*********
Habari za uhakika kutoka ndani ya Jeshi hilo zimedokeza kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Said Mwema anatarajiwa kustaafu mwezi ujao na haijafahamika kama ataongezewa mkataba ama la.
Vyanzo mbalimbali vimedai kuwa japokuwa IGP Mwema anasita kukubali kuongezewa muda, lakini Rais Jakaya Kikwete anaonelea aongezewe muda ili wamalize pamoja uongozi wao mwaka 2015.
IGP Mwema ambaye alikuwa Ofisi ya Polisi wa Kimataifa (Interpol) Jijini Nairobi, Kenya, aliteuliwa kushika wadhifa wake huo mwaka 2006 na Rais Kikwete, kumrithi Omar Mahita ambaye alistaafu.
Habari zinasema endapo IGP Mwema hatapewa mkataba wa ama miaka miwili, basi ni dhahiri Rais Kikwete atakuwa na kibarua kigumu cha kuanza mchakato wa kumtafuta mrithi wake.
IGP Mwema anachukuliwa kama mmoja wa viongozi wa juu wa Jeshi hilo aliyelifanyia mapinduzi makubwa aliposhika madaraka hayo, ikiwamo kuja na dhana ya ulinzi shirikishi ama Polisi Jamii.
Tayari mabadiliko hayo yameaanza kufanyika kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, Charles Kenyela kuhamishiwa makao makuu ya jeshi hilo.
Taarifa zaidi zimepasha kuwa nafasi nyingine ya juu ambayo kuna dalili ya kuwepo kwa mabadiliko ni ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), inayoshikiliwa na Robert Manumba.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya jeshi hilo aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa (jina linahifadhiwa), amehamishiwa makao makuu wakati tayari kuna taarifa za yeye kustaafu.
Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso alipotakia kueleza juu ya taarifa hizo za mabadiliko ndani ya jeshi hilo, kutokana na muda wa kustaafu kwa maofisa hao kufika alisema hizo ni taarifa za hisia.
“Hizo ni taarifa za hisia zako tu, lakini huwezi kuniuliza swali la mwezi wa saba leo, tusubiri muda ukifika tuone itakuaje,” alisema Senso.
Pia kuhusu taarifa za Kamanda wa Polisi Kinondoni, Charles Kenyela kuhamishia makao makuu alisema; “Subirini nitatoa taarifa kwani mbona kila mabadiliko yanayotokea ya makamanda huwa ninatoa taarifa hivyo subirini”.
Habari zisizo rasmi zimelidokeza gazeti hili kuwa huenda DCI Manumba akapumzishwa kutokana na hali yake ya kiafya kuonekana kutorejea vizuri, licha ya kupatiwa matibabu nchini Afrika Kusini.
MWANANCHI
Post a Comment