Na Zawadi Msalla na Lydia Churi-MAELEZO- DODOMA
Serikali
iko katika hatua za awali za uanzishwaji wa benki ya Vijana ya Taifa
ambapo hivi sasa unafanyika uchambuzi wa michanganuo (Proposal)
iliyowasilishwa katika hatua za kumpa mshauri mwelekezi.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Prof. Elisante Ole Gabriel alisema tayari taasisi tisa za kitaalamu zimeshajitokeza na kuwasilisha michanganuo yake.
Prof.
Ole Gabriel alisema msingi wa kuanzishwa kwa benki ya Vijana unatokana
na muendelezo wa kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana
ulioanzishwa katika mwaka wa fedha wa 1993/94.
Alisema
Mfuko huo umeshakopesha zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kwa SACCOS za
vijana kati ya mwaka 2009 na 2012,fedha ambazo kwa kiasi kikubwa
zimewasaidia vijana kuinua hali zao za kiuchumi.
Alisema
nia ya Serikali kutaka kuanzisha benki ya vijana si kujipatia faida kwa
kufanya biashara bali lengo kubwa ni kutaka kubadili hali ya maisha ya
vijana (economic status) ili kuwafanya vijana waweze kukabiliana na hali
ngumu ya maisha.
Alisema
benki hiyo itakuwa tofauti na benki nyingine kwa kuwa yenyewe itakuwa
ikitoa mikopo maalum kwa ajili ya vijana pekee. Aliongeza kuwa vijana
wanapofikisha umri wa miaka 35 hubaki kama wateja wa kawaida.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi huyo, benki ya vijana itaongeza utambuzi kwa
vijana kwenye mfumo wa uchumi kwa kuwa itakuwa ikitoa mafunzo ya moyo na
mbinu za ujasiriamali ili vijana waweze kulipa mikopo watakayokopeshwa.
Wakati
huo huo Idara ya vijana imeanzisha kanzidata (database)
itakayowawezesha kufahamu vijana wako wapi, wanafanya nini na wanashauri
nini kifanyike ili kuboresha maendeleo ya vijana. Katika hili, Idara
ilisambaza madodoso maeneo mbalimbali nchini.
Alisema
vijana 4699 tayari wameshajibu madodoso hayo kuonyesha wako wapi na
mikoa ya Singida na Tanga ndiyo inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya
vijana walioitikia zoezi hilo. Aliipongeza mikoa hiyo na kuitaka mikoa
mingine kuiga mfano huo.
Alisema
mpaka sasa vikundi 176 vimeshawasilisha taarifa zake na kati ya hivyo
vikundi 98 vimesajiliwa na vikundi 76 havijasajiliwa.
Post a Comment