Mtwara. Watuhumiwa 11 wa ugaidi waliokamatwa wakifanya mafunzo ya
kijeshi yenye asili ya kigaidi msituni Wilaya ya Nanyumbu, Mtwara
wamefikishwa katika mahakama ya Mkoa Mtwara na kufunguliwa upya mashtaka
baada ya kesi yao ya awali kuondolewa katika mahakama ya Wilaya ya
Nanyumbu.

Akisoma mashtaka, Wakili wa Serikali Mfawidhi Mtwara, Ladislaus Komanya
alisema shauri hilo limesomwa upya baada ya kuhamishiwa Mahakama ya Mkoa
kutoka Mahakama ya Wilaya.
Komanya alisema washtakiwa wote wanakabiliwa na makosa mawili.
Kwa mujibu wa wakili huyo, kosa la kwanza ni kuwa, kati ya Septemba 21
na 26 mwaka huu wanadaiwa kufanya mkusanyiko usiokuwa halali wenye lengo
la uvunjifu wa amani.
Shtaka la pili ni kufanya uchochezi, ambapo Septemba 26 mwaka huu Wilaya
ya Nanyumbu kwenye msitu walikutwa na machapisho ya kanda za cd zenye
video za uchochezi hali iliyowapelekea watu kujengea hofu.

Watuhumiwa 11 wa ugaidi waliofikishwa katika mahakama ya Mkoa Mtwara
Mahakama ilielezwa kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyingine ya kusikilizwa.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mtwara, Dynes Lyimo alisema dhamana ipo
wazi kwa kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wakazi Mtwara watakaosaini
mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh5 milioni mmoja kati yao awe ni
mtumishi wa Serikali ama taasisi inayotambulika na awe na barua ya
utambulisho toka kwa mtendaji wa Serikali ya Mtaa anakoishi.
Hakimu wa mahakama hiyo aliahirisha kesi hiyo na kusema kuwa itatajwa tena Novemba 11 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Stephen Zelothe alisema
kuwa watuhumiwa wengine wawili walikamatwa na kifikia adadi ya watu 13
na kwamba uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.
Chanzo - Mwananchi


Post a Comment