Msemaji
wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac J. Nantanga akizungumza na
Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio yaliyofikiwa
na Tanzania kuwarejesha kwao wakimbizi waliokuwa hapa nchini. Kulia
ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Uratibu wa
Mawasiliano ya Serikali, Bi. Zamaradi Kawawa.
*********************************
Serikali
ya Tanzania imewarejesha kwao kwa hiari wakimbizi wapatao 569,018 toka
nchi za Maziwa Makuu waliokuwa wamehifadhiwa hapa nchini kutokana na
machafuko katika nchi zao. Kati ya hao 502,358 walitoka nchini Burundi
na 66,660, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Wakimbizi
hawa wamerejeshwa kwao kufuatia zoezi lililoanzishwa rasmi mwaka 2002
kwa wakimbizi toka Burundi na mwaka 2005 kwa wakimbizi toka Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRS), baada ya usalama katika nchi zao kuimarika.
Sambamba
na mafanikio haya, pia kambi 12 kati ya 13 zilizokuwa zikitumika
kuwahifadhi wakimbizi hawa zimefungwa, na hadi sasa ni kambi moja tu ya
wakimbizi ya Nyurugusu, wilayani Kasulu mkoani Kigoma ndiyo iliyobakia
ikiwahifadhi wakimbizi kutoka DRC (63,728), Burundi (4,153) na nchi
nyingine mchanganyiko za Kiafrika (212).
Tanzania
inajulikana kimataifa kama nchi mojawapo ambayo imechangia kwa kiasi
kikubwa kutoa hifadhi kwa wakimbizi wanaokimbia nchi zao kutokana na
machafuko ya kiaiasa ambapo mwaka 1995 idadi yao ilifikia zaidi ya
milioni moja.
Lengo
la Serikali ni kuona kuwa suala la kuhifadhi wakimbizi hapa nchini
linafikia ukomo na juhudi zinaendelea kuona kuwa hata Kambi ya Nyarugusu
ambayo ndiyo kambi pekee iliyobakia inafungwa baada ya wakimbizi walio
katika kambi hiyo kurejeshwa kwao, pale hali ya usalama nchini DRC
itakapokuwa imeimarika.
Kuondoka
kwa wakimbizi hawa sasa kunatoa nafasi kwa Serikali na wananchi kutumia
kwa shughuli nyingine za kimaendeleo maeneo makubwa yaliyokuwa
yanatumika kuhifadhi wakimbizi, lakini pia kunatoa nafasi nzuri ya
kuweza kukabiliana na changamoto za kiusalama katika maeneo hayo ambayo
yapo katika mikoa ya mpakani mwa nchi.
Serikali
inapenda kuishukuru Jumuiya ya Kimataifa kupitia Shirika la Umoja wa
Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), kwa misaada ya hali na mali
waliyotoa na wanayoendelea kutoa kusaidia hifadhi ya wakimbizi hapa
nchini.
Pia
Watanzani wote na hasa wale wa mikoa ya Katavi, Kigoma na Kagera kwa
ushirikiano waliotoa kwa wakimbizi waliokuwa wamehifadhiwa katika maeneo
yao, na nchi za Burundi, Congo kwa ushirikiano wao uliowezesha
kuwarejesha raia wao waliokuwa wamehifadhiwa hapa nchini.
Mashirika
mengine ambayo pia yalihusika na yanaendelea kutoa huduma za kibinadamu
kwa wakimbizi ni pamoja na Shirika la Chakula Duniani (WFP), Mfuko wa
Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF), Kamati ya Kimataifa ya
Uokozi (IRC), na Shirila la Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS).
Imeandaliwa na Felix Mwagara
KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
Post a Comment