*********
Ni vigumu kuzungumzia historia ya vuguvugu la uanzishaji makanisa nchini, pasipo kumtaja Askofu Moses Kulola.
Askofu Kulola anajulikana na wengi kama mtu aliye
na nia ya dhati kutangaza neno la Mungu, kutokana na kile kinachoonekana
wazi kwamba hakujilimbikizia mali kama ambavyo tunaona baadhi ya
watumishi wa Mungu siku hizi wanavyomiliki majumba, benki na hata magari
ya milioni ya shilingi.
Hali halisi
Kwa namna inavyoonekana nchini, ni kama kuna kundi
kubwa la watumishi wanaohubiri kwa lengo la kushibisha matumbo yao
zaidi; Hawana mpango thabiti wa kusaidia yatima wala maskini, badala
yake waumini ndio wanaonyonywa kwa kutoa zaka na sadaka ambazo baadhi
yake hata matumizi yake yamekuwa yakizua maswali.
Utumishi wa Mungu na mali
“Hakuna shaka kwamba kama kila nyumba ya ibada
Tanzania ingekuwa na mpango thabiti wa kusaidia watu maskini, yatima na
watu wengine wenye hali ngumu, hali ya maisha ingekuwa nzuri zaidi kwa
wengi. Lakini wapi, baadhi ya watumishi wako ‘bize’ kujaza matumbo,
wanaendesha magari ya kifahari yenye thamani ya mamilioni ya shilingi
badala ya kutumia fedha hizo kutangaza neno la Mungu au kusaidia
wasiojiweza,” anasema Charles Mtanga, mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam.
Mtanga anawashauri viongozi wa nyumba za ibada
kuwa na mkakati wa kusaidia yatima na watu wengine wasio na uwezo, huku
wakiendelea kutangaza neno la Mungu, ili wote waweze kuufurahia
ulimwengu.
Utanuzi wa huduma
Kwa mujibu wa Askofu wa EAGT Sengerema, Joshua
Wawa, Askofu Kulola alizaliwa Juni 2, 1928 katika Kijiji cha Nyahonge
wilayani Kwimba mkoani Mwanza. Ameacha mjane, watoto 10, wajukuu 44 na
vitukuu 16.
Katika uhai wake, Askofu Kulola alifungua makanisa
4,600 ya EAGT ndani na nje ya Tanzania, ikiwemo Zambia, Malawi, Rwanda
na Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC) na ameacha wosia kwamba makanisa
yafunguliwe kadiri inavyowezekana.
Hata hivyo, licha ya kuwa na wingi wote huo wa
makanisa, Askofu Kulola anamiliki nyumba moja iliyoko mkoani Mwanza
aliyojengewa na waumini. MWANANCHI
Post a Comment