Wakati Jeshi la Polisi nchini limesema limepata taarifa za mwonekano wa mtu aliyetupa bomu katika mkutano wa kampeni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Arusha, Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe amesema wabunge wake leo hawataingia bungeni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mbowe alisema
wabunge hao watawasili Arusha kwa ajili ya kuungana na wananchi pamoja na
wanachama kwenye msiba huo.
Alisisitiza kwamba kuanzia leo mahema yatawekwa viwanja
vya Soweto kwa ajili ya kuomboleza msiba huo na mara polisi wakimaliza
uchunguzi wao na kutoa majibu juu ya vifo hivyo, marehemu hao
watasafirishwa.
Wakati Mbowe anatoa kauli hiyo Waziri wa Mambo ya
Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza jana mjini Arusha na waandishi wa habari,
alisema taarifa za awali zinaonesha mlipuko huo ni bomu la kutupwa kwa mkono
(grumeti) na hivi sasa timu ya wataalamu ikiongozwa na Kamishna wa Operesheni
Maalumu wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja inaendelea na uchunguzi wa tukio
hilo.
Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta
Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari
ameahidi kupambana na kuhakikisha wahusika wanapatikana.
Alitoa taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari Dar es
Salaam na kusema hadi jana, watu waliothibitika kufa katika tukio hilo ni wawili
na 68 ni majeruhi.
Waliokufa ni Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha) wa
Chadema, Kata ya Sokoni 1, Judith Moshi (25) na mtoto aliyejulikana kwa jina
moja la Justin.
"Mpaka hivi sasa watu waliokufa ni wawili na wengine
68 wamejeruhiwa na mlipuko huo, lakini naahidi kuwa tutapambana na kuhakikisha
tunawapata wahusika," alisema Mwema.
Sanjari na kupatikana taarifa juu ya mtu aliyetupa
bomu, Mwema alisema timu ya jeshi hilo imetumwa kutoka makao makuu kwenda
Arusha kuongeza nguvu katika upelelezi.
Hata hivyo, hakufafanua zaidi juu ya mtuhumiwa huyo
kutokana na kile alichosema taarifa husika zinafanyiwa uchunguzi kabla ya
kuwakamata watu sahihi waliohusika na tukio hilo.
Kwa mujibu wa IGP Mwema, timu ya polisi kutoka Makao
Makuu inayoongozwa na makamishna wawili, imeondoka kwenda mkoani Arusha
kuongeza nguvu katika operesheni na upelelezi.
Timu hiyo inaongozwa na Kamishna wa Operesheni na
Mafunzo, Paul Chagonja na Isaya Mngulu kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya
Jinai, wakishirikiana na vyombo vingine vya ulinzi.
Alisema polisi inafanya operesheni kali nchini kote
kuhakikisha inawatia mbaroni watu wote waliowezesha, waliofadhili na waliotenda
uhalifu huo.
"Kikubwa wananchi waendelee kuwa watulivu na waendelee
kutoa ushirikiano kwa wakati wote uchunguzi ukiendelea," alisema.
IGP ametaka mtu yeyote atakayekuwa na taarifa za
wahalifu hao, atoe taarifa kupitia namba yake ya simu ambayo ni 0754 785557 au kwenye kituo chochote cha polisi ili
wakamatwe.
‘Kwa nini iwe Arusha’ hii ni kauli ya Mkuu wa Mkoa wa
Arusha, Mulongo aliyoitoa baada ya kutembelea majeruhi katika Hospitali za Mount
Meru, St Elizabeth pamoja na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre jijini.
“Nawapa pole sana ndugu zangu wa Chadema, na wana
Arusha kwa ujumla pamoja na watanzania. Lakini najiuliza kwa nini Arusha …tukio
hili limenihuzunisha sana na nawaomba tusiingize masuala ya kisiasa, tuache
polisi wachunguze tukio hili kwani timu ya wataalamu kutoka Jeshi la Ulinzi la
Wananchi Tanzania (JWTZ) pamoja na wataalamu wengine wanachunguza tukio hili na
wahusika watachukuliwa hatua.’’
Mulongo ambaye tukio hilo la juzi limekuja ikiwa ni
mwezi mmoja tangu kutokea kwa mlipuko katika Kanisa Katoliki la Joseph
Mfanyakazi la Olasiti, alisema jana anayefanya ulipuaji wa mabomu na kumwaga
damu za watu mbalimbali na wengine kufa, ipo siku Mungu
atamhukumu.
Kati ya majeruhi 59 waliolazwa kwenye hospitali hizo,
wawili wamehamishiwa Hospitali ya KCMC kutoka Hospitali ya AICC kwa matibabu.
Wagonjwa wengi wamelazwa hospitali ya Selian ambao ni 40. Hata hivyo, wanane
waliruhusiwa baada ya matibabu.
Mkuu wa Mkoa alisema anajisikia mnyonge kutokana na
matukio hayo mawili tofauti; mlipuko wa kanisani na la juzi wakati Chadema
ilipokuwa ikihitimisha kampeni zake za udiwani kwenye kata nne za Themi,
Kaloleni, Elerai na Kimandolu ambao hata hivyo uliahirishwa kutokana na tukio
hilo.
Mulongo alitaka wananchi wasihusishe na masuala ya
kisiasa badala yake wawaachie polisi kuchunguza tukio hilo. Kwa mujibu wa
Mulongo, watu kadhaa wamekamatwa.
