Hivi
karibuni kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya watanzania dhidi
ya Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini Mhe. Prof Sospeter Muhongo
yakiongozwa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF)
ambae pia ni Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Bwana Reginald Mengi.
Malalamiko hayo ambayo yameendelea kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya
habari na kupelekea hata baadhi ya wahusika kutoka wizarani, Idara na
Mashirika yake kutakiwa kujibu na kutolea ufafanuzi malalamiko na tuhuma
hizo nzito dhidi yao. Moja ya vyombo hivyo ni gazeti la NIPASHE
linalomilikiwa na IPP media la tarehe 6 septemba, 2013 katika ukurasa
wake wa tatu kuna habari inasema “SERIKALI YAZIDI KUPUUZA USHAURI WA
TPSF” Inaeleza habari hiyo kuwa “ ..Wakati taasisi ya sekta binafsi
(TPSF) ikiishauri kuharakisha sera ya gesi badala ya ugawaji vitalu,
serikali imeendelea kupuuza ushauri huo na sasa kupitia Shirika la
maendeleo ya petroli Tanzania (TPDC) imetangaza rasmi kuharakisha suala
hilo kwa madai ya kuwahi ushindani wa masoko ulimwenguni..”
Lakini
TPDF nao katika gazeti la UHURU la jana Ijumaa katika ukurasa wake wa
tatu imeandikwa habari yenye anuani “MWENYEKITI TPDC: UBINAFSI
UNAWAPONZA WATANZANIA. ->wengi wanalalamika uwezo hawana,
->
Zabuni za vitalu mwezi ujao.” katika habari hiyo Mwandishi ameandika
kuwa “Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya
Petroli Tanzania (TPDC) , Michael Mwanda, amesema ubinafsi miongoni mwa
watanzania ndio unaowafanya washindwe kunufaika na fursa za kiuchumi
zilizopo nchini, zikiwemo mafuta na gesi. Mwanda alisema hayo jana
jijini Dar es salaam, alipokuwa akijibu moja ya maswali ya waandishi wa
habari juu ya malalamiko ya baadhi ya watanzania kuwa hawapewi nafasi
kushiriki katika utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi.”
Malumbano
hayo kupitia vyombo vya habari baina ya pande mbili yaani Mengi na IPP
yake na Muhongo na Mashirika yake ambayo yamedumu kwa muda, sasa
yanachukua sura mpya baada ya kuwepo kwa taarifa za chini chini kuwa
Mwenyekiti huyo wa TPSF na IPP ameandaa mpango wa kuwatumia vijana wa
Chama Cha Siasa cha Upinzani (CHADEMA) kufanya kongamano lenye maudhui
“rasilimali za nchi na manufaa kwa wazalendo” ambapo kongamano hilo
limepangwa kupewa airtime katika kituo maarufu cha television hapa
nchini cha ITV ambacho kinamilikiwa na IPP media lakini pia posho,
chakula na incentives mbalimbali zimepangwa kutolewa katika Kongamano
hilo.
Kama
ilivyo katika mkakati huo, lengo lililopo nyuma ya pazia la kongamano
hilo ni kutaka kuionyesha jamii kuwa Waziri na Wizara kwa ujumla haijali
maslahi ya wazawa na kwamba viongozi wakuu wa Wizara husika hawana
Utaifa wala Uzalendo (kwa maana ya upendo kwa Taifa) hivyo wanataka
kuzitumia nafasi zao ndani ya wizara katika kujitajirisha binafsi na
kufanya upendeleo kwa wawekezaji wageni ambao hawana manufaa ya moja kwa
moja katika maendeleo ya wananchi.
Madhumuni
ya andiko langu hili na kuvuta utafakari makini na wa wengi katika
suala hili ambalo kama hatua muhimu na za haraka hazitachukuliwa katika
kulikabili linaweza kuleta tafsiri hasi kwa jamii na hivyo kuwagawa na
kuwavuruga watanzania na hasa kuwafanya wapoteze imani na matumaini yao
kwa Serikali, Waziri, Wizara, Idara na Mashirika yaliyopewa dhamana ya
usimamizi wa rasilimali za nchi hii.
Naomba
ikumbukwe kuwa si mara ya kwanza kwa seke seke la aina hii kuzuka ama
kuzushwa chini ya uratibu na usimamizi wa Mzee Mengi. Na mara zote
amekuwa akitumia nguvu ya ushawishi wa vyombo vya habari anavyovimiliki
katika kutafuta kuungwa mkono na hata kuonyesha ubaya wa wabaya wake.
Ubaya, malumbano na mizengwe mingi ambayo huzalishwa na kusimamiwa na
Mzee wangu huyu asili yake ni Ubinafsi na kuguswa kwa maslahi ya
kiuchumi aliyonayo katika Sekta mbalimbali hapa nchini.
