Msajili Mkuu wa Mahakama ya Kenya, Gladys Shollei amefukuzwa
kazi kwa madai ya utovu wa nidhamu na kuwadharau makamishna wa Tume
inayosimamia idara hiyo (JSC).
Shollei ndiye aliyemwapisha Rais Uhuru Kenyatta alipoingia madarakani mwaka huu.
Kwenye taarifa ya uamuzi huo iliyosomwa na Jaji
Mkuu Willy Mutunga mwishoni mwa wiki, JSC ilitoa sababu tano za
kumsimamisha kazi Shollei, ambapo msajili huyo alishutumiwa kwa kukosa
maadili.
“Baada ya kusoma madai yote yaliyomkabili msajili
mkuu wa mahakama na baada ya kusoma majibu yake, ikizingatiwa kwamba
aliamua kujitokeza mbele ya tume, tumeamua kwa pamoja kumsimamisha kazi
mara moja,” alisema Jaji Mutunga.
Kwa hatua hiyo, Shollei anakuwa msajili mkuu wa
Mahakama wa kwanza kufutwa kazi tangu Idara ya Mahakama ifanyiwe
marekebisho ili kuafiki matakwa ya Katiba ya sasa.
Aidha, ni ofisa wa pili wa ngazi ya juu kwenye
idara hiyo kupigwa kalamu, baada ya aliyekuwa Naibu Jaji Mkuu, Nancy
Baraza kufutwa mwaka jana.
Akielezea uamuzi huo, Jaji Mutunga alitaja ukosefu
wa nidhamu, ukiukaji wa kanuni za kazi za maofisa wa mahakama, ukiukaji
wa sura ya sita ya Katiba inayohusu maadili na kukaidi maagizo ya
wakubwa wake, kama sababu zilizosababisha JSC kumsimamisha kazi Shollei.
“Kutokana na uzito wa masuala yaliyosababisha
kusimishwa kazi kwa Shollei, JSC inaialika Tume ya Maadili na Kupambana
na Ufisadi (EACC) ifanye uchunguzi wa kina kuhusu masuala haya,” alisema
Jaji Mutunga.
“Madai yaliyotolewa kumhusu Shollei ni mazito
sana. Pesa zinazohusishwa katika madai hayo ni Sh2.207 bilioni.
Amekubali madai 33 ambapo Sh1.7 bilioni pesa za walipa ushuru ziko
katika hatari ya kupotea. Amekataa madai 38 ambayo yanafikia Sh250
milioni ilhali majibu yake kuhusu Sh361 milioni yanakanganya,” alisema.
Jaji Mutunga alisema kuwa JSC imeweka madai yote
yanayomkabili Shollei, majibu yake na matokeo ya uchunguzi uliofanywa na
JSC katika tovuti yake.
Mwezi uliopita, Shollei aliiandikia barua JSC
akiifahamisha kwamba yuko tayari kufika mbele yake kuanzia Oktoba 15,
kujibu madai dhidi yake.
MWANANCHI
MWANANCHI
Post a Comment