Daktari wa timu ya Yanga, Nassor Matuzya, akimganga mchezaji Simon Msuva.
Eleuteri Mangi – Maelezo
BARAZA
la Michezo la Taifa (BMT) limeandaa mafunzo kwa madaktari wa michezo,
kinga, tiba na mafunzo ya wataalamu kwa wanamichezo ambayo yatafanyika
katika Ukumbi wa Uwanja wa Taifa kuanzia Jumatatu Juni 10 hadi 14, mwaka
huu.
Hayo
yamesemwa na Afisa Michezo Mwandamizi Baraza la Michezo Taifa Bwana
John Chalukulu alipokuwa akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar
es salaam.
“Lengo
kuu la la mafunzo haya ni kuboresha ujuzi wa madaktari na wataalam wa
kinga na tiba kwa wanamichezo, sambamba na hilo kuhuisha ufahamu na
ujuzi ili kufanikisha uponyaji ulio sahihi na wa haraka kwa wanamichezo
waweze kudumu kwa muda mrefu kwenye sekta ya michezo,” alisema
Chalukulu.
Bwana
Chalukulu alisema kuwa mafunzo hayo yanategemewa kuwa na washiriki
wapatao 35 ikiwa ni makadirio ya juu na si chini ya washiriki 15.
Aliongeza kuwa mpaka sasa malengo hayo yamefikiwa kwani ni washiriki 16 tayari wamethibitisha kushiki mafunzo hayo.
Kwa
upande wake Dkt. Anthoni Ngome kutoka Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo ametoa wito kwa vyama, taasisi na hata watu binafsi
kushiriki katika fursa hii adimu ya kuwajengea uwezo madaktari wa
michezo nchini.
“Fursa
hii imekuja muda mwafaka kwani kuna uhaba mkubwa wa madaktari wa
michezo. Nashauri vilabu, vyama, halmashauri na shule mbalimbali walete
washiriki katika mafunzo hayo.” alisema Dkt. Ngome.
Naye
katibu Mkuu wa Chama cha Wataalamu wa Tiba ya Wanamichezo Tanzania
(TASMA) Dkt. Nassoro Matuzya ameishukuru Serikali kupitia BMT kwa hatua
kubwa na ya pekee ya kuanzisha mafunzo hayo kwa kuwa miaka ya nyuma
ilikuwa inakosekana.
Mafunzo
hayo yataendeshwa kwa pamoja na Wataalamu kutoka wizara husika chini ya
Idara ya Michezo kupitia kitengo cha Kinga na Tiba kwa Wanamichezo,
Chama cha Wataalamu wa Tiba na Michezo Tanzania (TASMA) na Taasisi ya
Mifupa Muhimbili (MOI).



Post a Comment