WAKATI ushindi wa kishindo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) jijini Arusha ukimweka pabaya Meya wa Jiji la Arusha, mazito
mengine yameibuka baada ya Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Sipora Liana,
kutoboa siri kubwa.
Mbele ya madiwani wapya wa CHADEMA wakiongozwa na Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema, Liana alisema alikuwa anafikiria ‘kukimbia’
kutokana na hali tete ya usalama kugubika jiji hili.
Katika kikao kifupi cha utambulisho wa madiwani hao wapya, Liana
alisema: “Wakati ninakuja hapa (Arusha) kulikuwa na
taarifa za vurugu
na maandamano, jambo ambalo lilinifanya nifikirie kama hali ingeendelea
kuwa hivyo nitaomba niondoke, lakini nimeridhishwa na utulivu
uliokuwepo jana (juzi),” alisema Mkurugenzi Liana.
Kauli hiyo ilimfanya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kumweleza
mkurugenzi huyo kuwa hata wao CHADEMA wataendelea kumpa ushirikiano wa
kutosha kuhakikisha kuna kuwapo maendeleo ya wananchi wa jiji hilo, hasa
kutokana na namna alivyoonyesha ushirikiano wakati wa uchaguzi huo.
Alisema kuwa halmashauri hiyo inakabiliwa na kashfa za ufisadi wa
mabilioni ya fedha za wananchi, jambo alilosema kuwa madiwani na wabunge
wa CHADEMA wako tayari kumsaidia kuyafumua yote ili wayashughulikie
kwa masilahi ya wananchi wa Arusha na si vyama vya siasa.
“Kwa namna ulivyotoa ushirikiano (siku ya uchaguzi) kila nilipokupigia
simu hata kwa suala dogo ulikuwa unahakikisha linapatiwa ufumbuzi hata
zile taarifa kuwa uliletwa kuhakikisha CHADEMA haichukui hata kiti
kimoja cha udiwani sasa imeondoka,” alisema Lema.
Lema alisema kuwa nao wameanza kupata imani na mkurugenzi huyo kwa
namna alivyoendesha uchaguzi huo, kwani awali waliambiwa kuwa aliletwa
kwa ajili ya kuhakikisha CHADEMA hairudishi kata hizo.
Mkurugenzi huyo alimjibu Lema kuwa yeye yupo kwenye jiji hilo kwa
ajili ya kuwahudumia wananchi wote bila kujali itikadi za vyama, huku
akiwaahidi ushirikiano madiwani hao ambapo alisema kuwa
atahakikisha fedha za wananchi zinalindwa, huku akisisitiza kuwa jambo
hilo anaweza kulifanya hata bila madiwani, kwani hata madiwani hao
nao wakienda kinyume huwa anawakamata.
“Diwani aliyechaguliwa na wananchi ndiye nitakayefanya naye kazi, ila
na yeye akileta masuala binafsi, hapo na mimi atanikuta,” alisema Liana,
jambo lililofanya watu wote kucheka.
Naye Katibu wa CHADEMA Kanda ya Arusha, Amani Golugwa, alimpongeza
mkurugenzi huyo kwa namna alivyosimamia uchaguzi huo na kumtaka aendelee
hivyo hivyo ili ile dhana kuwa CHADEMA ndio wanasababisha vurugu Arusha
iondoke na ukweli ujulikane kuwa wanaosababisha vurugu mara zote ni
watawala.
Madiwani hao wapya na kata zao kwenye mabano, Bryson Ngowi
(Kimandolu), Emanuel Kessy (Kaloleni), Millace Kinabo (Themi) na
Jeremiah Mpinga (Elerai), ambao walisindikizwa na msafara mkubwa wa
viongozi na mashabiki wa CHADEMA ulioanzia kwenye ofisi zao za Mkoa wa
Arusha zilizoko Ngarenaro na kupita kwenye Barabara ya Sokoine kuelekea
kwenye ofisi hizo za mkurugenzi, hali iliyoamsha shamrashara kwa
wananchi kila walipokuwa wakipita.
Msafara huo uliojumuisha magari, pikipiki na waenda kwa miguu, ambapo
madiwani hao pamoja na Lema walikuwa kwenye gari la wazi, hali
iliyosababisha shughuli kusimama kwa muda kila ulipokuwa ukipita, huku
kelele za zamu ya meya kung’oka zikivuma kila mahali.
TANZANIA DAIMA
Post a Comment