Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Wakulima tumbaku walizwa Sh. bilioni 7

 

   
Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Christopher Chiza
******
UFISADI wa Shilingi bilioni saba umebainika katika Chama Kikuu cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (Wetcu), huku baadhi ya vyama vya msingi vya ushirika vikilalamika kukatwa fedha za pembejeo bila kupelekewa.

Imebainika kwamba, wakulima wamekuwa ‘wakiibiwa’ kwa mfumo wa kupelekewa pembejeo ‘hewa.’ Madai hayo yamebainisha kwamba wanaonufaika na wizi huo kwa wakulima ni vigogo wa Wetcu wakishirikiana na mawakala wanaosafirisha pembejeo hizo.

Akizungumzia na NIPASHE kwa simu jana, Mbunge wa Sikonge (CCM), Said Nkumba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa wabunge wa Mkoa wa Tabora, alisema kiasi hicho kikubwa cha fedha kinamwelemea mkulima wa tumbaku huku kukiwa na usambazaji hewa wa pembejeo.

Alisema wakulima wa zao hilo wamelalamika kwa muda mrefu kupinga wakala anayesambaza pembejeo pamoja na mfumo mzima wa Wetcu bila mafanikio.

Alisema wasambazaji wa pembejeo umepokonya majukumu ya vyama vya msingi na hivyo kumwongezea gharama mkulima zikiwamo za usafirishaji na uhifadhi.

“Jambo lingine baya ni kwamba wamekuwa wakisafirisha mbolea hewa ambazo baadaye wanawabambikizia wakulima, kwa hiyo madeni yanakuwa makubwa,” alisema.


Nkumba alisema hivi sasa, wakulima wamekubaliana na Wetcu kwamba madeni halali ndiyo yalipwe na kwamba wakulima ambao walilipia pembejeo bila kupelekewa, warudishiwe fedha zao.

“Wananchi wote hawataki mfumo huu unaotumiwa hivi sasa kuwapelekea pembejeo, lakini viongozi kule juu ndio wanaong’ang’ania…wamekuwa wakipewa ahadi ya kuletewa pembejeo wakati hawaletewi,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa muda wa bodi ya Wetcu, Hassan Wakasuvi, alipoulizwa kuhusiana na ufisadi huo alikiri kwamba kuna vyama vya msingi vinadai kwa kuwa vililipa fedha, lakini havikupelekewa pembejeo huku vingine vikikatwa misimu miwili bila kupelekewa pembejeo. “Vingine vilikatwa pesa hata mbolea haikuwafikia, vingine vinadai pembejeo lala yaani walilipa lakini hadi msimu wa kilimo unaisha hawajapata pembejeo.”

Alisema hivi sasa bodi hiyo inafanya ulinganifu ili kuwarudishia wakulima fedha zao.
Hata hivyo, Wakasuvi ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, alisema amekuwa kwenye wadhifa katika bodi ya Wetcu kuanzia Aprili hivyo ufisadi huo aliukuta.
“Deni hili linaweza kuzidi hata Sh. bilioni saba.”

Kwa upande wake, Kaimu Meneja Mkuu wa Wetcu, John Kusanja, alisema bodi inahakiki deni hilo ili wawalipe wakulima. Alisema “kuna vyama ambavyo vimelipa zaidi na vingine vililipa pungufu kwa hiyo anayedaiwa atalipa na anayedai atalipwa.”

Machi 23, mwaka huu, Mkutano Mkuu Maalumu wa Wetcu uliwasimamisha kazi wajumbe wa bodi kwa madai ya kutotekeleza majukumu yao ipasavyo baada ya ukaguzi kubaini kasoro mbalimbali za kiutendaji.
Taarifa ya ukaguzi ilibaini kuwa bodi ya Wetcu imeshindwa kusimamia utunzaji wa kumbukumbu hasa za hesabu na pia kutowachukulia hatua watumishi waliosimamishwa kazi na kuwaacha waendelee kulipwa mishahara wakati hawafanyi kazi.

Pia bodi hiyo ilikubali kuidhinisha malipo kwa wazabuni ambao hawakutoa huduma kama wasambazaji wa pembejeo na makandarasi wa ujenzi wa maghala.

Alisema kutokana na kasoro hizo na nyingine, athari zake ni kutoa mwanya kutokea kwa wizi ambao hatma yake ni wakulima kubebeshwa mzigo wa kulipa madeni yasiyo ya kwao.

Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, alipoulizwa kuhusiana na ufisadi huo alisema yuko kwenye mapumziko na kwamba asingeweza kuzungumza wakati huo.

Hata hivyo, NIPASHE ina taarifa kwamba Waziri Chiza alikuwa mkoani Tabora hivi karIbuni na alifanya mkutano Sikonge ambako suala la ufisadi wa tumbaku dhidi ya wakulima limepamba moto.

CHANZO: NIPASHE
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top