Babati. Mwanasiasa mkongwe nchini, Mateo Qaresi
ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali ya Awamu ya Pili na
Tatu, ikiwamo uwaziri na ukuu wa mkoa, amesema Tanzania kama taifa halina dira
wala mwelekeo na matokeo yake mambo yake yamekuwa yakienda bila utaratibu huku
akishauri Katiba Mpya iruhusu Rais ashtakiwe.
Waziri wa zamani
wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Mateo Qaresi akitoa maoni yake juu ya Rasimu ya
Katiba Mpya katika kikao cha wajumbe wa Baraza la Katiba la wilayani Babati,
jana. Picha na Mussa Juma
Akitoa maoni kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya jana,
Qaresi ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ya Babati amepinga
mapendekezo mengi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) akisema ni muhimu Katiba Mpya
itaje dira ya taifa.
Qaresi katika utumishi wake wa umma, amewahi
kuwa Waziri wa Ushirika na Masoko kati ya mwaka 1989 - 1990, Waziri wa Utumishi,
1996 - 2000 na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya tangu 2000 hadi Februari 2006.
“Hivi hawa viongozi wanajua tunapoelekea, leo
hii ukiulizwa dira yetu ni nini hakuna anayejua, bali tunajiendea tu,”
alisema.
Alisema kwa mfano, Wamarekani licha ya kuwa na
vyama viwili vikubwa, lakini dira yao ni ubepari, Wachina au Warusi dira yao ni
ujamaa (ukomunisti) na kwa mataifa yote yanazo dira, lakini Tanzania dira yake
haijulikani.
“Basi, watangaze kama sisi ni mabepari, wajamaa
au waliberali, ili tujue na tufuate misingi hiyo siyo kila kiongozi kuwa na
utaratibu wake, wengine ruksda wengine hivi lazima tubadilike,” alisema
Qaresi.
Rais aondolewe kinga, ashtakiwe
Akizungumzia ibara ya 83 ya Katiba ambayo
inazungumzia kinga za Rais, alisema ni muhimu sasa kuondolewa kwani marais
wamekuwa na viburi , hawashauriki.
Alisema kuna makosa ambayo marais wanayafanya
ambayo yanafaa kushtakiwa, lakini kutokana na kuwa na kinga, imekuwa ni vigumu
kufanya hivyo.
“Katiba ijayo lazima sasa iondoe kinga kwa
marais ili mtu yeyote aweze kumshtaki Rais na hatua za kisheria ziweze
kuchukuliwa,” alisema Qaresi.
Kuhusu hoja za Kundi la G55 ambalo yeye alikuwa
mwasisi na mwanachama la kutaka Serikali ya Tanganyika, alieleza kuwa Serikali
tatu haziwezi kuepukika na kuwataka wanasiasa wakiwamo wa CCM kuacha
ushabiki.
Qaresi ambaye alikuwa mwenyekiti wa wabunge wa
kundi ya G55 mwaka 1993 waliotaka Serikali ya Tanganyika, alisema si Serikali
mbili au moja ambazo sasa zitawezekana tena, kwani Wazanzibari wanataka uhuru
wao wa kujiamulia mambo na kama ushabiki ukiacha muungano utavunjika
kabisa.
“Hoja kuwa Serikali tatu ni gharama kubwa si
ukweli, gharama kubwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma na ubadhirifu
serikalini na siyo kuwa na Serikali tatu. Leo hii katika bajeti ya nchi ya
Sh18.2 trilioni, ni trilioni tano tu ndiyo za maendeleo, sasa tuna Serikali tatu
hapo,” alihoji.
Alisema Serikali inajiongezea matumizi makubwa
bila sababu ikiwapo kuanzisha wakala katika sekta mbalimbali na kutoa mfano wa
Mkurugenzi mkuu wa Wakala kama EWURA ambaye ana mshahara mkubwa zaidi ya katibu
mkuu wa wizara.
“Serikali inajenga majengo makubwa bila sababu,
mfano jengo la RC (Mkuu wa Mkoa) wa Manyara ni kubwa kupita kiasi hadi wahudumu
wana ofisi na kuna vyumba havina watu sawa na jengo la halmashauri ya Mji wa
Babati, haya ni matumizi mabaya ya fedha za umma,” alisema.
Alisema wakati wao walipokuwa wanataka Serikali
ya Tanganyika, hali haikuwa mbaya, lakini sasa hali ni mbaya zaidi na mahitaji
ni makubwa zaidi na haiwezekani upande mmoja tu wa Muungano kuendelea
kung’angania mfumo uliopo.
“Malalamiko ya kutaka Serikali tatu, hayajaanza
leo, kilichomwondoa madarakani aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Abdu Jumbe ni hoja
hiihii na viongozi kadhaa waliondolewa pia, nadhani ndiyo sababu hata leo kuna
viongozi wa Zanzibar wanaogopa kuwa wakweli na kudai nao wanataka Serikali
mbili,” alisema Qaresi.
Alifafanua kuwa kwa sasa Zanzibar imefika mbali
zaidi kwani ina wimbo wake wa taifa, bendera, majeshi yake kama KMKM na JKU na
hata wakati wa Sherehe za Mapinduzi Rais wao (Dk Ali Mohammed Shein) ndiye
anakagua gwaride kama Amiri Jeshi Mkuu.
“Ni vyema tuache ushabiki wa kisiasa na
kuogopa, sasa kama tunataka Muungano ni Serikali tatu tu na wala siyo mbili au
moja,”alisema.
Hoja ya uwazi
Qaresi alisema anashangaa kuna watu wanapinga
uwazi kwenye tunu za taifa, kwani anashindwa kujua ni kwa manufaa ya nani.
“Kila mtu sasa anataka uwazi katika matumizi ya
umma, utendaji serikalini na sehemu nyingine, sasa hawa wanaopinga wanataka
nini,” alihoji.
Katika utumishi wake wa umma, amewahi kuwa
Waziri wa Ushirika na Masoko kati ya mwaka 1989 hadi 1990, Waziri wa Utumishi
mwaka 1996 hadi 2000 na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya tangu 2000 hadi 2006.
Pia, alikuwa Mbunge wa Babati nwaka 1985 hadi
1995 na baadaye Mbunge wa Jimbo la Babati Magharibi mwaka 1995 hadi 2000
aliposhindwa katika kura za maoni ndani ya CCM.
Chanzo Mwananchi.
Post a Comment