Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiufungua Mkutano wa
31 ya Kimataifa wa Tathmini ya Elimu ya Afrika unaofanyika katika Hoteli
ya Ngurdoto Mkoani Arusha.
Baadhi
ya wajumbe wa mkutano wa 31 wa Kimataifa wa Jumuiya ya Tathmini ya
Elimu ya Afrika wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Mkutano huo
iliyotolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
kwenye hoteli ya Ngurdoto Mkoani Arusha. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
***************************************
Na Othman Khamis Ame
Mataifa
ya Bara la Afrika yana wajibu wa kuhakikisha kwamba Elimu inayotolewa
na kufundishwa katika Taasisi zote za Elimu Barani humu inakuwa bora na
kumnufaisha vilivyo Mtoto wa Afrika.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati
akiufungua Mkutano wa 31 wa siku Tano wa Kimataifa wa Jumuiya ya
Tathmini ya Elimu ya Afrika { AEAA } unaofanyika katika Ukumbi wa
Victoria wa Hoteli ya Ngurdoto iliyopo Mkoani Arusha Tanzania.
Balozi
Seif aliwaambia washiriki wa Mkutano huo kutoka Nchi 28 Barani Afrika
sambamba na wadau wa Elimu wa Nchi washirika Duniani kwamba Serikali za
mataifa hayo wanachama ziangalie njia muwafaka katika kuona hadhi na
ubora wa elimu inaendelea kupatikana kwenye mataifa yao.
Alisema
mara nyingi wananchi na hasa wazazi wa wanafunzi wamekuwa wakilalamikia
kushuka kwa kiwango cha elimu suala ambalo linafaa kuchukuliwa hatua za
ziada katika kupatikana kwa vifaa ambavyo ndivyo vinavyochangia
kupunguza ubora wa elimu.
Alisema
hivi sasa kiwango cha elimu kinaonekana kuchuka kinachochangiwa na
ukosefu wa vifaa vya sayansi jambo ambalo linahitaji mazingatio makubwa
katika mabadiliko ya viwango bora vya elimu.
Balozi
Seif alieleza kuwa Mkutano huo wa Tathmini ya Elimu ya Afrika umekuja
muda muwafaka kwa wanachama hao katika kubadilisha uzoefu wa tathmini ya
elimu ambapo utasaidia kujenga nguvu za pamoja katika kukabiliana na
changamoto zinazoikabili sekta ya elimu Barani Afrika.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba elimu ndio uti wa
mgongo wa maendeleo popote pale duniani, hivyo jitihada za ziada
zinapaswa kuchukuliwa katika kuona eneo hilo linajengewa mazingira
mazuri na ya uhakika.
“
Na matumaini makubwa kwenu washiriki wa Mkutano huu wa Tathmini ya
Elimu ya Afrika kwamba mtatumia fursa na nafasi ya mkutano huu kuondoka
na wazo litakalosaidia kuimarika kwa ubora wa elimu Barani Afrika ”.
Alifafanua Balozi Seif.
Aliwakumbusha
wajumbe wa Mkutano huo kuelewa kwamba Mataifa ya Afrika yamejikubalisha
kuimarisha Mpango wa Elimu kwa wote na Malengo ya Milenia hadi ifikapo
mwaka 2015 ikiwa ni hatua inaozitaka nchi hizo kufikia.
Hata
hivyo Balozi Seif alisisitiza umuhimu wa kukabiliana na tatizo la
kuvuja kwa mitihani ambalo kwa kiasi kikubwa limekuwa likichangia
kushuka kwa kiwango cha elimu katika mataifa mengi dunia likiwemo Bara
la Afrika.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitolea mfano wa mpango wa uimarishaji wa
elimu unaofuatwa Zanzibar unaofuatwa kuanzia Maandalizi,Msingi,
Sekondari hadi chuo Vyuo Vikuu unaweza kusaidia katika baadhi ya Mataifa
ya Afrika endapo utafanyiwa utafiti na Jumuiya hiyo ya Tathmini ya
Elimu ya Afrika.
Mapema
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tathmini ya Elimu ya Afrika { AEAA }
Dr. Joyce Lazaro Ndalichako alisema lengo la Mkutano huo ni kuangalia
njia bora za kuimarisha hadhi ya Elimu katika Mataifa wanachama wa {
AEAA }.
Dr.
Joyce alisema kwamba Jumuiya yake imekuwa ikitumia njia kadhaa ikiwemo
kuwashirikisha wataalamu sambamba na Kamati za Utafiti ili kuhakikisha
lengo hilo linafikiwa vyema.
Alisema
upo utaratibu wa kubadilishana vipindi na uzoefu katika utunzi wa
mitihani kwa hatua ya kujenga nguvu za pamoja za kuimarisha kiwango cha
elimu Barani Afrika.
Akimkaribisha
Mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mkutano huo Naibu Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.
Phillip Mulugo alisema wakati umefika kwa Taasisi za elimu kuhakikisha
ongezeko la Maskuli popote pale linakwenda sambamba na ubora wa elimu.
Mh.
Mulugo alifahamisha kwamba mfumo huo ukitekelezwa kwa pamoja unaweza
kusaidia kupata wataalamu wenye kiwango kinachokubalika vyema kitaifa na
Kimataifa.
Mkutano
huo wa 31 wa Kimataifa wa Jumuiya ya Tathmini ya Elimu ya Afrika
uliojumuisha washiriki wa Mataifa 28 ya Bara la Afrika umehudhuriwa pia
na wadau wa Elimu kutoka mataifa zaidi ya kumi Duniani zikiwemo
Uingereza,Marekani, India, China na Ujerumani.
Post a Comment