Wakazi wa Mtwara wameshauriwa kujenga umoja na mshikamano ili kuona jinsi wanavyoweza kufanya maendeleo yao.
Akizungumza kwenye semina ya viongozi wanawake
Mkoa wa Mtwara juzi, Mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale-Mwiru,
aliwasihi wakazi wa Mtwara kuwa na umoja na mshikamano, kuona jinsi
watakavyofaidika na mradi wa gesi.
Hata hivyo, Kingunge hakutaka kuzungumzia zaidi
masuala ya gesi kwa kile alichokidai hana elimu nayo, hivyo kutaka
mjadala wa katiba uendelee bila kuingiliwa.
“Gesi siwezi kuizungumzia sana, ila ikitumika
vizuri itasaidia kusukuma mbele maendeleo ya watu, hivyo kinachotakiwa
ni sera ya uwezeshaji wananchi kuona jinsi watu watakavyoshiriki
kufaidika na gesi,” alisema.
Kingunge alisema hivi sasa watu wanajadili mambo
ya Serikali tatu na vyeo, hawafikirii na kuzungumzia mambo ya msingi
kama ufugaji, kuona jinsi wafugaji watakavyosaidiwa.
“Mjadala wa katiba uendelee, kwani walikofikia
watu sasa wanajadili vyeo na Serikali tatu hakuna mustakabali wa watu
kufikiria,” alisema Kingunge na kuongeza:
“Wanaacha kuzungumzia mambo ya msingi kama ufugaji
na kuangalia masuala ya ufugaji jinsi ya kuwasaidia wasihamehame na
kuwajengea mazingira mazuri ya kuendeshea ufugaji.”
Hata hivyo, Kingunge aliwabeza watu wanaodai
wananchi wa Mtwara ni wabinafsi, kwani wanaosema hivyo hawajui kama
wakati wa mapigano ya uhuru walivyofanya kazi kubwa.
“Siwaungi mkono watu wanaosema watu wa Mtwara ni
wabinafsi, hao hawajui kama wakati wa vita watu wa Mtwara ndiyo
waliofanya kazi kubwa kupigania uhuru,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Viongozi Wanawake Mtwara
Vijijini, Maimuna Lipungu, alisema lengo la semina hiyo ni kutoa mawazo
yao ya mwanzo kwa nafasi zao, angalau wapate elimu ili wananchi wajue
mradi huo utakavyowanufaisha. MWANANCHI
Post a Comment