Mkuu wa kitengo cha Sayansi ya Makosa ya Jinai Biologia na
Vinasaba kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali(GCLA) Bi. Gloria
Machuve(kulia) akizungumza na vyombo vya habari kuhusu matumizi ya Teknolojia
ya Vinasaba vya Binadamu kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika
katika ukumbi wa Idara ya Habari leo Jijini Dar es Salaam, kushoto ni Afisa
Habari kutoka Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Bi. Fatma Salum. Picha na FRANK MVUNGI-MAELEZO
*********************************
Na Fatma Salum - MAELEZO
Serikali kupitia
ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ina mpango wa kuanzisha utaratibu wa kutambua
raia wake kupitia taarifa za vipimo vya vinasaba vya binadamu maarufu kama DNA.
Akifafanua mpango huo katika mkutano wa waandishi wa habari
na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, Mkuu
wa Kitengo cha Sayansi ya Makosa ya Jinai Biolojia na Vinasaba Gloria Machuve
amesema kupitia mfumo wa taarifa za vinasaba utaiwezesha serikali kutambua raia
wake na wahamiaji wasio raia kutokana na taarifa zao kutokuwepo kwenye mfumo
huo.
Bi Machuve ameeleza kuwa mpango huo ukikamilika watanzania
wataweza kupimwa vinasaba vyao na taarifa zao zitawekwa kwenye mfumo rasmi wa
taarifa (Database) hivyo kurahisisha shughuli za uhamiaji ikiwemo utoaji wa
pasipoti na vitambulisho vya uraia.
Aidha mfumo huo utarahisisha utambuzi wa viungo vya miili ya
watanzania wanaofariki kwenye majanga kama moto na ajali za vyombo vya usafiri wakiwa
nje ya nchi kwani taarifa za vinasaba vyao zitakuwepo kwenye mfumo hivyo
zitaoanishwa na majibu ya vinasaba vya viungo hivyo na hatimaye serikali kupata
miili ya raia wake.
Pia Bi Machuve ameongeza kuwa kupitia mfumo huo utoaji wa
vyeti vya kuzaliwa utaambatana na taarifa kamili za vinasaba vya wazazi hivyo kurahisisha watu kupata vyeti vyenye
majina ya wazazi wao halali.
Naye Mkemia kutoka Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa
Serikali Fidelis Segumba amesema kuwa mfumo huo pia utasaidia kupunguza tatizo
la kubadilishwa watoto hospitalini kwani utawezesha kutambua mama halali wa
mtoto aliyezaliwa.
Segumba amesema faida nyingine za mfumo huo ni pamoja na
utambuzi wa viungo vya watu wenye ulemavu ngozi , kuondoa tatizo la watoto wanaoishi
katika mazingira hatarishi na kutambua wahalifu husika wa makosa ya ubakaji.
Ili kufanikisha mpango huo Segumba amesema serikali inabidi
kuongeza wataalamu na kuongeza fedha kwa ajili ya kununulia mitambo mingi ya
kufanyia kazi hiyo.
Post a Comment