*Asema bila kujali walimu hakuna matokeo bora
*Adai ana ndoto siku moja watoto watasoma bure
*Adai ana ndoto siku moja watoto watasoma bure
WAZIRI Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, ‘ameivua nguo Serikali’, baada ya kusema Tanzania inaweza kutengeneza sera, mitaala bora na kuunda tume nyingi, lakini kama haitawajali walimu, elimu bora itaendelea kubaki ndoto. Lowassa alitoa kauli hiyo jana, kwenye viwanja vya Ushirika, mkoani Kilimanjaro, wakati wa maadhimisho ya siku ya SACCOS ya Walimu.
Alisema kuwajali walimu ni pamoja na kuwapa mafunzo kazini ili waweze kujifunza mbinu mbadala za kufundishia, wajue namna mbalimbali za kuwahamasisha wanafunzi kupenda masomo.
“Ifike mahala sasa turejeshe heshima ya mwalimu, lakini ifike mahala, nanyi walimu muonyeshe kwa vitendo kuwa taifa hili lina wajibu wa kuwapa heshima hiyo.
“Ninayo ndoto kwamba, siku moja katika nchi hii hakuna mtoto atakayeshindwa kusoma kwa sababu mzazi wake hana kipato.
“Katika nafsi yangu, naamini maslahi bora kwa walimu ndio mwanzo wa kuiboresha elimu ya Tanzania, ndiyo maana niko hapa kwenye tukio hili la kuichangia SACCOS hii.
“Hakika nyie, badala ya kuweka nguvu nyingi kuidai nchi iwaboreshee maisha, mmeamua kuweka nguvu zenu zaidi katika kuisaidia nchi yenu na kwa tukio la leo (jana), mmewaonyesha walimu wengine nchini kwamba walimu kwa umoja wenu mnao uwezo wa kuifanyia Tanzania yetu jambo la maana mkiamua,” alisema.
Aliwataka viongozi kujiuliza, ni kwa nini mwalimu anayeanza kazi hapewi chombo cha usafiri, lakini bwana shamba anapewa, kwa nini walimu wengi hawapewi nyumba za kuishi, wakati wafanyakazi wengine wenye elimu inayolingana nao wanapewa nyumba za kuishi.
“Tujiulize kwa nini maofisa wengine wa Serikali wanapata posho mbalimbali, lakini walimu tena si wote wanaambulia posho wakati wa uchaguzi au sensa tu.
“Tukishajiuliza maswali haya, tusiishie hapo, tuchukue hatua ya kuirekebisha hali hii ili watu wenye uwezo mkubwa kitaaluma nao wavutiwe kuwa walimu, kazi ya ualimu iweze kupiganiwa na watu wenye ufaulu wa juu kama udaktari na sheria, na ipewe heshima hiyo inayostahili,” alisema Lowassa.
Alisema anatambua wapo viongozi wenye hofu ya kuboresha mazingira ya kazi za walimu, eti si jambo rahisi kwa sababu ya wingi wao.
Alisema Watanzania, wanapaswa kuondokana na woga unaowafanya kuona kuwa pamoja na madini, gesi, mbuga nyingi za wanyama na ardhi nzuri ya kilimo, hawawezi kusimamia rasilimali hizi na kupata mapato makubwa yatakayowezesha kuwalipa walimu vizuri.
Lowassa, ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM), alisema leo hii kila mpenda ukweli atakiri kuwa elimu ya Tanzania iko mahututi kiasi cha kuwakatisha wengi tamaa, ambapo aliwataka walimu kutokata tamaa.
Alisema kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia, hivi sasa hali ya ujinga (illiteracy rate), imeongezeka.
“Mwaka 1992 tulikuwa na Watanzania asilimia 15 tu wasiojua kusoma na kuandika, hivi sasa tuna Watanzania takribani asilimia 31 wasiojua kusoma na kuandika.
“Mwaka 2011, tumeshuhudia takribani wanafunzi 5,000 waliohitimu darasa la saba walifaulu na kujiunga kidato cha kwanza, ilhali hawajui kusoma na kuandika na ufaulu kidato cha nne unazidi kushuka mwaka hadi mwaka,” alisema Lowassa.
Hadi tunakwenda mitamboni, jumla ya Sh bilioni 1.2, zikiwamo ahadi na fedha taslimu zilikuwa zimeahidiwa, huku Mbunge wa Vunjo, Agustine Mrema (TLP), akichangia Sh milioni 10.
Kauli ya Lowassa, imekuja wakati Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia, akizidi kuikaba koo Serikali kuwa haina mitaala ya elimu.
Wiki iliyopita, Mbatia aliitaka Serikali kuacha mara moja kusambaza vitabu kwa shule za msingi, akidai haviendani na mitaala.
MTANZANIA
Post a Comment