Dar es Salaam. Hali imeendelea kuwa tete ndani ya Jumuiya ya
Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM), huku jumuiya hiyo ikitengua
uteuzi wa wakuu watatu wa idara zake ambao walikataliwa na Baraza Kuu la
chombo hicho lililokutana hivi karibuni, Visiwani Zanzibar.
Wakati hayo yakiendelea kuna na taarifa kwamba
kumekuwa na mwendelezo wa harakati za kuandaa mkakati wa kumwondoa
madarakani mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Sadifa Juma Khamis na kwamba
vikao vya kupanga mkakati huo vilianza mara tu baada ya mkutano wa
Zanzibar.
Watendaji waliosimamishwa ni Wakuu wa Idara za
Oganaizesheni, Tumaini Mwakasege, Fedha na Uchumi, Omary Suleiman na
yule wa Idara ya Chipukizi na Uhamasishaji, Omary Justus.
Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda
alilithibitishia gazeti hili kung’olewa kwa watendaji hao na kwamba
kuendelea kwao na majukumu yao kutategemea iwapo watathibitishwa na
Baraza Kuu la jumuiya hiyo linalokutana mjini Dodoma Oktoba mwaka huu.
“Sisi tuliomba hawa wathibitishwe kwenye kikao
kijacho kwa kuwa kulitokea kidogo mkanganyiko wajumbe wakataka tujadili
suala hili kwenye Baraza Kuu lililopita lakini kwa kuwa tulikuwa na
ajenda moja tu ya kumthibitisha Katibu tukaomba suala hili lisogezwe
mbele,” alisema Mapunda.
Mapunda alisema tayari watendaji hao walikuwa
wameanza kazi lakini kutokana na baadhi ya kanuni kujikanganya, wameona
ni vyema waache suala hilo mpaka kwenye mkutano ujao.
“Kuna kanuni inayotoa mamlaka kwa Kamati ya
Utekelezaji na vilevile Baraza Kuu, kwa hiyo inabidi sasa tuweke kwanza
mambo sawa kisha kwenye Baraza Kuu la Oktoba, hawa watathibishwa,”
alisema.
Hata hivyo habari ambazo zimelifikia gazeti hili
zinasema si rahisi kwa wakuu hao wa idara kurejea kwenye nafasi zao,
kwani kitendo cha wajumbe kuwakataa katika kikao cha Zanzibar
kinathibitisha kwamba hawana imani nao.
“Kama wajumbe wa Baraza Kuu wangekuwa wanawaamini,
shinikizo lingekuwa ni kuwathibitisha, lakini sisi wajumbe ni kwamba
hatuwataki. Inabidi Sadifa na kamati yake ya utekelezaji watuteulie watu
wengine,” alisema mmoja wa viongozi wa UVCCM wa mikoa ambaye hakutaka
kutajwa jina lake.
Suala la uteuzi wa wakuu wa idara za UVCCM pia ni
mtihani wa kwanza kwa Katibu Mkuu mpya, Mapunda ambaye mara baada ya
kuthibitishwa alionja chungu ya mgogoro katika taasisi ambayo yeye ni
mtendaji mkuu wake, pale alipopingwa vikali na wajumbe, alipojaribu
kumtetea Sadifa.
Katika mazingira hayo, Mapunda anaweza kujikuta
katika mgogoro mkubwa zaidi na wajumbe wa Baraza Kuu, ikiwa atawasilisha
majina ya watu walewale waliong’olewa ili wapigiwe kura kwa ajili ya
kuthibitishwa. MWANANCHI
Post a Comment