Na Anna Nkinda- Gaborone, Botswana
Jamii
imetakiwa kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa hakuna
unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto wa kike pia inawalinda ili wasiingie
katika mazingira hatarishi yatakayowapelekea kupata kupata maambukizi
ya Virusi vya Ugonjwa wa Ukimwi (VVU) .
Wito
huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na
waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa kamati
maalum ya viongozi wanaoshughulikia huduma na elimu ya afya ya uzazi na
ujinsia kutoka nchi za Jumuia ya Afrika ya Mashariki (EAC) na Jumuia ya
Ushirikiano wa Maendeleo ya Kikanda kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)
uliofanyika katika Hoteli ya Lansmore Masa Square iliyopo mjini
Gabarone nchini Botswana.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) alisema huwa anajisikia uchungu pale anaposikia kuwa mtoto wa
kike amebakwa au amefanyiwa ukatili wa kijinsia na kuiomba jamii nzima
iweze kumsaidia na kumkomboa mwanamke.
“Kama
jamii yetu ya nchi za kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika itaungana
kwa pamoja na kuamua kumsaidia mtoto wa kike itawezekana kwani hata
kama watoto hawa wakipata huduma bora ya afya bila ya kuwapatiwa elimu
hakuna jambo la maana watakalolifanya kwakuwa watakuwa na afya
bora lakini watakosa kujiamini kwani hawana elimu”, alisema Mama
Kikwete.
Akiongelea
kuhusu Taasisi ya WAMA alisema kitaaluma yeye ni mwalimu na wakati
anafundisha aliona changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto wa kike
na pale alipoanzisha taasisi hiyo aliamua kuwasaidia watoto wa kike
ambao ni yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi ambao wamekosa
nafasi ya kwenda shule ili nao waweze kusoma kama watoto wengine.
Mama
Kikwete alisema, “ Tuna shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mfano ya
WAMA-Nakayama ambayo ina jumla ya wanafunzi 325 wa kidato cha kwanza
hadi cha nne pia Taasisi ya WAMA inawagharamia masomo wanafunzi
wasichana 300 ambao wanasoma shule mbalimbali za Sekondari katika mikoa
yote ya Tanzania.
Alimalizia
kwa kuiziomba nchi wanachama wa EAC na SADC kutunga na kufuata sera na
sheria zitakazomlinda mtoto wa kike kwa kufanya hivyo ataepukana na
unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo ubakwaji, udhalilishwaji, kutopewa
huduma bora za afya na elimu.
Mkutano
huo wa siku mbili uliandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la
Kupamba na Ukimwi (UNAIDS) , UNFPA, Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia watoto (UNICEF), Shirika la Chakula Duniani (WHO),
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Sayansi na Utamaduni
(UNESCO) lengo kuu likiwa ni kuhakikisha kuwa vijana wote wanapata
elimu kuhusiana na afya ya uzazi na ujinsia na stadi za maisha jambo
ambalo litawasaidia kufahamu zaidi ugonjwa wa Ukimwi.
Post a Comment