Tume
ya vyuo vikuu Tanzania (TCU) imekifunga Chuo Kikuu cha Kimataifa
Tanzania(Tanzania International University -TIU) kudahili wanafunzi
ngazi ya shahada kutokana na kutotimiza masharti na vigezo
vinavyohitajika na Tume hiyo ili kuendesha mafunzo hayo.
Akizungumza
na waandishi wa habari Afisa habari mwandamizi wa Tume hiyo Edward
Makaku, (leo) jijini Dar es salaam amesema kuwa Chuo hicho kimefungwa
kutokana na kutotimiza masharti ya kufundisha kozi ya shahada ikiwa ni
pamoja na kukosa walimu wanaokidhi vigezo vya kufundisha ngazi hiyo.
“Tunapenda
kuwatangazia kuwa chuo hicho ni chuo kikuu binafsi na kimesajiliwa
kuendesha mafunzo yake kwa leseni namba CR1/028 na imepitiwa na Tume ya
vyuo vikuu na kuruhusiwa kutoa mafunzo yake kwa ngazi ya cheti,
stashahada na kozi za muda mfupi lakini sio kwa ngazi ya shahada, naomba
wananchi waelewe hili”, alisema Edward.
Aidha
Edward ameongeza kuwa mapema Aprili mwaka huu Tume ilitoa mwongozo
kukitaka chuo hicho kusitisha mafunzo yake katika ngazi ya shahada
mpaka kitakapokidhi masharti na kupatiwa usajili.
“Napenda
kutoa tahadhari kwa wananchi kutojiunga na chuo hicho kwa ngazi ya
shahada kwani hakijakidhi vigezo vya kutoa shahada kama inavyotakiwa na
Tume bali wanaweza kujiunga katika ngazi za cheti, stashahada na mafunzo
ya muda mfupi”, ameongeza.
Tume
imeutaka uongozi wa chuo hicho kuacha kudahili wanafunzi na kurudisha
ada na gharama nyinginezo kwa walosajiliwa ngazi ya shahada.
Post a Comment