Na James Katubuka
Uwajibikaji
katika Taasisi za Umma nchini ndiyo njia pekee itakayowezesha
utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP)
2011/12-2015/16, sanjari na Malengo ya Milenia (MDGs) . Kwa kuzingatia
hilo Serikali inaendelea kuhakikisha mazingira ya kazi yanaboreshwa ili
watumishi wawe na kasi zaidi kama sehemu ya utekelezaji wa mipango ya
maendeleo kwa kutoa huduma bora kwa Umma.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mh. Celina O.
Kombani (MB) amesema hayo hivi karibuni wakati akifungua mkutano kuhusu
Mchango wa Utumishi katika Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka
Mitano jijini Dar es Salaam.
“Kutokana
na kuthaminiwa kwa mchango wa watumishi wa umma katika kuleta maendeleo
Serikali nyingi ikiwepo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimewekeza
katika kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma ili waweze kuwajibika
ipasavyo” Mh. Kombani alisema.
Aliongeza
kuwa ubora wa Rasilimaliwatu katika utumishi wa umma ni suala muhimu
katika kuleta maendeleo ya nchi yoyote, hivyo Tanzania kwa kuwekeza
katika rasilimali hiyo itapiga kasi zaidi ya kimaendeleo.
“Mimi
ni miongoni mwa wanaoamini kwamba utendaji mzuri au mbaya wa Serikali
unahusishwa moja kwa moja na kiwango cha huduma zitolewazo na Serikali
kwa umma kupitia taasisi zake” Mh. Kombani alitoa angalizo.
Aidha,alisema
ukiilinganisha Tanzania na nchi za Barani Asia na Amerika ya Kusini
ambazo tuna historia zinazoshabihiana, inaonekana kuwa zimepiga hatua
ingawa mbinu zilizotumika toka nchi hizo zinakaribiana, hivyo kutokana
na uhalisia huo Serikali imefanya jitihada za kuboresha na kufikiri
upya namna ya kufikia malengo ya maendeleo haraka husani mchango wa
Utumishi wa Umma.
Mh.
Kombani alisema kwamba uwajibikaji wa watumishi wa Umma nchini ni chachu
ya kufikia malengo ya Kitaifa ya Milenia mwaka 2025, ikizingatiwa kuwa
malengo hayo yamejikita katika kuleta hali bora zaidi kwa maisha ya
wananchi, utawala bora, amani ,umoja na mshikamano na kujenga uchumi
imara.
Katika
kuchangia hilo, Mtendaji Mkuu Msaidizi wa Tume ya Mipango nchini Bw.
Florence Mwanri alisema mpango huo uliozinduliwa na Serikali mwaka 2011
kwa lengo la kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Milenia wa mwaka 2025,
umetoa vipaumbele ambavyo ni kuimarisha Miundombinu, Kilimo, Uvuvi na
Misitu, Kuboresha Elimu, na kuendeleza Sekta ya Utalii, Biashara na
Uchumi.
Hata
hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Dkt. Martern Lumbanga akitoa
mchango wake alisema ili kutekeleza mpango huo ipasavyo ni vizuri
kujifunza kutoka kwa nchi nyingine ambazo miaka thelathini iliyopita
zilikuwa sawa na Tanzania kimaendeleo.
Dtk.
Lumbaga aliainisha nchi hizo ni kama vile Jamhuri ya watu wa China,
Korea ya Kusini, Vietnam, Cambodia, Botswana na Ghana.
“Utawala
wa Kisiasa wa nchi hizi uliweza kuziunganisha Sekta za Umma na Sekta
binafsi kutumia Rasilimali muhimu katika kubuni mbinu mbalimbali za
kuwavutia wawekezaji wa nje kuwekeza katika sekta nyeti za uchumi
zilizoimarisha pato kwa kiwango cha juu” Dkt. Lumbaga alisema.
Katibu
Mkuu Kiongozi mstaafu Dkt. Lumbanga alisisitiza kwamba Sekta za Umma
zinatakiwa kuwa chombo cha kubuni na kuwezesha maendeleo kwa mifumo ya
kiufundi, kwa kuzingatia maadili ya kiutawala ili kujenga imani kwa umma
na kuhakikisha mpango huo wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP)
unaratibiwa kikamilifu.
Mkuu
huyo wa Utumishi mstaafu alisisitiza kuwa sekta ya umma nchini inatakiwa
kuwajengea uwezo Watumishi wake ili wawajibike ipasavyo, kuwa na
mawasiliano ya kiutendaji yaliyo hai muda wote na kutambua kwamba
Utumishi wa Umma upo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
Naye
Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu Bw. Phillemon Luhanjo akizungumzia kuhusu
changamoto zinazoukabili Utumishi wa Umma na mtazamo wa Sekta binafsi
dhidi ya Utumishi wa Umma nchini, alisema moja ya changamoto ni dhana
ya kukubali kubadili fikra na kuleta fikra endelevu zitakazokuwa chachu
ya maendeleo nchini katika nyanja za Kijamii, Kiuchumi na Kiutamaduni.
“Sekta binafsi zinatakiwa kushirikishwa katika kuandaa mipango yetu ya maendeleo” Bw. Luhanjo alisema.
Alifafanua
kuwa kwa upande wa sekta binafsi zinatakiwa kupewa fursa ya kuchangia
mawazo endelevu ili mpango wa maendeleo uwe wenye manufaa.
