Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

SIRI ZA VURUGU ZA MTWARA HII HAPA

• Brigedia Ngwilizi avilaumu vyombo vya dola, serikali


na Edson Kamukara, Dodoma

SIRI za mzozo wa gesi mkoani Mtwara, imeelezwa kuchangiwa na udhaifu wa serikali pamoja na vyombo vya dola, Tanzania Daima Jumapili limedokezwa.

Mzozo huo ambao tayari umeshasababisha vifo, maafa na madhara makubwa ya uharibifu wa mali na baadhi ya watu kuachwa majeruhi, unadaiwa kutokana na uzembe wa serikali kupuuza hoja za msingi za wananchi wa Mtwara, pamoja na vyombo vya dola, hasa Idara ya Usalama wa Taifa kutokuwa makini katika kubaini mipango ya vinara wa mzozo huo.

Ingawa Bunge limeunda kamati teule kwenda kuchunguza chanzo cha vurugu hizo, taarifa za kiintelijinsia zinataja makundi makubwa matatu kwamba yako nyuma ya vurugu hizo.

Makundi hayo ni pamoja na wanasiasa, serikali, polisi, vyama visivyo vya kiserikali na wadau wengine wa ndani na nje.

Tayari Jeshi la Polisi linamshikilia kinara aliyekuwa akisambaza karatasi za kuchochea vurugu hizo.

Lawama kwamba vyombo vya dola na viongozi wa serikali wamechangia kutokea kwa hali hiyo, zimekuwa zikitolewa kila kona na hata bungeni jana.

Katika vurugu za juzi, baadhi ya wananchi wa Mtwara waliitahadharisha serikali kabla, kwamba wangepinga hotuba ya Waziri wa Nishati na Madini kama haitajibu maswali yao.

“Serikali, vyombo vya dola vikapuuzia. Wakaahirisha mpango huo baada ya waziri kuahirisha hotuba yake. Waliposikia hotuba ya waziri itasomwa siku nyingine, siku moja kabla wakatoa tahadhari hiyo hiyo. Serikali, vyombo vya dola vikashindwa kudhibiti, leo madhara yametokea ndio wanakimbia kama hawajui,” kilisema chanzo chetu cha habari.

“Ni kweli kwamba Mtwara na sehemu nyingine za nchi zimekuwa nyuma sana kimaendeleo.


“Ni vema na ni busara, na kwa kuwashirikisha wazee wa Mtwara, kuwa Wana Mtwara wakasikilizwa. Kuna mambo ya msingi ambayo Wana Mtwara na serikali wanaweza kukubaliana kwenye meza ya mazungumzo, lakini kwa muda wote serikali imepuuzia na leo inakumbuka shuka wakati kumekucha,” alisema mmoja wa wabunge kutoka mkoani humo.

Mmoja wa mawakili maarufu nchini, ambaye hakutakakutajwa jina gazetini, alisema ni aibu kwa kitengo cha usalama wa taifa kushindwa kubaini na kuzuia vurugu hizo, kwani zilijulikana mapema kwamba zingetokea.

Alisema inashangaza kwa wataalamu wa idara hiyo na polisi kuwa mabingwa wa kubaini uvunjifu wa amani katika mikutano ya hadhara ya wapinzani, na kushindwa kubaini suala hili ambalo maandalizi yake yanahusisha umma mpana.

Kwa mtazamo wa wakili huyo, idara ya usalama na polisi zimekuwa dhaifu kwa kuwa zimegeuzwa vitengo vya CCM, kwani kazi kubwa wanayofanya sasa hivi ni jinsi ya kunusuru CCM dhidi ya wapinzani na wakosoaji wake; jambo ambalo alisema ni aibu kwa taifa, na hatari kwa usalama wa nchi.

Brigedia Ngwilizi anena

MBUNGE wa Mlalo (CCM), Brigedia Jenerali mstaafu Hassan Ngwilizi ameishambulia serikali ya chama chake akisema kuwa badala ya kudhibiti vurugu zisitokee nchini, imegeuka kufanya kazi ya waandishi wa habari.

