Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko
wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Crescentius Magori, akifafanua
jambo mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu wa tano wa wadau wa NSSF, uliofanyika
mwishoni mwa wiki jijini Mwanza.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Injinia Evarist Ndikilo (wa tatu kushoto), Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Crescentius Magori (wa pili kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Mkutano Mkuu jijini Mwanza.
Na Sitta Tumma, Mwanza
MFUKO
wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umetenga zaidi ya sh. Bilioni 72.8
kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa hoteli ya kitalii,
itakayokuwa na nyota tano katika jiji la Mwanza.
Mbali
na mradi huo, NSSF pia imekusudia kuanza ujenzi wa nyumba 500 kwa ajili
ya kuuza kwa wananchi na wanachama wa mfuko huo, ikiwa ni lengo la
kuinua uchumi wa jamii na taifa kwa ujumla.
Kauli
hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi wa Utekelezaji wa NSSF, Crejcentius
Magori, wakati alipozungumza kwenye mkutano mkuu wa tano wa wadau wa
NSSF, uliofanyika ukumbi wa JB Belmont hoteli jijini Mwanza,
uliowashirikisha maofisa wa migodi ya madini nchini.
Alisema
kwamba, mkakati wa Mfuko huo wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii ni kuona
jamii, wanachama wake na taifa zima wananufaika na kazi zake, na kwamba
tayari mradi wa kitegauchumi hicho cha hoteli mkandarasi wake yupo eneo
la mradi.
"NSSF imedhamiria kuwekeza zaidi katika miradi mingi ya kiuchumi hapa Mwanza, Kanda ya Ziwa na maeneo mengine nchini.
"Kwa
sasa tumetenga bilioni 72.8 kwa ajili ya kujenga hoteli ya nyota tano
hapo Capri-Point jijini Mwanza. NSSF pia tuna mpango wa kujenga nyumba
500 za wanachama wetu na jamii," alisema Mkurugenzi Magori.
Kwa
upande wake, Meneja Mipango na Uwekezaji wa NSSF, Mseli Abdallah
alieleza kwamba, mradi wa ujenzi wa nyumba upo katika hatua ya michoro,
na kwamba ujenzi wa hoteli hiyo ya nyota tano utasaidia sana kukuza
uchumi wa jiji la Mwanza.
Kwa
mujibu wa Abdallah, NSSF imedhamiria pia kuwekeza miradi mbali mbali ya
kiuchumi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, na kwamba kwa sasa kuna mradi
wa jengo la kitega uchumi linajenga mjini Shinyanga.
Naye
Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Injinia Evarist Ndikilo (RC), ambaye ndiye
aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, aliwataka waajiri wote kulipa
michango ya wafanyakazi wao katika mifuko ya jamii.
Alisema
kwamba, kuna baadhi ya waajiri wamekuwa wakishindwa kutekeleza wajibu
huo wa kulipa michango hiyo, na kutoa onyo kuwachukulia hatua za
kisheria wale wote watakaoshindwa kutekeleza suala hilo.
Aidha,
aliupongeza uongozi wa Mfuko huo wa Taifa wa Hifadhi ya Jami kwa
mikakati yake ya uwekezaji nchini, kwani kazi hiyo inachangia maradufu
kuimarika kwa uchumi wa jamii na taifa zima.


Post a Comment