Mfumuko
wa Bei wa Taifa kwa mwezi Agosti, 2013 umepungua hadi kufikia asilimia
6.7 kutoka asilimia 7.5 za mwezi Julai, 2013 kutokana na kupungua kwa
bei za bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.
Akitoa
taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu mfumuko wa bei wa Taifa kwa
mwezi Agosti 2013 leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Sensa na
Takwimu za Jamii Ephraim Kwesigabo amesema kupungua
kwa mfumuko wa Bei nchini kumechangiwa na kupungua kwa bei za Bidhaa
za Vyakula na Vinywaji Baridi kutoka asilimia 8.0 kwa mwezi Julai, 2013
hadi asilimia 6.5 za mwezi Agosti, 2013.
Kwesigabo
amefafanua kuwa kasi ya ongezeko la bei kwa bidhaa zisizo za vyakula
imebaki kuwa asilimia 7.3 kwa mwezi Agosti, 2013 kama ilivyokuwa mwezi
Julai, 2013.
“Kupungua
kwa Mfumuko wa Bei kunamaanisha kuwa, kuna unafuu wa maisha kwa mlaji;
kwa maana hiyo Tanzania inaonyesha kuwa inapiga hatua nzuri katika
uchumi wa nchi yetu”, amesema Kwesigabo.
Amezitaja
bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei kuwa ni
pamoja na mikate na nafaka (asilimia 2.2), vitafunwa (asilimia 3.8),
mahindi (asilimia 1.6), unga wa ngano (asilimia 2.5), unga wa muhogo
(asilimia 0.6), mtama (asilimia 3.4) na kuku wa kienyeji (asilimia 0.9).
Bidhaa
nyingine ni samaki wabichi (asilimia 2.6), karanga (asilimia 2.0),
mbogamboga (asilimia 2.4), nyanya (asilimia 9.9), vitunguu maji
(asilimia 2.0), viazi vitamu (asilimia 4.8), mihogo (asilimia 4.1) na
sukari (asilimia 0.5).
Bidhaa
zisizo za chakula zilizochangia kupungua kwa Mfumuko wa Bei ni pamoja
na; viatu (asilimia 0.3), samani (asilimia 0.1), vyombo vya udongo
(asilimia 1.0), na vifaa vya elekroniki vya kurekodia picha na sauti
(asilimia 0.3).
Wakati
huohuo Mkurugenzi Kwesigabo amesema kuwa thamani ya shilingi ya
Tanzania kwa mwezi agosti, 2013 imepanda ikilinganishwa na mwezi
septemba 2010.
Akitolea
mfano wa shilingi 100, Kwesigabo amefafanua kuwa uwezo wa Shilingi 100
ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umepungua hadi kufikia
Shilingi 71 na Senti 46 kwa mwezi Agosti 2013.
“Hii
inamaanisha kuwa, ili Mlaji aweze kununua bidhaa na huduma sawa na
alizokuwa akinunua kwa Shillingi 100 mwezi Septemba, 2010 atahitaji
Shilingi 28 na Senti 54 zaidi, yaani awe na Shilingi 128 na Senti 54
mwezi Agosti, 2013”, amesema Kwesigabo.
Mfumuko wa Bei nchini umeanza kuonyesha mwelekeo unaofanana na nchi jirani za Afrika mashariki hususani Kenya na Uganda.
Post a Comment