Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

CCM YAHOFIA 2015

Makamu Mwenyekiti wa CCM taifa (Zanzibar), Dk. Ali Mohamed Shein
*Mbio za urais, ubunge zamshtua Dk. Shein
*Akemea wanaojipitisha, asema dawa yao inachemka

MBIO za urais za mwaka 2015, zimeonekana kukipa wakati mgumu Chama Cha Mapinduzi (CCM), hatua inayofanya baadhi ya viongozi wake kutokulala usingizi. Mbio hizo ambazo zinavuta hisia za wengi, zimefikia pabaya kiasi cha kukifanya chama hicho kukumbwa na hofu ya mpasuko, iwapo nidhamu ya wanachama wake haitadhibitiwa.

Hofu hiyo imekolezwa jana na Makamu Mwenyekiti wa CCM taifa (Zanzibar), Dk. Ali Mohamed Shein alipokuwa akizungumza na makatibu wa chama hicho wa wilaya na mikoa mjini Dodoma.

Katika hotuba yake, Dk. Shein aliwapiga marufuku makatibu hao kujihusisha na watu ambao wameanza kujiandaa kugombea urais, ubunge na udiwani katika uchaguzi huo.

Mbali na hilo, Dk. Shein pia aliwaonya wanachama wanaoanza harakati hizo mapema za kuwania nafasi hizo, kwa kuwa viongozi waliopo bado hawajamaliza muda wao kikatiba.
Dk. Shein ambaye pia ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, alitoa onyo hilo katika ufunguzi wa mafunzo ya watendaji na viongozi wa CCM ngazi ya mikoa na wilaya yaliyoanza jana katika ukumbi wa White House mjini hapa.

Alisema makatibu au viongozi wa CCM, watakaojihusisha na watu hao, hawafai kwa kuwa tabia hiyo inakichafua chama na kwamba watakaobainika kushindwa kujirekebisha wanapaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Alisema baadhi ya wanachama wa CCM wenye nia ya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wameanza harakati za kutaka kugombea na kuanza kujipitisha maeneo waliyoyalenga.

“Kutokana na sifa zenu za kukitumikia chama chetu, msijihusishe na watu hao hata kwa kuwa karibu na wale wanaojiandaa na urais, ubunge na hata udiwani.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yupo na ana muda wake bado, Rais wa Zanzabar bado yupo na muda wake kikatiba haujaisha, wabunge na wawakilishi nao bado wapo na madiwani nao muda wao haujamalizika.

“Wakati ukifika sote tutaarifiwa nini cha kufanya, tuwape nafasi viongozi tuliowapa dhamana ya uongozi watekeleze na kusimamia ilani ya uchaguzi wengine kazi yao iwe ni kushirikiana nao katika utekelezaji wake,” alisema.

Alisema mafunzo hayo yatakapomalizika yawe yametoa somo la kutosha kwa watendaji kuacha kuwa wapambe, yaani kuwaunga mkono wale wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali.

Alisema taratibu za kiutawala, makatibu kazi yao ni utendaji na kutoa ushauri wa kitaalamu kwenye vikao na kwamba haileti sura nzuri kila wakati shutuma za kuvuruga mchakato wa uchaguzi katika mikoa na wilaya zielekezwe kwao.

“Makatibu ni viongozi mahiri na wenye dhamana nzito na mnaozijua kazi zenu, lawama si stahili yenu mnastahili sifa wakati wote,” alisema.

Dk. Shein pia alizungumzia maadili kwa viongozi wa CCM na kwamba watendaji wenye vitendo vya kuichafua CCM wazingatie nidhamu na wajirekebishe.

“Muda wa kujirekebisha bado upo, milango haijafungwa, najua kumaliza chuya kwenye mchele huchukua muda, wahenga wanasema ‘ndege wa rangi moja huruka pamoja’ kwa hiyo asiyependa kwenda na mwendo wa CCM atupishe njia tuendelee na safari yetu ya ushindi,” alisema.

Alisema CCM haiwezi kushinda uchaguzi wowote kama hakuna uadilifu, uaminifu na nidhamu miongoni mwao.

Akizungumzia suala la mchakato wa uundwaji wa Katiba Mpya, Dk. Shein alisema mawazo ya baadhi ya watu wanaodai kwamba CCM inataka kuhodhi mchakato wa Katiba kwa sababu ya hofu ya kushindwa uchaguzi, ni mawazo ya wafa maji.

Alisema CCM ilichofanya ni kuwasilisha maoni ya wanachama wao katika Tume ya Kukusanya Maoni na kwamba yalikuwepo mapendekezo mengi ya wanachama yaliyotofautiana na yaliyomo kwenye rasimu.

“CCM haijawahi kutamka kwamba tunataka maoni yetu ndiyo yachukuliwe na Tume ila chama chetu kitaendelea kuheshimu maoni ya Watanzania wote, kupitia kura ya maoni wakati ukifika.

“Wenzetu badala ya kukusanya maoni kwa wanachama wao na kuyawasilisha katika Tume, wamekuwa wakifanya mikutano ya hadhara eti ndio wanakusanya maoni, mwenendo huo ni kinyume na maelekezo ya Tume iliyoundwa kisheria.

“Hivi sasa walipotufikisha sote tunajua, nimesema hili kwa kuwa mjadala unaoendelea sasa usipotolewa ufafanuzi mapema, utachelewesha kupata Katiba Mpya katika muda tuliojipangia na utawafanya Watanzania waingie katika malumbano yasiyo na haja wala hoja,” alisema.

Dk. Shein pia alizungumzia umuhimu wa chama hicho kujitegemea na kuachana na kutegemea wafadhili au wahisani katika kukiendesha.

“Sio jambo la kupendeza kwa chama kikubwa na cha siku nyingi kama CCM chenye wanachama zaidi ya milioni sita kushindwa kuendesha shughuli zake kwa kukosa fedha.

“Nafahamu kila wilaya inazo fursa ambazo, tukizitumia vizuri ni wazi tutaondokana na utegemezi, lazima tuwe wabunifu wa kutafuta vyanzo endelevu vya kupata fedha kwa ajili ya shughuli za chama chetu,” alisema Dk. Shein.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema lengo la semina hiyo ya siku nne kwa viongozi na watendaji hao, ni kuimarisha chama hasa katika ngazi za wilaya, matawi na mashina.

Pia Kinana alisema semina hiyo itawajengea uwezo viongozi hao kufanya kazi kwa ujuzi na ufanisi na kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 baadaye.

Kauli ya Dk. Shein imeakisi taarifa zilizoandikwa katika vyombo vya habari vikimnukuu Rais Jakaya Kikwete kwamba aliruhusu wanachama kupita pita, huku akiwataka wachukue tahadhari dhidi ya vishoka wa siasa.

Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM taifa, alidaiwa kutoa kauli hiyo wakati akiongoza kikao cha Halmashauri Kuu (NEC), kilichofanyika Juni mwaka huu mjini Dodoma.

Taarifa hizo ambazo siku moja baadaye zilikanushwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, zilibainisha kuwa Rais Kikwete alionya hatakati za kujipitisha zisije zikaathiri kwa kujenga makundi hasi yatakayoweza kukipasua chama.
MTANZANIA
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top