MATUMIZI ya Shirika la Umeme (Tanesco) kwa mwaka ujao wa
fedha yameiweka Serikali njia panda hasa baada ya kutakiwa kutafuta fedha hizo
nje ya bajeti.
Kamati ya Bunge ya
Bajeti imeweka wazi kuwa fedha zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya matumizi ya
shirika hilo linalotegemea zaidi ruzuku ya Serikali, ni ndogo kuliko
mahit
aji halisi ya
Shirika hilo kwa mwaka.
Kutokana na hali
hiyo, Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na
wabunge wameungana kuitaka Serikali kutobadilisha matumizi ya fedha zilizopangwa
na Bunge katika bajeti yake, huku wakiitaja Wizara ya Nishati na Madini kuwa
moja ya wizara zilizotumia fedha zaidi ya bajeti waliyopangiwa mwaka
jana.
Kwa mujibu wa
Chenge, Wizara ya Nishati na Madini katika mwaka wa fedha unaoisha, ilipangiwa
kutumia Sh bilioni 76.99 lakini ikatumia Sh bilioni 148.42, sawa na ongezeko la
Sh bilioni 71.43.
Wizara nyingine
zilizotumia fedha zaidi ya bajeti ilizopangiwa ni Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, ambayo ilipangiwa kutumia Sh bilioni 80.6 lakini
ilitumia Sh bilioni 112.08 sawa na ongezeko la Sh bilioni 31.47.
Pia Wizara ya Afya,
lipangiwa kutumia Sh bilioni 219.36 lakini ilitumia Sh bilioni 246.71, sawa na
ongezeko la Sh bilioni 27.35.
Deni la Taifa nalo,
lilipangiwa kutumia Sh trilioni 1.9, lakini lilitumia Sh trilioni 2.5 sawa na
ongezeko la Sh bilioni 624. Akizungumzia hali hiyo juzi bungeni, Chenge alisema
katika hali ya kushangaza wizara hizo zimetumia fedha zaidi ya zilizoidhinishwa
na Bunge.
Ili kukabili hali
hiyo, Chenge akaitaka Serikali, itakapotaka kuongeza fedha zaidi ya
zilizoidhinishwa na Bajeti, kwa maana ya kuhamisha mafungu, iwasiliane kwanza na
Kamati yake.
Matumizi ya Tanesco
nje ya bajeti Kuhusu Tanesco, Chenge alisema; “Ni muda mrefu sasa Shirika hili
limekuwa likitumia fedha nyingi kwenye ununuzi wa mafuta kwa ajili ya kuendesha
mitambo ya kuzalisha umeme.
“Kamati imebaini
kuwa Serikali imekuwa ikitenga fedha kidogo kwa ajili ya kuendesha Shirika hili,
hali inayosababisha kufanyika kwa uhamisho wa fedha kutoka katika maeneo mengine
kwa ajili ya kupeleka Tanesco,” alisema.
Ili kuzuia hali
hiyo, Chenge alisema Kamati yake ilikutana na Tanesco pamoja na Wizara ili
kupata taarifa za gharama halisi ya Tanesco kwa mwaka ujao wa fedha, ambao
shirika hilo limetengewa Sh bilioni 273.
“Katika kikao
hicho, ilibainishwa kwamba kwa mwaka 2013/14, Tanesco itaendesha mitambo kwa
asilimia 78, na kwa mpango huo, Tanesco itatumia Sh trilioni 1.2,” alisema
Chenge na kuongeza kuwa mitambo hiyo ikiwashwa kwa asilimia 100, shirika hilo
litatumia Sh trilioni 2.2.
Zigo la Serikali
Badala ya kujadili wapi fedha hizo zitapatikana, au kutoa nafasi ya Wizara
kukutana na Kamati kutafuta fedha hizo, Chenge alitaka Serikali itafute fedha
hizo sehemu nyingine bila kugusa bajeti.
“Kamati inashauri
kuwa fedha hiyo ipatikane bila kuathiri Bajeti ya Serikali,”
alisema.
Wakati wa kuchangia
bajeti hiyo, wabunge wengi pia walisimamia msimamo huo, bila kuitaja Tanesco,
wakataka Serikali isibadilishe matumizi ya fedha zilizopangwa katika bajeti, na
wengine kufikia hatua ya kutaka Sheria ya Bajeti, ili kuidhibiti Serikali
isihamishe vifungu. CHANZO HABARILEO


Post a Comment