CHINA imeahidi kuleta nchini Tanzania watalii 30,000 katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwakani.
******
Ahadi
hiyo imetolewa leo asubuhi (Jumapili, Oktoba 20, 2013) na Mwenyekiti wa
Wakala wa kutoa huduma za usafiri wa China na Hong Kong (China Travel
Services – Hong Kong Limited – CTS) Bw. Zhang Xuewu alipofanya
mazungumzo na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jijini Shenzen, China.
Alisema
kampuni yake itawandaa mawakala wa usafirishaji watalii ili kuhakikisha
kuwa watalii 10,000 wanapatikana kila mwaka ambao kiu yao ni kuja
Tanzania. “Wengi wanapenda kutembelea mbuga, lakini hapa nchini wamezoea
kuona walio sakafuni, wakija watawaona wanyama live” (akimaanisha kuwa Wachina wamezoea kuona wanyama wa sanamu kwenye makumbusho yao hapa jiji la Shenzen).
Waziri
Mkuu ambaye yuko katika siku ya tano ya ziara yake ya kikazi ya siku
tisa kwa mwaliko wa Serikali ya China alisema haelewi ni kwa nini
kampuni hiyo imeweza kupeleka watalii Afrika Kusini na nchi jirani za
Afrika Mashariki wakati haina urafiki nazo lakini imeshindwa kuwaleta
Tanzania kwenye ambayo ina mahusiano mazuri na ya muda mrefu.
Akizungumza
na Bw. Xuewu pamoja na baadhi ya viongozi kutoka Tanzania alioambatana
nao, Waziri Mkuu alisema amepewa maelekezo rasmi na Rais Jakaya Kikwete
ya kufuatilia suala la watalii wa kutoka China hasa ikizingatiwa kwamba
mazungumzo ya jambo hili yalianza wakati wa Rais wa awamu ya tatu, Bw.
Benjamin Mkapa.
“Katika bara la Afrika hakuna nchi yenye vivutio lukuki kama Tanzania. Na tovuti ya www.safaribooking.com
imeitangaza Tanzania kuwa nchi inayofaa kwa safari za mbugani kama mtu
anataka kuona vivutio vizuri na vya asili. Sasa ni kwa nini hatupati
watalii wa kutosha na tunafanyaje ili kubadilisha hali hiyo?,” alihoji.
Alisema
njia mojawapo ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na ndege ya moja moja
kutoka miji ya China hadi Dar es Salaam jambo alisema litasadia
kupuinguza kero kwa wasafiri ambao hivi sasa inabidi waunge safari mara
mbili hadi tatu ili kufika Tanzania. “Tuangalie uwezekano wa kuwa na
ndege ya moja kwa moja kutoka China hadi Dar es Salaam au Arusha…
wenzetu Kenya na Afrika Kusini wameweza kupata watalii wengi sababu wana
ndege za moja kwa moja,” alisema.
Alimshawishi
Mwenyekiti huyo aangalie pia uwezekano wa kujenga mahoteli katika mikoa
ya Tanzania ili kupunguza uhaba wa vyumba punde watalii wakianza
kufurika. Pia alimhakikishia fursa ya kujenga uwanja wa gofu chini ya
mlima Kilimanjaro kwani yote mawili ni maeneo ambayo kampuni yake inao
uwezo wa kufanya kama sehemu ya majukumu yake.
Pia
alimpa wazo kwamba kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya urafiki
baina ya Tanzania na China, CTS inaweza kuandaa kundi kubwa la wakala
wakaja Arusha na kufanya mkutano wa siku mbili au tatu na kisha wakapata
fursa ya kujadili namna ambavyo Tanzania na China zinaweza kushirikiana
kukuza suala la utalii. “Mkimaliza mkutano wenu mnasaini makubaliano
baina yenu na Bodi ya Utalii, mambo yanasonga mbele,” aliongeza.
Kwa
upande wake, Bw. Xuewu alikiri kuwepo kwa mazungumzo ya wakuu wa nchi
akisema: “Mwaka 2004, Rais Hu Jintao alifikia makubaliano na Rais
(Benjamin) Mkapa kwamba watafungua milango ya utalii kwa Tanzania. Mwezi
Machi, 2013, Rais Kikwete na Rais wa China, Bw. Xi Jinping walirudia
tena mazungumzo hayo na kukubaliana kuwa Tanzania itapewa kipaumbele cha
pekee kwa watalii wa kutoka China. (agreed to make Tanzania a leading
destination for Chinese tourists).
“Na
hata wewe na Waziri Mkuu wetu, Bw. Li Keqiang, mwezi huu (juzi)
mmeshuhudia mawaziri wakisaini makubaliano kuhusiana na suala hilo, kwa
kweli kama Serikali mmedhamiria kuhakikishia kuwa mnainua viwango vya
utalii ili kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa Watanzania,” alisema.
Alimshukuru
Waziri Mkuu kwa wazo lake kuhusu mkutano na MoU na kumhakikishia kuwa
wako tayari kujenga hoteli, viwanja vya gofu, kuanzisha tawi la kampuni
yao ya uwakala kama ambavyo Waziri Mkuu amewasahauri.
Katika
ziara hiyo, Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Nchi, (OWM) Uwezeshaji
na Uwekezaji, Dk. Mary Nagu; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah
Kigoda; Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe; Waziri wa Uvuvi na
Mifugo wa Zanzibar, Bw. Abdallah Jihad Hassan na Naibu Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Juma Maalim.
Pia
amefuatana na Balozi wa Tanzania nchini China, Luteni Jenerali (Mst.)
Abdulrahaman Shimbo, Wakuu wa mikoa ya Mtwara, Shinyanga na Simiyu;
wabunge wawili, Bw. Godfrey Zambi (Mbozi) na Dk. Titus Kamani (Busega),
Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji, Bibi Julieth Kairuki na viongozi wa
Tanzania Private Sector Foundation, Bw. Salum Shamte na Bw. Godfrey Simbeye.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, OKTOBA 20, 2013



Post a Comment