Ngwilizi alitoa kauli hiyo jana wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2013/2014 na kuainisha kuwa kazi ya serikali ni kudhibiti vurugu wakati waandishi wa habari ni kuripoti kilichotokea.

Ingawa Ngwilizi hakutaja eneo husika, lakini ni dhahiri kwamba alikuwa akiwalenga baadhi ya wakazi wa mkoani Mtwara ambao walifanya vurugu kubwa hivi karibuni na kuteketeza mali, wakipinga ujenzi wa bomba la gesi asilia unaotekelezwa na serikali.

Alisema kuwa kazi ya serikali ni kutumia vyombo vya dola kuwasaka wahusika na kuwachukulia hatua bila kujali nyadhifa zao wala uwezo wao, lakini kinyume chake serikali inakuja kutoa taarifa baada ya fujo kutokea.

Kauli ya Ngwilizi inakuja zikiwa ni siku tatu tangu Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi kutoa taarifa bungeni kuhusu vurugu zilizotokea Mtwara Mei 22 mwaka huu, pamoja na kuainisha hasara ya mali iliyopatikana.

Katika tamko hilo la serikali, Nchimbi alisema wahusika watasakwa popote, iwe ndani na nje ya Mtwara ama nje ya nchi na kuwafikisha kwenye mkono wa dola, hatua ambazo Ngwilizi alisema zilipaswa kuchukuliwa mapema.

Akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM) naye aliwatahadharisha wabunge wenzake akisema kuwa wasiombe majimboni mwao wawe na madini ya dhahabu kwa kuwa watapata adha kama wanayoipata wananchi wa Kahama kutoka kwa wawekezaji.

Alisema kuwa wawekezaji wamewatelekeza wananchi huku serikali ikikaa kimya.

Lembeli alihoji ni kwanini mgodi wa Buzwagi unaweza kuwasha umeme kwa saa 24 bila kukatika, huku wananchi wa Kahama mjini, kilomita chache kutoka ulipo mgodi, wakikatiwa nishati hiyo kila mara.

Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige, aligusia sakata la vurugu za Mtwara akisema ni ujumbe kwa serikali kuwa Watanzania wagawane rasilimali kadiri zinavyopatikana.

Alisema kwenye maliasili maeneo yenye rasilimali hizo yanabaki na mrabaha huku akitolea mfano Tume ya Jaji Mark Bomani kuwa ilipendekeza kwamba eneo lenye mgodi libakiwe na mrabaha asilimia 40 na ile 60 ndiyo iende maeneo mengine.

“Maeneo yenye madini, gesi, vivutio vya utalii hawafurahii kuona madini yao yanakwenda kujenga miji ya mataifa mengine wakati wao wakiachiwa mashimo,” alisema.

Bajeti yapitia, gesi lazima itoke

Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ambayo ilikuwa imeahirishwa kupisha vurugu za Mtwara, hatimaye jana imepitishwa na Bunge kiaina huku Spika Anne Makinda, akiwazima wabunge waliotaka kushika mshahara wa waziri.

Akihitimisha hoja za wabunge, Waziri Prof. Sospeter Muhongo alifafanua faida ambazo zitapatikana kama nchi na wakazi wa mikoa ya kusini kwa ujumla ilipo gesi asili, na kusisitiza kuwa rasilimali hiyo lazima itoke kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kuchochea uchumi.

“Bila umeme vijijini hakuna maendeleo na hata dira ya Maendeleo ya Taifa 2015 hatuwezi kuifikia bila kuwa na nishati ya uhakika,” alisema.

Alisema kuwa kwa sasa serikali inatumia fedha nyingi kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme, lakini akabainisha kuwa iwapo ujenzi wa bomba la kusafirishia gesi hiyo utakamilika, nishati hiyo itakuwa nafuu.

“Waheshimiwa wabunge mnaweza kuona mathalani tangu tumesaini mkataba huo Septemba mwaka jana hadi Mei 22 mwaka huu, zilipoibuka vurugu huko Mtwara, tumetumia kiasi cha dola za Marekani milioni 596.49 kununua mafuta mazito ya mitambo,” alisema.

Waziri Muhongo aliongeza kuwa kuanzia Juni mwaka huu hadi Desemba mwaka 2014 ujenzi wa bomba hilo utakapokamilika, yatatumika mafuta ya dola za Marekani trilioni 1.44.

