Na Hassan Ali
Ame
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) visiwani Zanzibar
kimemtuhumu Mwenyekiti wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa
Ponda, kuwa anaendesha kampeni za uchochezi wa kidini.
Uchochezi huo umedaiwa kuhatarisha amani ya
nchi, hivyo kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kumchukulia hatua za
kisheria.
Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu
(NEC) Zanzibar, Itikadi na Uenezi, Waride Bakari Jabu, alisema jana kuwa ni wiki
moja sasa tangu Ponda afanye mihadhara kwenye misikiti ya Mbuyuni, Kwarara na
Nungwi kisiwani Unguja.
Waride alisema kuwa hotuba za Sheikh Ponda
alizozitoa kwa nyakati tofauti kwenye misikiti hiyo zinapandikiza mbegu ya
chuki, kuondosha upendo na kuhatarisha amani.
Alisema matamshi yake ni hatarishi kwa amani na
utulivu uliopo, kwani anawataka Waislamu kupigana vita ya dini (Jihad) na
kushiriki harakati za kuikomboa Zanzibar, kwa madai kuwa serikali iliyoko
madarakani inawakandamiza na kuwanyanyasa wananchi.
“Sheikh Ponda ni hatari, anapanda shari na
chuki miongoni mwa wananchi, anahamasisha wananchi wafanye uasi, kulipiza
visiasi na kutaka waingie barabarani kwa maanadano ya kutetea haki kama
inavyotokea Misri,” alisema.
Aidha, alisema CCM imeshangazwa na ukimya wa
vyombo vya ulinzi na usalama wa raia kumtazama kiongozi huyo bila ya kumchukulia
hatua za kisheria wakati akiwatukana matusi ya nguoni viongozi wa serikali na
chama tawala.
Aliongeza kuwa Sheikh Ponda huenda anatumiwa na
mtandao wa vurugu ili kuharibu na kuvuruga amani ambapo hamu yake ni kuona damu
ya wananchi ikimwagika na nchi ikiingia kwenye machafuko.
Kwa mujibu wa Waride, kitendo cha Ponda
kulitumia jukwaa la dini na kufanya siasa misikitini hakikubaliki na kwamba
kikiachiwa kiendelee kinaweza kuleta madhara na mgawanyiko.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa,
alisema jeshi hilo limeanza kumtafuta Sheikh Ponda tangu walipopokea taarifa za
kuendesha mihadhara ya uchochezi katika baadhi ya misikiti, ikiwa na lengo la
kuibua chuki.
Mussa alisema kitendo anachokifanya kinakwenda
kinyume cha sheria, hivyo kumtaka popote alipo ajisalimishe kwa hiari
yake.
Tangu kuingia visiwani Zanzibar, Sheikh Ponda
amekuwa akifungamana na viongozi wa Jumuiya ya Uamsho wakipinga kitendo cha
viongozi wa jumuiya hiyo kuendelea kubakia mahabusu baada ya kukamatwa na
kufunguliwa mashtaka ya uharibifu wa mali na kuhatarisha usalama wa taifa.
Viongozi hao wa Uamsho wako mahabusu baada ya
Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar, Ibrahim Mzee Ibrahim, kuwasilisha ombi la
kufunga dhamana yao kwa kutumia sheria ya Usalama wa Taifa na marekebisho yake
ya mwaka 2002
Chanzo - Tanzania
Daima
Post a Comment