Na
Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UMOJA
wa Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA) umelalamikia ongezeko la bei za bima,
ukisema hazijazingatia uhalisia wa soko, pamoja na kukosa uhalali kwa kuwa
hazijashirikisha wadau wa sekta ya usafiri pamoja na jamii kwa
ujumla.
Msemamaji
wa Umoja wa wamiliki wa Malori Tanzania, Bwana Elias Lukumay akizungumza na
waandishi wa habari kuhusiana na malalamiko ya kampuni yake kuhusiana na
ongezeko la bima. Kulia kwake ni Makamu mwenyekiti wa TATOA, Bi Angellina
Ngalula.
Makamu
Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Malori Tanzania, Bi Angellina Ngalula
akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na
malalamiko ya umoja wao ya kupanda kwa bei za bima kwa asilimia 400. Kushoto
kwake ni msemaji wa TATOA, Bwana Elias Lukumay.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake, msemaji wa TATOA Bwana Elias Lukumay,
alisema wanasikitishwa na mamlaka ya uthibiti wa bima Tanzania (TIRA) kuongeza
malipo ya bima kwa asilimia 400 bila kutoa sababu za msingi lakini pia bila
kushirikisha wadau.
‘Majaribio
yetu ya kuzungumza na TIRA yameshindika baada ya TIRA kutojibu barua wala
mawasiliano rasmi ya kukutana nao, tofauti na makubalino yetu ya kikao cha mwezi
wa pili, kati yetu na wao ambapo tulikubaliana kuwa na kikao kabla ya mazungumzo
baina ya wadau na umma juu ya swala hili’ alisema Lukumay.
Akielezea
zaidi kuhusu malalamiko hayo, Lukumay alisema vigezo maalumu vya kupandisha bei
hizo haviko bayana lakini pia ushindani wa biashara haukuzingatiwa.
‘TATOA
inaamini kuna njia nyingi za kufata ili kupandisha bei, lakini kubwa zaidi ni
kuacha soko lijiendeshe lenyewe, kwani tuko kwenye soko huria’ alisema
Lukumay.
Kwa
upande wake makamu mwenyekiti wa TATOA, Bi Angellina Ngalula, alisema ongezeko
hili la bei ni kubwa mno kwa mara moja na litapunguza ushindani wa makampuni ya
usafirishaji ya ndani, lakini pia litaongeza bei za usafirishaji kwa kiwango
kikubwa sana na hivyo kuumiza uchumi wa nchi na mwananchi wa kawaida ataathirika
kwa bei za bidhaa kupanda.
‘Sababu
za TIRA kupandisha bei sio za msingi, sababu kama udanganyifu na kuongezeka kwa
kesi za bima pamoja na ajali za barabarani, sio sababu tosha za kupandisha bima
kwani kufanya hivyo kutaongeza malalamiko zaidi, na pia kuwavunja moyo wateja
waaminifu’ alisema Bi Ngalula.
Bi
Angellina pia alitoa wito kwa wahusika, yaani TIRA, kuacha tamaa na
kutokuendeshwa na genge la makampuni ya bima na kurudi kwenye meza ya
majadiliano ili kuweza kupata muafaka kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi
kwa maendeleo ya taifa.
‘Bila
TIRA kurudi kwenye meza ya majadiliano TATOA itabidi ichukue hatua mbadala kama
kwenda mahakamani na kugomea bei hizi mpya, jambo ambalo litasababisha usumbufu
kwenye uchumi wetu’ alisitiza Bi Ngalula
Post a Comment