Siku moja baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuomba
kuongezewa muda, Mnadhimu wa Chadema, Tundu Lissu (pichani) amesema Tume
haijakosea kuomba muda kwani kifungu cha 8 (4) cha Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba kinaeleza kuwa wanaweza kuomba muda wa miezi miwili zaidi.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeomba kuongezewa
mwezi mmoja kukamilisha majukumu yake, ambayo awali ilikuwa yakamilike
Novemba Mosi na sasa yatakamilika Desemba Mosi.
Lissu alisema lakini huku akihadharisha kuwa
kitendo cha kuongeza muda ni wazi Bunge la Katiba halitakutana Novemba
mwaka huu kutokana na mambo ya msingi kutokuwa yamepatiwa ufumbuzi. Kwa
upande wake, Katibu Mkuu wa NCCR- Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema hakuna
tatizo kwa Tume kuomba kuongezewa muda.
Mkurugenzi wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape
Nnauye alisema hawezi kuzungumza lolote hadi pale atakapolifikisha
katika ngazi husika. Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Bashiru Ally alisema kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuomba kuongezewa
muda, kunaashiria kuna matatizo katika mchakato mzima wa Katiba, licha
ya sheria ya Mabadiliko ya Katiba inaruhusu tume kuongezewa muda.
MWANANCHI
Post a Comment