Katika kipindi kisichozidi miezi miwili, mji wa Arusha
umeshuhudia majeruhi wasiopungua 130, na vifo vya watu watano vilivyotokana na
kurushwa mabomu na watu wasiojulikana katika mikusanyiko kanisani na kwenye
mkutano huo wa siasa wa Chadema.
Katika tukio la mwezi uliopita katika Kanisa Katoliki
la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, watu watatu walifariki na wengine wapatao 59
kujeruhiwa.
Mmoja wa watuhumiwa ambaye ni dereva wa pikipiki
maarufu kama bodaboda, Victor Ambrose alifikishwa mahakamani akidaiwa kuhusika
katika shambulio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, daktari wa
hospitali ya Selian, Paul Kisanga alisema walipokea wagonjwa 48 kabla ya wanane
kuruhusiwa.
Alisema miongoni mwa wagonjwa hao, wamo watoto watano
wanne wakiwa wa kiume na mmoja wa kike. Mtoto Fahad Jamal (7) amelazwa kwenye
wadi ya wagonjwa mahututi chini ya uangalizi wa madaktari.
Hospitali ya St Elizabeth wapo wagonjwa wanane na Mount
Meru imepokea wagonjwa tisa. Mganga Mkuu wa Mkoa wa hospitali ya Mount Meru,
Frida Mokiti alisema wamepokea miili ya marehemu wawili ambao ni Judith Moshi
(25) ambaye ni Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha) kata ya Sokoni 1, Jijini
Arusha pamoja na mtoto aliyejulikana kwa jina moja la Justin (13).
Kwa mujibu wa majeruhi wa tukio hilo, Abraham Samuel
waliona kitu kikiwa kwenye mfuko wa rambo kikirushwa juu na baada ya muda mfupi
walisikia vilio na wengine kuzimia.
Kitu hicho kilirushwa kabla ya Mwenyekiti wa Taifa wa
Chama hicho Taifa, Freeman Mbowe kuhitimisha kampeni za uchaguzi za udiwani wa
kata nne za Jimbo la Arusha Mjini.
Mlipuko huo unadaiwa kuwa ulitokea jirani na gari la
matangazo la Chadema, aina ya Mitsubishi Fuso lililokuwa karibu na jukwaa
alilokuwa akitumia Mbowe.
Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe amedai tukio hilo si la
bahati mbaya bali lilipangwa na kundi la watu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema
wabunge wa chama hicho leo hawataingia bungeni bali watawasili jijini Arusha kwa
ajili ya kuungana na wananchi pamoja na wanachama wa kwenye msiba
huo.
Kwa mujibu wa Mbowe, marehemu Judith atapelekwa mkoani
Kilimanjaro na Justin atapelekwa mkoani Tabora kwa ajili ya maziko mara baada ya
polisi kukamilisha uchunguzi juu ya tukio hilo.
Alisisitiza kwamba kuanzia leo mahema yatawekwa viwanja
vya Soweto kwa ajili ya kuomboleza msiba huo na mara polisi wakimaliza
uchunguzi wao na kutoa majibu juu ya vifo hivyo marehemu hao
watasafirishwa.
‘’Nimetembelea majeruhi jana
hospitalini lakini kwa Hospitali ya Selian, Arusha Lutheran Medical Centre
majeruhi ni wengi lakini walioumia sana ni watoto kuna mtoto mmoja amekatika
mkono na mguu ambaye ni Sharifa Jumanne na Amiri Ally ana vyuma vitatu mwilini
mwake,’’ alisema Mbowe.
Ingawa polisi imesema inaendelea na uchunguzi wa tukio
hilo kabla ya kutoa taarifa kamili, Mbowe aliwaambia waandishi wa habari kwamba
zipo taarifa kwamba shambulio hilo liliambatana na risasi za moto.
Chama cha Wananchi (CUF) kupitia kwa Mwenyekiti wake,
Profesa Ibrahim Lipumba, kimelaani tukio hilo na kutaka Serikali ichukue hatua
za haraka na kukamata waliohusika na matukio hayo iwe
fundisho.
“Hatuna sababu na tusijenge
utamaduni wa nchi yetu kugeuka eneo ambalo palipo na mkusanyiko mabomu
yanalipuka, Tanzania ni nchi ya amani, kwa matukio haya CUF tunalaani kwa nguvu
zote na kutoa pole kwa familia zilizoathirika,” alisema
Lipumba.
Lipumba alisema kitendo kilichofanyika katika mkutano
huo wa Chadema ni unyama wa kutisha wenye makusudi ya kundi fulani kutekeleza
azma yao dhidi ya chama, watu, kundi na viongozi.
Alisisitiza kuwa utamaduni huo wa kufanya unyama katika
mkusanyiko wa watu unapaswa kudhibitiwa mapema ili kuepusha madhara mengine
ndani ya jamii kwa kusababisha vifo, ulemavu wa kudumu na familia
tegemezi.
“Tumefikia hatua mbaya sana ya
kufanya siasa za mabomu huu ni utamaduni unaopaswa kukemewa na kupingwa, matukio
haya yanajirudia kutokana na Serikali yenyewe kuyakaribisha kwa kushindwa
kuwachukulia hatua kali wahusika, tunaomba dola ifanye ifanyalo katika uchunguzi
wake na kuwakamata na kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria,”
alisisitiza.
Post a Comment