Suala hili linahitaji muda na heshima kwa wananchi. Ni vema tuache sauti ya wananchi kusikika na kuzitolea maamuzi sahihi yenye kujenga kuaminiana na kuheshimiana kati ya dola na wananchi.
Suala la Mtwara ni zaidi ya gesi asilia. Ni matokeo ya kutengwa kimaendeleo kwa muda mrefu. Suala la Gesi ni nafasi ya kuunganisha watu wa kusini na Jamhuri ya Muungano. Tuamue sasa kufanya maamuzi sahihi na kuunganisha Jamhuri yetu au kukosea na kudharau na kuivunja Jamhuri yetu.
Kama Kuna mataifa ya kigeni/makampuni binafsi yanahusika na hali ya Mtwara. Serikali iyataje mataifa hayo na makampuni hayo hadharani na vibaraka wao.Vinginevyo nadharia hizi zitaonekana ni ni propaganda tu kwa lengo la kufunika kombe mwanaharamu apite.
Nadharia zote za kuelezea masuala ya Mtwara zinakimbia suala la msingi ie kutengwa kwa muda mrefu sana kwa mikoa ya kusini kwenye maendeleo ya nchi. Ahadi za Rais Ben Mkapa kuhusu Mtwara Corridor, ahadi za Rais Jakaya Kikwete za 2005 na biashara ya korosho ni miongoni mwa malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wa Mtwara. Suala hili la msingi lazima lipatiwe majawabu mwafaka kwa maelezo yenye heshima kwa wananchi badala ya dharau na vijembe dhidi ya raia.
Kuna kukosa imani kukubwa kwa wananchi dhidi ya Serikali. Suala hili ni pana zaidi na linasambaa Tanzania nzima. Malalamiko yanaposhawishiwa kihofu tu huleta matatizo makubwa sana. Hali ya namna hii haijawahi kutokea nchini mwetu. Kukamata na kufunga viongozi wa wananchi haitosaidia kamwe.
Kutumia nguvu ya dola kuzima vuguvugu la wananchi sio njia pekee ya kujenga amani. Makovu ya kutumia nguvu ya dola huchukua muda mrefu sana kupona. Lazima kubadili mkakati wa kuongoza na kuliweka Taifa sawa.
Zitto Zuberi Kabwe (Mb)
24th May 2013
Post a Comment