Habari zilizopatikana mjini Dar es Salaam jana, zinasema ingawa Polisi wa Kimataifa, (Interpol), wamekamilisha kazi ya kumkamata na kumkabidhi mtuhumiwa kwenye vyombo vya usalama vya nchini Dubai, lakini taarifa zinasema taratibu za kimahakama nchini humo ndizo zinazochelewesha kurejeshwa nchini.
Mkuu wa Interpol Tawi la Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile, alipoulizwa na RAI juu ya kuchelewa kwa hatua hizo, alisema Polisi wa Kimataifa wamemaliza kazi yao na kusisitiza suala lililobaki liko mikononi mwa taratibu za mahakama za Dubai na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje Tanzania.
“Zipo taratibu za kimahakama zinashughulikiwa kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje, kuhakikisha mtuhumiwa anarejeshwa nchini, nadhani zikikamilika tu, atarejeshwa na kupanda kizimbani hapa,” alisema Babile.
Alex Massawe alitarajiwa kurejeshwa nchini tangu Agosti, mwaka huu, lakini hadi sasa taratibu hizo zinaonekana kugonga mwamba na haijafahamika mpaka sasa iwapo tayari amefikishwa mahamakani nchini Saudi Arabia kujibu makosa ya mauaji na kughushi yanayomkabili.
Awali Mkuu wa Interpol, Tawi la Tanzania, aliwahi kuiambia RAI kuwa taratibu za kumrejesha Massawe nchini zimekamilika na hakuna vikwazo vitakavyosababisha asiletwe kujibu tuhuma zinazomkabili.
Kamishna Babile alisema tuhuma zinazomkabili Massawe alizitenda akiwa katika ardhi ya Tanzania, hivyo ni lazima ajibu tuhuma hizo katika ardhi ya Tanzania.
Alisema taarifa za kupandishwa kizimbani, Massawe katika Mahakama ya Dubai, hazikuwa sahihi na kusisitiza hakuna mabadiliko katika taratibu zinazofanywa kumrejesha kujibu tuhuma zake.
“Process zinaendelea vizuri, kamwe hamna mabadiliko wala vikwazo, katika kipindi cha mwisho wa mwezi huu, anaweza kuwa nchini,” alisema Kamishna Babile.
“Makosa yote aliyafanya Tanzania, kwa hiyo kamwe hawezi kushitakiwa kwingineko, kama atashitakiwa itakuwa ni Tanzania tu,” alisema Babile.
Juzi kulikuwa na taarifa kwenye baadhi ya vyombo vya habari nchini, zilizodai, mfanyabiashara huyo amefikishwa katika mahakama ya Dubai, akikabiliwa na tuhuma za mauaji, baada ya Polisi wa Kimataifa (Interpol), kuiomba Serikali ya nchi hiyo kumkamata.
Massawe anayefanya biashara zake katika miji ya Arusha, Moshi na Dar es Salaam, alikamatwa kati ya Juni, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai, akitokea Afrika Kusini.
Akiwa Dubai, Massawe alikutwa na pasi tatu bandia za kusafiria zilizokuwa na majina tofauti.
“Hawezi kuhukumiwa kule, kwa sababu hawezi kufunguliwa mashitaka Uarabuni kwa makosa aliyoyafanya Tanzania,” alisema Babile katika ujumbe mfupi wa simu ya mkononi.
Nayo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, iliwahi kuthibitisha kuwa taratibu za kumrejesha nchini, Massawe zimekamilika na kuongeza taratibu hizo zinafanywa kwa karibu mno kati ya Jeshi la Polisi Tanzania, Polisi wa Kimataifa (Interpol) na Serikali ya Dubai.
Massawe, anatuhumiwa kufanya uhalifu mbalimbali, ikiwamo kughushi nyaraka mbalimbali na tayari Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mjini Dar es Salaam, imetoa hati ya kukamatwa na kurejeshwa nchini ili kukabiliana na kesi mbili.
KAULI MAMBO YA NJE
Katika Hatua nyingine, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imesema haina taarifa zozote juu ya kuchelewa kuletwa nchini kwa Massawe kujibu tuhuma zinazomkabili.
Msemaji wa wizara hiyo, Mkumbwa Ali aliiambia RAI jana kuwa taratibu zote za kurejeshwa Massawe ziko mikononi mwa mahakama.
Hata hivyo, Ali aliahidi kufuatilia suala hilo kwa ukaribu na kutoa majibu leo.
MWANANCHI


Post a Comment