Bagamoyo
Spika
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anne Makinda amewataka
wajumbe wa Kamati za Hesabu za Serikali kuwa waadilifu katika utendaji
wao wa kazi ili fedha zinazotengwa kwenye Bajeti zitumike ipasavyo
katika kuleta maendeleo na hatimaye kumnufaisha kila mwananchi.
Akizungumza
leo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wiki moja ya kamati zinazohusika
na hesabu za Serikali wilayani Bagamoyo, Makinda amesema wabunge ndio
tegemeo kubwa la wananchi hivyo ni lazima wafanye kazi zao kwa ufanisi
na uadilifu mkubwa ili kuwanufaisha wapiga kura wao.
“Hili
neno bahasha, bahasha lisiwepo kabisa katika utendaji kazi wa wabunge,
na ni lazima wajumbe mkumbuke kuwa ninyi wabunge ndio tegemeo la
wananchi katika kusimamia ipasavyo fedha za Serikali”, amesisitiza
Makinda.
Amewashauri
wajumbe wa kamati hizo kufuatilia kwa makini matumizi ya fedha za
Serikali kwenye ofisi za wizara, idara, taasisi, na mashirika muhimu ya
Serikali ili ofisi hizo ziwe mfano kwa zingine.
Kamati
zinazopewa mafunzo hayo ni pamoja na Kamati ya Kudumu ya Hesabu za
Serikali (PAC), Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati
mpya ya Bajeti ambazo pamoja na mambo mengine zina jukumu la kusimamia
uhalali wa matumizi ya bajeti kwa kukagua kama fedha za Serikali
zimetumika kama zilivyokusudiwa.
Anne
Makinda amewaambia wajumbe wa kamati hizo kutumia fursa ya mafunzo hayo
kujifunza kwa makini kwa kuwa ukaguzi wa fedha unahitaji utalaamu ambao
utawasaidia kufanya kazi yao kwa ufanisi.
Baadhi
ya mada zitakazowasilishwa katika mafunzo hayo ni pamoja na nafasi ya
Bunge katika kusimamia matumizi na mapato ya Serikali, mbinu mbalimbali
zinazotumika kutathmini uhalisia wa matumizi ya fadha za umma, uhusiano
wa Bunge na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na
uendeshaji wa vikao vya kamati za uwajibikaji.
Post a Comment