* NI JUU YA MRADI WA AIRTEL RISING STARS NCHINI
Viongozi wawili kutoka Manchester United — Anthony Benerjee, Mkurugenzi wa Uhusiano na Michael Higham, Meneja Uhusiano — wanatua jijini Dar es Salaam Jumatano hii kufanya manzungumzo na viongozi wa Airtel Tanzania namna bora ya kuendesha michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars mwaka huu.
Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania Jackson Mmbando amesema mkutano huo utakaojumuisha wadau mbalimbali utafanyika makao makuu ya Airtel Tanzania jijini Dar es Salaam na kutathimini ARS ya miaka miwili iliyopita ili kuona namna nzuri ya kuendesha michuano siku za usoni kuanzia mwaka huu.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni moja ya wadau wataoshiriki mkutano huo ili kutoa mchango wao hasa katika masuala ya kifundi kama vile upangaji wa ratiba ya mashindano. Ratiba ya kuanza kwa ARS 2013 inatarajiwa kutangazwa mwezi huu.
Michuano ya soka Airtel Rising Stars ilizinduliwa hapa nchini Tanzania na sehemu nyingine barani Afrika mwaka 2011 ikiwa na lengo mahsusi la kusaidia kuvumbua vipaji vya wanasoka chipukizi na kuwafanya waonekane
kwa makocha na mawakala wa kusaka vipaji vya wachezaji nyota.
Mashindano haya huanzia ngazi ya chini ambapo timu za sekondari ngazi ya mkoa huchuana ili kupata wachezaji nyota wa kuunda kombaini inayowakilisha mkoa husika kwenye mashindano ya Taifa ambayo hufanyika jijini Dar es Salaam. Jumla ya timu 48 zimepata fursa ya kushirikia ARS katika miaka miwili iliyopita.
Katika mwaka wa uzinduzi 2011 mashindano ya ARS ngazi ya Taifa yalifuatiwa na kliniki ya kimataifa chini ya usimamizi wa makocha kutoka Manchester United iliyofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kushirikisha wavulana na wasichana kutoka nchi za Kenya, Malawi, Sierra Leone na mwenyeji Tanzania.. Mwaka jana fainali za taifa za ARS zilifuatiwa na michuano ya kimataifa ya ARS zilizofanyika jijini Nairobi zikishirikisha nchi ambazo kampuni ya Airtel hufanya biashara. Vile vile kliniki ya mwaka
jana ilifanyika Nairobi chini ya usimamizi ya makocha wazoefu kutoka shule za mafunzo ya soka ya vijana za Manchester United ambapo vijana walipata fursa ya kujifunza mbinu mbalimbali za soka.
Post a Comment