*********
Siku
chache baada ya mabingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara, Klabu ya Yanga
ya Dar es salaam kulamba madume mawili katika usajili, Mrisho Khalfan
Ngassa “Anko” na Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima “Fabrigas” baraza
la wazee wa klabu hiyo wameendelea kutia baraka kwa uongozi kwa Yusuf
Manji.
Katibu
wa baraza la wazee wa klabu hiyo, Mzee Ibrahim Akilimali amesema
usajili mzuri unaofanywa na viongozi wao unaleta matumani ya kufanya
vizuri ligi ya mabingwa barani Afrika mwakani.
“Tunapopanga
kikosi chetu tunataka huyu mtoto Ngassa, Twite, na Niyonzima wakae
pamoja kufanya maajabu ya soka, timu yetu inajiandaa na michuano ya
Afrika mwakani na ndio maana tunafanya usajili makini sana”. Alisema
Akilimali.
Akilimali
alitamba kuwa jeuri ya pesa waliyonayo Yanga ndio sababu ya kusajili
vijana wazuri, na kama mtu anabisha aangalie orodha ya viongozi wa Yanga
kama kuna mtu mwenye njaa.
“Mimi
nasema viongozi wetu wana uwezo wa kutumia pesa zao kabla hawajatafuta
msaada kwa watu wengine, na matokeo yake tutazidi kuwapiga bao wapinzani
wetu”. Alitamba Akilimali.
Mzee
huyo aliyeongea kwa kujiamini alisisitiza kuwa wakati wanaendesha
harakati za kupindua uongozi wa mwana sheria Llod Nchunga, wazee
walitangaza kuwa wana fedha kiasi cha milioni mia saba kuiendesha klabu
na hivyo mwenyekiti huyo ang`atuke, lakini hawakuwa na maana ya kwamba
wao ndio wenye fedha hizo.
“Nilitangaza
tunazo milioni mia saba, watu hawakuelewa, maana yangu ilikuwa ni
kupata viongozi wenye pesa zao kama Yusuf Manji, Clement Sanga, Binkleb
na wengineo ambao ukipima na mzani, thamani yao ni zaidi ya shilingi
milioni mia saba”. Alisema Akilimali.
Akilimali aliwataka mashabiki na wanachama wa Yanga kuendelea kuunga mkono jitihada za viongozi wao wakiongozwa.
“Sisi
tunabariki sana kazi za mwenyekiti wetu, uongozi wake umetupa matumaini
makubwa sana, tutafika mbali zaidi kwa mpango huu”. Alisema Akilimali.
Jana
Yanga imetangaza kumsajili Haruna Niyonzima kwa mkataba wa miaka miwili
na mei 19 mwaka huu walimtambulisha Mrisho Ngassa masaa machache baada
ya pambano la watani wa jadi ambapo Yanga alishinda mabao 2-0.
Simba
wanadai Ngassa ana mkataba nao wa mwaka mmoja na Yanga walitangaza
kumsainisha mkataba wa miaka miwili na Ngassa alikaririwa akisema
ameamua kujiunga na klabu yake hiyo ya zamani yenye makazi yake mitaa ya
Twigar na Jangwani.
Post a Comment