Mkurugenziwahospitaliya
IMTU Dkt. Ali Mzige akisitiza umuhimu wa wazazi kujali afya za watoto
na kufuatilia uzito wa watoto wao walio chini ya umri wa miaka mitano
alipokua akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam
,Kulia kwake ni Bw.Saibal Sarbadhikari Meneja Mkuu wa umoja wa BANGO
SANGHO.
Mkurugenzi
wa hospitali ya IMTU Dkt. Ali Mzige akihamasisha wananchi kujitokeza
katika zoezi la upimaji afya bure kwa watoto walio chini ya miaka
mitano,utakaofanyika jumapili Mei 26 katika hospitali hiyo iliyopo Mbezi
Beach. Kushoto kwake ni Bw.Saibal Sarbadhikari Meneja Mkuu wa umoja wa
BANGO SANGHO.
**********
Na Genofeva Matemu -MAELEZO
HOSPITALI ya Chuo Kikuu cha Kimataifa
cha Tiba na Tekinolojia (IMTU hospital) kwa kushirikiana na Umoja wa
Jamii ya watu kutoka India Bengali waliopo nchini Tanzania watatoa
huduma ya upimaji afya bure jumapili Mei 26 mwaka huu kwa watoto wenye
umri chini ya miaka mitano wanaoishi maeneo ya Mbezi Beach .
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa
hospitali ya IMTU Dkt. Ali Mzige alipokua akizungumza na waandishi wa
habari leo jijini Dar es Salaam kuhusiana na afya ya mtoto na umuhimu wa
maziwa ya mama hasa kwa watoto walio chini ya miezi 6 .
Dkt. Mzige amesema wanakusudia kupima
uzito, presha na kutazama afya ya kinywa kwa watoto wenye umri chini ya
miaka mitano ambapo watatumia vifaa maalumu vya upimaji presha kwa
watoto hao.
“Tutapima uzito ambao takwimu zake ni
Kg 10 kwa mtoto wa mwaka mmoja, Kg 11 kwa mtoto wa mwaka mmoja na nusu,
Kg 12 mtoto wa miaka 2, Kg 13 kwa mtoto wa miaka miwili na nusu, Kg 14
kwa mtoto wa miaka 3, Kg 15 kwa mtoto wa miaka mitatu na nusu, Kg 16
mtoto wa miaka 4, Kg 17 mtoto wa miaka minne na nusu, na Kg 18 ni kwa
mtoto wa miaka mitano”, amesema Dkt. Mzige.
Akirejea matokeo ya sensa ya mwaka 2012
Dkt. Mzige amesema matokeo hayo yalionesha kuwa asilimia 42 ya watoto
chini ya miaka mitano hapa nchini wamedumaa, ambapo asilimia 16 wana
uzito pungufu (Underweight) na asilimia 5 wamekonda (Marasmic) wako
kwenye rangi nyekundu ya kadi za watoto za kliniki.
Aidha Dkt. Mzige ameishauri jamii kula
lishe bora na kamili sababu lishe bora huanzia nyumbani hivyo ni jukumu
la jamii kupata elimu ya chakula bora na mlo kamili wenye kujenga afya
bora kwa watoto.
Zoezi la upimaji wa afya kwa watoto
limeanza rasmi mwaka huu na linatarajiwa kufanyika kila mwaka au mara
mbili kwa mwaka kwa kushirikiana na uhisani wa Bango Sangho jamii ya
wahindi wanaoishi hapa nchini ambao wamekua wakitoa vifaa vya kupimia
afya za watoto.
Post a Comment