Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki
******
Aliyekamatwa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Aggrey Kalolo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Deusidedit Nsimeki, alithibitisha kukamatwa kwa Kalolo kuhusiana na tuhuma za ujangili, lakini amekataa kueleza kwa undani tukio hilo kwa maelezo kuwa kuwa lipo kwenye kampeni maaalum ya kitaifa na kwamba alilamatwa siku kadhaa zilizopita na kuachiwa kwa dhamana juzi baada ya mahojiano.
Kamanda Nsimeki alisema kuwa kutokana na hali hiyo yeye siyo msemaji kwa kuwa kampeni hiyo inashirikisha vyombo vingine vya dola, hivyo hawezi kulizungumzia tukio hilo zaidi mpaka hapo wakubwa watakapotoa ripoti ya jumla kuhusiana na matukio mbalimbali ya ujangili mkoani Ruvuma.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Robert Manumba, alisema hana taarifa zozote kwa kuwa yuko nje ya nchi na kumtaka mwandishi kuwasiliana na wahusika wengine.
Hata hivyo, hakuna kiongozi mwingine wa makuu ya Jeshi hilo aliyepatikana jana kutoa maelezo.
Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Senso na Naibu Mkurugenzi Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya Jinai, Isaya Mungulu, simu yao ziliita bila majibu.
Katibu wa CCM mkoa wa Ruvuma, Verena Shumbusho, alipotafutwa na NIPASHE ili atoe ufafanuzi kuhusiana na tukio la kukamatwa kwa kada wao kuhusiana na tuhuma za ujangili, alisema yuko nje ya mkoa kwa shughuli za kikazi na hafahamu lolote zaidi ya kusikia kukamatwa kwake.
Shumbusho alishauri watafutwe viongozi wenginewa CCM walioko mkoani Ruvuma kwa kuwa ndio wanaweza kulizungumzia vizuri jambo hilo.
Alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo, Kalolo alithibitisha kukamatwa na Jeshi la Polisi na kufafanua kwamba baada ya kupekuliwa nyumbani kwake hakukutwa na kitu chocho kinachoonyesha ushahidi juu ya tuhuma hizo.
Hivi karibuni wanyamapori hususani tembo wamekuwa wakiuawa kwa kasi na kutishia sekta ya utalii mchini.
Takwimu zinaeleza kuwa takribani tembo 30 wanauawa kila siku katika hifadhi za taifa na katika mapori ya akiba.
Wiki kadhaa zilizopita, baadhi ya magazeti yalichapisha habari kuhusiana na kasi kubwa ya ujangili hususani mauaji ya tembo zikiwataja kwa majina baadhi ya wafanyabiashara na wanasiasa wanaotuhumiwa kuhusika na vitendo vya ujangili.
Tayari Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amekwisha kusema kuwa wizara yake imeandaa operesheni maalum ya kuwaangamiza majangili huku akivitaka vyombo vya dola kuwaangamiza majangili hao kwenye mbuga badala ya kuwakamata.
Aidha, Rais Jakaya Kikwete alisema kuwa ataliamrisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuingilia kati vita dhidi ya ujangili.
Imeandikwa na Gideon Mwakanosya, Songea; Richard Makore na Gwanaka Alipipi, Dar.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment