Ndugu zangu,
MTANZANIA mwenzetu marehemu Shaaban Robert anaandika;
” Wasadikika wana desturi ya kutafuta fimbo baada ya kuumwa na nyoka. Tumekwisha umwa na nyoka kwa matendo yetu mabaya ya zamani.
Nyoka mwenyewe amekwishakimbia. Hapatikani kwa kujilipiza kisasi, lakini, sumu yake imebakia katika jeraha tulilolipata. Sasa, shauri lililo jema ni kuzuia sumu hii isienee miilini mwetu ikaleta kifo.
Maovu yana hatari kubwa kukaa kati yetu. Tumedumu nayo kwa muda mrefu. Hayakutuletea faida ila hasara, huzuni na kilio siku zote.”- Shaaban Bin Robert.
Yanayotokea Mtwara Na Kinachohitajika Sasa...
Ndugu zangu,
Yanayotokea Mtwara yanatuletea mashaka kama taifa. Linalohitajika sasa si tamko la Serikali tu, bali, tamko letu Watanzania kwenye mioyo yetu, kwamba, pamoja na haki yetu ya kimsingi ya kudai haki, lakini, lililo la hekima na busara ni kutumia njia mujarab za kuitafuta haki hiyo.
Na njia hiyo haiwezi kuwa ni matumizi ya nguvu ikiwamo kufanya vurugu. Hivyo, kufanya maovu ikiwamo kutoa roho za wenzetu na uharibifu wa mali, iwe imefanywa na wananchi au Serikali.
Kama Watanzania huu ni wakati wa kufikiri kama taifa. Hii ni Nchi Yetu. Huu si wakati wa kufikiri kwa mitazamo ya kiitikadi au kiimani. Yanayotokea Mtwara yana madhara kwa nchi nzima, na yakiachwa bila kupatiwa ufumbuzi wa haraka, yatatawanya sumu mahala pengine pia.
Ni wakati wa Viongozi wa Serikali, Viongozi wa Chama Tawala, Viongozi wa Vyama Vya Upinzani , Viongozi wa kidini na kwa kuwashirikisha wazee wa Mtwara, kutoa matamko yatakayosisitiza umuhimu wa kutumia majadiliano katika kupata ufumbuzi wa tatizo lililopo.
Tukumbuke, kuwa nchi yetu ina mipaka, hivyo basi, ina maadui pia. Tusipotanguliza hekima na busara, yumkini tunaweza kutoa nafasi kwa maadui kutugombanisha zaidi. Na hivyo ikawa hasara zaidi kwetu , na faida kwa wengine.
Hakika,tunaweza kuyamaliza yetu kwa mazungumzo. Tuianze kazi hiyo sasa.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
0754 678 252
Post a Comment