ASKARI WAKIWA KAZINI.
ASKARI 15 wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar
es Salaam waliofukuzwa kazi hivi karibuni kwa kosa la kupokea rushwa ili
kupitisha mizigo bandarini kwa njia za magendo wameibuka na kutoa siri ya
kufukuzwa kwao.
Mmoja wa askari hao akizungumza kwa niaba ya
wenzake, alisema sababu ya kufukuzwa kwao imetokana na wao kukamata magari ya
vigogo serikalini, akiwemo aliyekuwa Rais mstaafu wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ambaye anadaiwa kuwa kinara wa
kukwepa kodi.
Akizungumza na gazeti hili, askari huyo alisema
baadhi ya viongozi wa juu wa
jeshi hilo wamekuwa wakiwasaidia wafanyabiashara wakubwa kukwepa kodi na pindi
askari wadogo wanapoyakamata magari hayo hufukuzwa kama ilivyotokea
kwao.
Kwa mujibu wa habari hizo, katika kesi ya kijeshi
iliyotolewa hukumu ya kuwaondoa kazini askari hao, waliomba waoneshwe dereva na
gari linalodaiwa kuwa lilitoa rushwa kwao kama kielelezo muhimu katika kesi yao,
lakini hadi sasa gari na dereva huyo hawajapatikana.
Mashtaka ya askari hao, yalitarajiwa kusomwa na
askari mmoja wa juu, lakini alipobaini kwamba hakuna ushahidi, aliamua kujiondoa
na kuchukuliwa na askari mwingine ambaye ndiye aliyewasomea
mashitaka.
“Baada ya kesi kusomwa Juni sita mwaka huu,
ikatolewa hukumu ya kutuondoa kazini pasipo walalamikaji na vidhibiti
kuwasilishwa katika mahakama ya kijeshi. Kwa kifupi hatukutendewa haki na
tunakusudia kukata rufaa,” alisema askari huyo kwa niaba ya
wenzake.
“Ukweli ni kwamba wanaofanya biashara ya kuingiza
bidhaa bila kulipia kodi ni viongozi wakubwa wa nchi hii hasa huyu kiongozi
mstaafu wa Zanzibar na mkewe, sisi leo hatupo kazini na wao wanaendelea
kupitisha bidhaa bandarini kwa rushwa,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius
Wambura, akizungumzia hatua ya askari hao kufukuzwa kazi alisema alichofanya ni
kuthibitisha adhabu yao baada ya kupitishwa katika kitengo cha nidhamu ya
jeshi.
“Kwangu si muhimu kujadili adhabu iliyotolewa na
mahakama ya kijeshi, nilichofanya ni kuthibitisha tu na kama wanaona wameonewa,
tumewaambia wakate rufaa,” alisema Wambura.
Akizungumzia madai ya kuwalinda baadhi ya
viongozi katika tuhuma za kusafirisha mizigo pasipo kulipia ushuru, Kamishna wa
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema yeyote mwenye ushahidi wa
tuhuma hizo aziwasilishe kwake.
Kuhusu kukosekana ushahidi pamoja na wahusika
waliotumika kutoa rushwa, CP Kova, alisema hawezi kuwataja kwa kuwa walitumwa
kuweka mtego wa kuwanasa askari wanaosaidia watu kukwepa
kodi.
Taarifa za kukamatwa kwa askari hao,
zilifichuliwa na gazeti hili na kuripoti kuwapo kwa mtandao mpana wa askari wa
jeshi hilo wanaojihusisha kuwasaidia wafanyabiashara kukwepa kulipa
kodi.
Post a Comment