Alisema kuwa kanuni inayotumiwa sasa katika kuelekea karne ya 22 ni sayansi+teknolojia+mitaji+rasilimali fedha huku akibainisha kwamba porojo hazina nafasi.

Alifafanua kuwa katika mageuzi hayo, wizara imeanza mkakati wa kulisuka upya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) ambapo wanatarajia kupata mikopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Muhongo alilieleza Bunge kuwa hadi sasa amekwishapokea dola za Marekani milioni 500 kutoka ADB. Kwamba huo ndio utendaji unaotakiwa ili kuondokana na mfumo wa kufukuza mawaziri kila mwaka.

Azozana na Sendeka

Hata hivyo, Muhongo alitofautiana na Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), akisema kauli zake ni za uongo kwa vile Rais Jakaya Kikwete hakuwahi kutoa ahadi ya kuwakabidhi wachimbaji wadogo mgodi wa TanzaniteOne baada ya leseni ya wawekezaji hao kuisha mwaka huu.

“Prof. Muhongo napenda nikushauri kuwa usikubali kuuziwa mbuzi kwenye gunia, ni vizuri ukawa shahidi uthibitishe mwenyewe kama Thomaso usije kuingizwa mjini kama ulivyoingizwa mwaka jana kwenye bajeti iliyopita na Katibu Mkuu Eliakim Maswi.

“Mwaka jana uliliambia Bunge hili kuwa nguzo zinatolewa Iringa zinakwenda Mombasa, Afrika Kusini kisha zinakuja hapa zinauzwa kwa bei ya ghali, ukazungumza kuwa baadhi yetu tunafanya biashara na kampuni za mafuta,” alisema.

Aligusia pia kampuni ya mafuta ya Puma Energy ambayo alihoji mwaka jana kuwa ilipata zabuni kinyume na taratibu.

“Kauli zako hizo zimethibitishwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwa Kampuni ya Ernest & Young ambayo ilifanya ukaguzi imethibitisha kuwa kauli zako ulizozitamka bungeni ni za uongo kwa kiwango cha kupindukia.

“Kauli za waziri aliyoambiwa na wataalamu wake ni za uongo kwa mujibu wa ripoti hiyo. Ripoti hiyo imefungiwa haitaki kutolewa hadharani hadi leo waziri umeingizwa tena mtegoni kwenye sekta ya madini,” alisema.

Sendeka alifafanua kuwa walipitisha sheria kuwa madini ya vito yachimbwe na Watanzania, lakini wizara imekiuka uamuzi wa Bunge kwa wataalamu wake kutoa leseni kinyume cha sheria.

Alisema kuwa badala yake leseni hiyo imetolewa kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) wakati Rais Kikwete alipokuwa kwenye kampeni mwaka 2010 aliahidi kuwa watapewa wachimbaji wadogo.

Sendeka aliongeza kuwa hiyo ni kauli ya Rais Kikwete, lakini wizara inakwenda kinyume na hivyo akahoji ni kauli ya nani inaheshimiwa kati ya rais na Waziri Muhongo.

Alisema hata tume za Jaji Mark Bomani na Robert Mboma zilipendekeza kwenye ripoti zao kuwa leseni za wawekezaji wakubwa zikimalizika migodi wapewe wachimbaji wadogo.

Akijibu hoja hiyo, Waziri Muhongo alisema madai ya Sendeka si ya kweli na kwamba alikaa naye Arusha akarudia hilo la Rais Kikwete kutoa ahadi, lakini bahati nzuri Mkuu wa Mkoa wa Manyara alikuwepo, akaangalia kwenye daftari la ahadi hizo, lakini hakuikuta ahadi ya rais.

“Ndugu zangu, mheshimiwa Ole Sendeka tumsikilize, tukune vichwa hapa wakati Mkuu wa Mkoa wa Manyara hana hiyo ahadi, na isitoshe wakati nikiwa naenda kwenye hicho kikao nilimpigia rais, nikamuuliza. Lakini akaniambia wanamlisha maneno mdomoni,” alisema.

Credits: TANZANIA DAIMA
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top