Bw.
Luhanjo aliainisha kuwa Taasisi za umma zinatakiwa kufikiri juu ya
mahitaji ya wananchi hususani suala la umasikini na kusisitiza Utumishi
wa Umma lengo lake si kujilimbikizia mali, bali lengo kuu ni kutekeleza
malengo madhubuti ya Serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Alisema
ili kukabiliana na changamoto zilizopo Serikali inatakiwa kuhakikisha
kuwa Utumishi wa Umma unaendelea kuimarika, mahusiano na Sekta binafsi
yanaimarishwa zaidi, bajeti ya nchi iimarishwe ili kupunguza utegemezi
wa wafadhili wa nje na Sekta ya Umma kutambua mchango wa Sekta binafsi
katika kuleta kasi zaidi ya maendeleo.
Pamoja
na hayo, Katibu Mkuu mstaafu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi
wa Umma Bw. Joseph A. Rugumyamheto akizungumzia kuhusu ushirikishwaji na
wajibu wa Utumishi wa Umma katika kuleta maendeleo nchini alisema
jukumu la Utumishi wa Umma katika kuleta maendeleo ya kitaifa limekuwepo
toka kipindi cha uhuru mpaka sasa.
Bw.
Rugumyamheto alisisitiza Utumishi wa Umma ndio chombo pekee chenye
jukumu kubwa la kuwezesha uratibu wa programu za maendeleo za kijamii na
kiuchumi hapa nchini.
Katibu
Mkuu mstaafu alisema wachambuzi wa masuala mbalimbali wameandika kuwa
Utumishi wa Umma katika kipindi cha Uhuru ulikuwa unazingatia taaluma na
ulikuwa ni chombo kilichowajibika kikamilifu kutimiza matakwa ya
Kisiasa na Kijamii. Hivyo, kwa sasa kasi iongezeke zaidi.
Bw.
Rugumyamheto aliainisha kuwa kwa sasa Utumishi wa Umma una wigo mkubwa
wa uwepo wa wataalamu wengi wenye ujuzi katika fani mbalimbali tofauti
na ilivyokuwa hapo awali, pia matumizi ya teknolojia hususani maendeleo
ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yamerahisisha uandaaji
wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kusimamia utekelezaji wake, hivyo
Utumishi wa Umma uliopo una nafasi kubwa ya kuwahudumia wananchi
ipasavyo na kufikia malengo kwa haraka.
Akizungumzia
kuhusu hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Vijana nchini
Nigeria Dkt. Tunji Olaopa alisema kinachohitajika ni kuwa na mpango
utakaoiwezesha kuondokana na dhana ya utendaji wa mazoea na kutoka
katika fikra ya utamaduni wa kitawala wa kirasimu na kujikita katika
mfumo wa ujasiriamali ikiwamo ubunifu katika kushughulikia masuala ya
mishahara na masilahi ya watumishi ili kuwajengea morali na uwajibikaji
kwa umma.
“Utawala
makini na uliojitolea kuutumikia umma ndio nguzo ya maendeleo, na
ikumbukwe kwamba Utumishi wa Umma ukishindwa kuwajibika ipasavyo na
masuala yote yahusuyo maendeleo yanakwama” Dkt. Olaopa alisema.
Aidha,
Dkt. Olaopa aliipongeza Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi zenye sifa
ya kuwa na utawala bora unaoheshimika Barani Afrika.
Mtafiri
Adamolekun katika tafiti yake ya mwaka 2005 aliyoitoa mwaka 2009 kuhusu
masuala ya Utawala Barani Afrika imeainisha kuwa Tanzania ni moja kati
ya nchi zilizofanya mabadiliko makubwa katika Sekta ya Umma. Utafiti huo
ulihusisha nchi nyingine kama Benin, Burkina Faso, Ethiopia, Ghana,
Kenya, mali na Senegal.
Akichangia
mada, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Prof. Rwekaza
Mkandala alisema Rasilimaliwatu ni msingi wa maendeleo,hivyo ni lazima
nchi kuwa na Watumishi wa Umma waliopewa mafunzo bora na ujuzi unaokidhi
mahitaji.
Prof.Rwekaza
alisema kuwa Watumishi wa Umma wanatakiwa kuwa na uzalendo na nchi yao
na wasiohitaji kusimamiwa ili kutekeleza majukumu yao.
Alisema
“ili Utumishi wa Umma ufanikiwe unahitaji kwenda sambamba na Teknolojia
kulingana na mazingira halisi yaliyopo na muda husika, pia unahitaji
kuwa na vitendea kazi mahimu kufanikisha hilo ikiwamo mifumo ya kompyuta
itakayoiwezesha mifumo mbalimbali niliyobuniwa na Serikali kufanya kazi
ipasavyo”.
Naibu
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejjimenti ya Utumishi wa Umma Bw. HAB
Mkwizu alisema Serikali imeainisha maeneo matano ya utekelezaji wa
mpango wa maendeleo ambayo ni kilimo, elimu, nishati, miundombinu na
rasilimali na hivi sasa kuna chombo kitakachosimamia na kutathmini
mipango itakavyotekelezwa, chombo hicho kinaitwa Presidential Delivery
Bureau.
(Mwandishi WA makala hii ni Afisa Habari, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma)
Post a Comment