezaji wa Ilani ya CCM katika majimbo yao.
Licha ya Nape kusema kwamba kikao hicho hakitahusu yale yanayotokea
katika mkutano wa sasa wa Bunge la Bajeti, ni dhahiri kwamba masuala
hayo hayaepukiki hasa ikizingatiwa tofauti za wazi miongoni mwa wabunge
wa CCM.
Kadhalika, suala la kutotekelezwa kwa ahadi za Rais wakati wa kampeni za
2010 linaweza kuibuka kwani ni jambo ambalo limekuwa likijitokeza
katika mijadala kadhaa ya wizara zilizowasilisha bajeti zake bungeni.
chanzo:mwananchi
Post a Comment