Dar es Salaam. Wamiliki wa simu nchini kuanzia
mwezi ujao wataanza kuingia gharama zaidi kwa asilimia 14.5 ili kuongeza mapato
ya Serikali na kugharimia elimu.
Hayo yalisemwa bungeni jana na Waziri wa Fedha,
Dk William Mgimwa wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Serikali kwa mwaka wa fedha 2013/14 unaoanza Julai Mosi, mwaka huu.
Akifafanua suala hilo kama chanzo kipya cha
mapato ya Serikali, Dk Mgimwa alisema Serikali inakusudia kuanzia mwezi ujao
kutoza ushuru wa bidhaa wa kiwango hicho kwenye huduma zote za simu za
kiganjani, badala ya muda wa maongezi peke yake.
“Katika ushuru huu, asilimia 2.5 zitatumika
kugharimia elimu hapa nchini... Hatua hii imezingatia mapendekezo ya Kamati
Maalumu ya Spika ya Kushauri kuhusu mapato na matumizi ya Serikali,” alisema Dk
Mgimwa.
Kama vile haitoshi, Waziri Mgimwa alitangaza
kuongeza wigo wa kutoza ushuru wa bidhaa kwenye huduma za simu za mezani
(zinazojulikana kama za TTCL) na zisizokuwa na waya.
Pia waziri alitangaza kuanzisha kodi ya zuio ya
asilimia 10 ya kamisheni (commission) ya usafirishaji wa fedha kwa njia ya simu
za mkononi. Kodi hiyo itakusanywa na kampuni za simu kutoka kwa wakala wanaotoa
huduma za kusafirisha fedha kupitia simu za mkononi;
Mapendekezo hayo ya Waziri Mgimwa ni
utekelezaji wa ushauri wa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Ludovick
Utouh kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), itafute vyanzo vipya vya kodi ili
kuongeza mapato ya Serikali. Miongoni mwa maeneo ambayo Ripoti ya CAG iliyoishia
Juni 30, mwaka jana ilishauri kuangaliwa, ni pamoja na huduma za kuhamisha fedha
kwa njia ya simu za kiganjani maarufu kama M-Pesa, Tigo Pesa, Airtel Money na
Easy Pesa.
CAG alishauri kuwa kampuni za simu kulipa kodi
ya zuio ya malipo ya kamisheni inayolipwa kwa wanaofanya biashara hiyo na kodi
hiyo ya zuio ipunguzwe kutoka katika kodi ya mwisho itakayotakiwa kulipwa na
kampuni za simu.
Chanzo: Mwananchi
Post a Comment