WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA.
LETECIA NYERERE
WAZIRI Mkuu Mizengo
Pinda amesema anatamani siku moja Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere
(CHADEMA) arudi Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Pinda alitoa kauli
hiyo jana jioni wakati wa uzinduzi wa kitabu cha Sumbawanga ng’ara
kilichoandikwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Stella Manyanya (CCM), ambaye pia ni
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Hafla hiyo ya
uzinduzi ilifanyika katika hoteli ya Dodoma na kuhudhuriwa na Mawaziri,
Manaibu Mawaziri,
viongozi kutoka Mkoa wa Rukwa, viongozi wengine wa Chama na
Serikali.
Leticia Nyerere
baada ya kuinuka ili kutoa salamu zake ndipo Waziri Mkuu Pinda aliposema kuwa
anatamani siku moja Mbunge huyo wa Upinzani arudi CCM.
“Natamani siku moja
urudi CCM,” alisema Waziri Mkuu.
Hata hivyo baada ya
Mbunge huyo kufika mbele na kupewa kipaza sauti alisema ‘peoples power’ salamu
ambayo hutumiwa na chama cha Chadema, hali iliyofanya watu waliokuwa ukumbini
hapo kushindwa kujibu salamu hiyo na kubaki wakiangua kicheko.
Leticia alisema
alikwenda pale kwa ajili ya kumuunga mkono Manyanya ambaye ni mwanamke kiongozi
jasiri, ambaye mara nyingi amekuwa hasiti kuonesha ujasiri wake.
Alisema kuwa
wabunge wanatakiwa kuonesha ushirikiano katika masuala ya maendeleo badala ya
kuweka mbele itikadi za vyama.
“Tunapokuwa bungeni
tunatakiwa tuwe wapinzani lakini tunapokuja katika suala la maendeleo tunatakiwa
kuwa kitu kimoja,” alisema.
Leticia katika
hafla hiyo aliongozana na watoto wake wawili wa kike wanaosoma Maryland,
Marekani na Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipowaona aliwataka watoto hao kwenda
mbele ili wasalimie.
“Hawa ni watoto wa
Madaraka Nyerere, ni wajukuu wa hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere,”
alisema Waziri Mkuu.
Alipouliza watoto
hao wamefanana na nani, mmoja wa watoto hao alisema amefanana na bibi yake Maria
Nyerere huku mwingine akisema amefanana na baba na mama yake.
Pia akitoa salamu
zake, mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda alimpongeza Mkuu wa mkoa wa Rukwa,
Manyanya kwa juhudi anazofanya katika suala zima la kutunza
mazingira.
Aliwataka wanawake
wengine kuwa mstari wa mbele katika kuleta mabadiliko katika nyanja mbalimbali
ikiwemo kujitosa kuwania Urais mwaka 2015.
“Kwa nini mwanamke
asishinde Urais wa mwaka 2015 wao waweze wana nini na sisi tushindwe tuna nini,”
alisema Mama Pinda
Post a Comment