JESHI la Polisi jijini Mwanza linatuhumiwa kumuachia mtuhumiwa
aliyetajwa na watu waliokamatwa katika tukio la ujambazi, kuwa ndiye
mfadhili mkuu wa matukio ya ujambazi jijini humo na maeneo mengine ya
nchi.
Mtuhumiwa anayelalamikiwa kuachiwa kutokana na amri ya Mkurugenzi wa
Mashitaka nchini (DCI), Robert Manumba, ametajwa kuwa Jackson Robert
maarufu kwa jina la Masamaki ambaye aligombea udiwani katika Kata ya
Kirumba kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Tanzania Daima, imepata taarifa kutoka jijini Mwanza kuwa Juni 23, mwaka
huu watuhumiwa watatu ambao ni Anthony Joachim, Sylvester Saimon na
mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Siri, walikamatwa katika eneo la
Nyamanoro wakiwa katika harakati za kutaka kufanya uhalifu.
Inaelezwa kabla ya watuhumiwa hao kukamatwa, Sylvester aliwarushia
askari risasi ingawa hakufanikiwa kuwajeruhi, na baada ya kudhibitiwa
alimtaja Masamaki kuwa mfadhili wao aliyewapatia silaha waliyokutwa
nayo.
Kutokana na maelezo hayo, polisi walifika nyumbani kwa Masamaki eneo la
Igore Kirumba kufanya upekuzi uliofanikisha kukutwa kwa maboksi ya
risasi yakiwa yamehifadhiwa.
Tanzania Daima limedokezwa kuwa baada ya upekuzi huo, polisi waliamua
kuondoka na mtuhumiwa hadi kituoni ambako mahojiano zaidi yaliendelea.
Mtoa taarifa alilieleza Tanzania Daima kuwa wakiwa katika kituo cha
polisi Kirumba lilifunguliwa faili lenye namba MZN/RB/4686/2013 kesi
ikiwa ni unyang’anyi wa kutumia silaha. Kisha Masamaki aliomba kufanya
mawasiliano na Christopher Gachuma, ambaye ni mjumbe wa NEC ya CCM taifa
kupitia Mkoa wa Mara.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa baada ya muda watuhumiwa waliondolewa
katika kituo hicho cha polisi na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi cha
Centre.
“Pale kituoni siku ile walilala na Juni 24 Masamaki akaachiwa kwa
dhamana. Nasikia Gachuma aliongea na DCI Manumba, wale wana undugu, na
baada ya muda Ofisa Upelelezi wa Mkoa (RCO) akapigiwa simu ya kumuachia
kwa dhamana. Lakini wenzake wanaendelea kushikiliwa,” alisema mtoa
taarifa wetu jijini humo.
Aliongeza kuwa baada ya Masamaki kuachiwa faili liliandaliwa huku kukiwa
na mkakati wa kumuondoa mtuhumiwa huyo katika sakata hilo, na kwamba
baada ya faili kurejeshwa kutoka kwa DCI, jina lake halikuwepo kati ya
watu wanaopaswa kupelekwa mahakamani.
Tanzania Daima iliwatafuta Gachuma, DCI Manumba na RPC wa Mwanza kwa ajili ya kupata ukweli wa kumuachia mtuhumiwa huyo.
Kauli ya Gachuma
Gachuma alipopigiwa simu kuulizwa juu ya kumkingia kifua Masamaki
asijumuishwe na watuhumiwa wenzake wa unyang’anyi kwa kumuomba DCI
Manumba aingilie kati, alikana kuhusika.
Alisema hadi leo hii hajui kama DCI Manumba amesharejea nchini kutoka
Afrika Kusini alikopelekwa kwa ajili ya matibabu akitokea hospitali ya
Agha Khan ya jijini Dar es Salaam.
“Mimi nipo Dodoma, huyo Manumba sina mazoea ya kuongea nae kwenye simu.
Si nilisikia anaumwa, kwani amesharudi? Jamani hawa watu wanaonihusisha
na mipango hiyo wana lao jambo,” alisema Gachuma.
DCI Manumba
Manumba alipopigiwa simu juu ya suala hilo, alisema hana taarifa hizo na
kumtaka mwandishi azungumze na kamanda wa polisi jijini Mwanza
lilikotokea tukio hilo.
Tanzania Daima ilipotaka kujua ilikuwaje akatoa maagizo kwa Mkuu wa
Upelelezi wa Mkoa wa Mwanza ili wamuachie kada huyo wa CCM, hakujibu na
akakata simu.
RPC Mwanza
Kamanda wa Polisi jijini Mwanza, RPC Ernest Mangu, alikiri jeshi hilo
kumuachia Masamaki, lakini si kwa sababu ya maagizo ya DCI bali ushahidi
uliopatikana.
Mangu alisema taarifa za polisi kumuachia Masamaki kwa shinikizo fulani
zinalenga kuwachafua na zinatolewa na watu wenye nia ovu.
Alisema polisi walifanya uchunguzi na kubaini Masamaki hahusiki na watu
waliokamatwa katika tukio hilo, na hata walipopeleka faili kwa mwendesha
mashtaka wa serikali, akaona hakuna sababu ya kumfikisha mahakamani.
“Sisi ndio tunaopeleleza na kujiridhisha, sasa hao wanaosema tumepewa
amri ya kumuachia watakuwa na sababu zao. Lakini ukweli ni huo,
imeonekana hakuna sababu za kumfikisha mahakamani,” alisema Mangu.
Alipoulizwa sababu ya watuhumiwa kumtaja Masamaki ndio aliyewapa silaha
pamoja na kukutwa kwa maboksi ya risasi nyumbani kwake, alisema silaha
iliyotumiwa na watuhumiwa haikutoka kwa Masamaki na kwamba waliomtaja
wanaweza kuwa na chuki naye.
chanzo: Tanzania daima
Post a Comment