Wakati sakata la kodi ya simu ya Sh1,000 kwa kila laini ya simu kwa mwezi, inayotakiwa kulipwa na watumiaji wa simu likiwa limerejeshwa bungeni na Serikali, Spika wa Bunge, Anne Makinda ameibuka na kusema fedha hiyo ni ndogo na kila Mtanzania ataweza kuilipa.
Spika Makinda alishangazwa na Mtanzania
anayeshindwa kupata Sh1,000 kwa mwezi, kufafanua kuwa kama wananchi wataifanya
nchi yao kuwa rahisi, watalalamika na umaskini mpaka siku watakayokufa. Julai 30
mwaka huu, Waziri wa Fedha, William Mgimwa alikaririwa akisema suala hilo
litamalizwa bungeni kisheria na kwamba wameanza kutekeleza agizo la Rais Jakaya
Kikwete la kuitaka Wizara ya Fedha kukutana na wadau wengine, kuangalia namna ya
kupata vyanzo vingine vya mapato mbadala na kodi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya
ufunguzi wa mafunzo ya wajumbe wa kamati ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC),
Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Bajeti, Spika Makinda alisema, “Haya
maendeleo tunayoyataka sisi kama Watanzania yatapatikana kwa kulipa kodi, hata
vitabu vitakatifu vinasema kila mtu lazima achangie,”alisema.
Alisema bila kukusanya kodi nchi itashindwa
kujiendesha na kusisitiza kuwa kama angeulizwa kuhusu masuala ya ulipaji kodi
angesema uanzishwe hata mfuko maalumu wa kuwasaidia vijana.
Alisema kwa kuwa suala hilo la kodi hivi
sasa ni sheria, mabadiliko yake ni lazima yarudi bungeni na kwamba haamini
katika kushindwa kulipa fedha hiyo.
“Tunataka kufanya vitu vingi na hatuwezi
kuitegemea Serikali katika kila kitu sasa yenyewe itatoa wapi fedha. Hayo ni
maoni yangu lakini hiyo ni sheria,” alisisitiza Spika
Makinda.
Post a Comment