Taifa Stars inatupa karata yake ya pili ugenini kwenye mechi za mchujo za Kombe la Dunia kwa leo kuikabili Morocco (Lions of the Atlas) kwenye Uwanja wa Grand Stade hapa Marrakech, Morocco.
Ilipoteza
ya kwanza ugenini dhidi ya Ivory Coast mwaka jana, na kushinda mbili
mfululizo nyumbani dhidi ya Gambia na Morocco. Mechi hiyo itakayochezwa
kuanzia saa 3 usiku kwa saa za Morocco ni ya pili kwa Stars katika
uwanja huo ambapo mwaka juzi ilifungwa mabao 3-1.
Washabiki
wa Morocco wanaonekana kuikatia tamaa timu yao yenye pointi mbili tu
nyuma ya Ivory Coast inayoongoza kundi hilo la C ikiwa na pointi saba
ikifuatiwa na Tanzania yenye sita. Huo ni mtazamo wa washabiki, lakini
kwa upande wa timu inaonekana imepania kujichomoa katika nafasi za
chini.
Kwa upande wa Kocha wa Stars, Kim Poulsen
amesema timu yake imepania mechi hiyo, lengo likiwa ni kuona inapata
matokeo mazuri baada ya dakika 90 za mechi hiyo itakayokuwa chini ya
refa Daniel Frazier Bennett wa Afrika Kusini.
Amesema timu yake itacheza kwa umakini na
uangalifu kwa vile wanajua wapinzani wao wakicheza mbele ya washabiki
wao watakuwa katika shinikizo za kushinda, jambo ambalo wamejiandaa
kukabiliana nalo.
Kwa upande wa maandalizi, Kim amesema
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wadhamini wa timu hiyo
Kilimanjaro Premium Lager wameiandaa vizuri kwani iko kambini kwa wiki
tatu sasa na kupata mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan iliyochezwa wiki
iliyopita nchini Ethiopia.
Stars iliifunga Morocco mabao 3-1
zilipokutana Machi 24 mwaka huu jijini Dar es Salaa. Lakini zilipokutana
hapa Marrakech mara ya mwisho mwaka 2011, Morocco iliibuka na ushindi
wa mabao 3-1.
Kim
amesisitiza kuwa kikosi chake kimepania kufanya vizuri katika michuano
hii ya mchujo ya Kombe la Dunia, ha hiyo inathibitishwa na matokeo ya
timu kadri inavyoendelea kucheza mechi za mashindano.
“Moja
ya mipango yetu katika mechi hizi za Kombe la Dunia ni kushinda
nyumbani, hilo hadi sasa tumelifanya kwa asilimia 100. Lakini ili tukae
vizuri zaidi tumekuja hapa Morocco kwa lengo la kupata matokeo mazuri,
ingawa tunajua mechi itakuwa ngumi,” amesema kocha huyo raia wa Denmark.
Kwa
Marrakech mechi hiyo imekuwa haizungumzwi mara kwa mara, na kubwa ni
kuwa Wamorocco wengi wanaamini kuwa timu yao ambayo hadi sasa ina pointi
mbili haina nafasi ya kusonga mbele katika hatua inayofuata ya michuano
hiyo.


Post a Comment