Hivi
karibuni kulizuka sekeseke mfano wa hili la sasa ambalo lilihusu
VING'AMUZI na kabla ya hapo TBC, UBINAFSISHAJI WA KILIMANJARO HOTEL,
SUALA LA YUSUPH MANJI, SHEIKH AL BASALEHE na katika migogoro yote hiyo
Mzee Mengi amekuwa akitumia vyombo vya habari katika kuwakandamiza,
kuwazushia, kuwatuhumu na hata kuwadhalilisha wapinzani wake. Nitaomba
wanajamvi wakumbuke kuwa Mwaka 2008 kulipokuwepo mgogoro baina ya Mzee
Mengi na Al Basalehe, Katika mgogoro huo Mzee mengi alimrubuni Ustadhi
Mmoja wa madrasa (jina linahifadhiwa kwa sababu za kimaadili) na
kuwatumia wanafunzi wa madrasa hiyo kutunga nyimbo za kaswida za
kumdhalilisha Sheikh Al Basalahe na kisha nyimbo hiyo kupewa airtime
katika kituo cha ITV, na kwa mfano kama huo akaitumia ITV kuwataja
washindani wake kiuchumi kuwa ni MAFISADI PAPA.
Sina
kumbukumbu kuwa alitumia vigezo gani kuwataja wapinzani wake hao
kibiashara kama mafisadi papa, ila kumbukumbu yangu inaniambia aliwataja
hadharani na kupelekea baadhi kumpeleka mahakamani na kumfungilia kesi
ambazo hata hivyo hazikupata airtime za kutosha kwenye vyombo vya habari
na hata mwisho wake haukuwa umefahamika kwa wengi.
Tukirudi
katika hoja yetu ya vitalu vya gesi ambavyo Mwenyekiti huyo wa IPP na
TPSF amekuwa akividai kwa hamu kubwa na kuwatuhumu Viongozi wa Wizara,
Wakuu wa Idara na Mashirika yanayohusu Rasilimali gesi na mafuta kuwa
hawana hata chembe ya Uzalendo na wabinafsi, nahofu nitaeleweka vibaya
kwa baadhi ya watu nikisema kuwa kauli hii haina uhalisia na si ya
kweli, na kwamba inalenga kuchochea hisia za chuki na imetolewa kwa
misingi ya Chuki, it's simply a hate speech that hate are produced.
Kwa
mujibu wa TPDC, kuchimba kisima kimoja kwa ajili ya kutafuta gesi na
mafuta katika nchi kavu ni dola za Marekani milioni 40 (Tshs. Bilioni
64) na kwa kina kirefu cha bahari ni dola 120 (Tshs Bilioni 190) na pia
ili kupata mafuta au gesi baada ya kupata uhakika, mwekezaji anapaswa
kuchimba visima vinne hadi vitano, hivyo inahitaji mwekezaji kuwa na
mtaji usiopungua dola za kimarekani milioni 600 ~ 800 kiasi ambacho
watanzania wengi hawana (MENGI akiwemo) na kwa Kauli ya Mwanda,
Mwenyekiti wa TPDC alisema kuwa Watanzania ili waweze kunufaika na
rasilimali hiyo, hawana budi kuungana na wabia wenye uwezo wa kimtaji na
teknolojia (Suala ambalo Mengi analipinga)
Tatizo
la kimsingi hapa ni Ubinafsi wa baadhi ya watu ambao wanataka upendeleo
kwa maslahi binafsi ya kibiashara kwa nembo ya uzalendo na uzawa.
Kumekuwepo na rekodi zenye kusikitisha ambazo zinaonyesha tatizo la
msingi linalowakabili hawa tycoon wetu katika mikopo waliyochukua katika
mabenki makubwa mbalimbali hapa nchini na hata nje ambapo bado
hawajarejesha mikopo hiyo na hivyo kutokopesheka tena kwa miradi mikubwa
kama hii ya vitalu vya gesi lakini pia zipo rekodi nyingine
zinazoonyesha wametumia mikopo kwa shughuli ambazo hawakuombea mikopo
hiyo ikiwemo mikopo kutoka benki ya kilimo (Takwimu zipo)
Kama
hayo ya mikopo hayatoshi, tayari Kampuni za Mzee Mengi zinashikilia
vitalu takribani 59 vya madini vyenye Ukubwa wa mita za mraba 3,752. 37
(sq km) na baadhi ya vitalu hivyo alivyovishikilia ameshindwa
kuviendeleza na matokeo yake Serikali inakosa mapato kutokana na
kutoendelezwa kwa vitalu hivyo lakini pia watanzania wanakosa ajira na
manufaa mengine, najiuliza kama hii ndio tafsiri ya UZAWA ambayo Mzee
Mengi anaizungumza, ama ni AINA nyingine ya UFISADI ambayo watanzania
walio wengi bado hawajaung'amua kwa kuwa vyombo vya habari haviandiki
wala kusema kuhusu habari hizi. Katika attachment ni orodha ya vitalu
mbalimbali vinavyomilikiwa na Kampuni za Mzee Mengi hapa nchini.
Tunaweza
kutofautiana katika mengine lakini katika yale yanayohusu mustakabali
wa nchi naomba watanzania tuungane na tuseme hapana. Matumizi ya Vyama
vya Siasa, wanasiasa na hata pressure group katika kutetea maslahi ya
baadhi ya tycoon wa hapa nchini ni hata nje ni katika makosa makubwa
ambayo yanaweza kutuletea madhara makubwa sana hasa kutokana na
rasilimali zilizopo hivi sasa hapa nchini. Nitoe ombi kwa Vijana hawa wa
Chadema, watambue nafasi yao kama vijana na Safari waliyonayo ya
kuijenga kesho yao na kusahau posho za siku moja na vyakula. Ni wakati
wa kusimamia haki na kuitetea kweli, hata ikiwa kweli hiyo inakinzana na
maslahi binafsi.
Chanzo: New Habari Blog
Post a Comment